Putin awaandikisha wanaume 160,000 katika jeshi la Urusi

Rais Vladimir Putin amewaita wanaume 160,000 wenye umri wa miaka 18-30, idadi kubwa zaidi ya walioandikishwa jeshini nchini Urusi tangu 2011.

Muhtasari

Moja kwa moja

Abdalla Seif Dzungu

  1. Tumefika tamati ya taarifa zetu kwa leo... Asante!

  2. Rais wa Zambia aagiza mawaziri kuacha kulala kwenye baraza la mawaziri

    Hakainde Hichilema

    Rais wa Zambia Hakainde Hichilema amewaonya mawaziri tabia ya kusinzia wakati wa mikutano, akieleza ukosefu wao wa usikivu na "kujiachia" na kutojidhibiti.

    "Katika baraza la mawaziri mtu analala saa 10, swali ni walikuwa wapi... kama unaweza kuanza kudanganya huko? Kwangu mimi huo ni uhalifu, uhalifu mbaya," Hichilema alisema wakati wa hafla ya kuapishwa kwa waziri mpya.

    Hakueleza alichomaanisha hasa kwa "kujifurahisha" lakini vyombo vya habari vya nchini vimefasiri hili likirejelea unywaji pombe kupita kiasi na karamu za usiku.

    Rais alionya kuwa tabia hiyo inahatarisha kufichua siri za serikali na kuchelewesha utoaji wa huduma kwa umma.

    "Nimeshauri baraza la mawaziri kwamba lazima tujihusishe. Unapokuwa katika ofisi ya umma lazima uwe na... kujidhibiti, sio kujifurahisha kupita kiasi," rais aliongeza.

    Akitoa mfano wa Biblia, alionya tabia hiyo inaweza kusababisha kujiangamiza.

    "Kwa hiyo unashiriki vipi katika mkutano unapolala? Ujumbe uko wazi kabisa: hupendi mashauri ya baraza la mawaziri kwa niaba ya Wazambia. Kwa hivyo kwa nini unakaa hapo?" Aliuliza.

  3. Putin awaandikisha wanaume 160,000 katika jeshi la Urusi

    Wanajeshi

    Rais Vladimir Putin amewaita wanaume 160,000 wenye umri wa miaka 18-30, idadi kubwa zaidi ya walioandikishwa jeshini nchini Urusi tangu 2011, huku nchi hiyo ikipiga hatua ya kupanua ukubwa wa jeshi lake.

    Kuitwa kwa jeshi la majira ya kuchipua kwa huduma ya kijeshi ya mwaka mmoja kulikuja miezi kadhaa baada ya Putin kusema Urusi inapaswa kuongeza ukubwa wa jumla wa jeshi lake hadi karibu milioni 2.39.

    Imeelezwa kuwa wanajeshi hao wapya hawatatumwa kupigana nchini Ukraine kwa kile Urusi inachokiita "operesheni maalumu ya kijeshi".

    Hatahivyo, kumekuwa na ripoti za askari waliouawa katika mapigano katika mikoa ya mpaka wa Urusi na walitumwa kupigana huko Ukraine katika miezi ya mwanzo ya vita.

    Rasimu ya sasa, ambayo inafanyika kati ya Aprili na Julai, inakuja licha ya majaribio ya Marekani ya jitihada ya usitishaji vita.

    Hakukuwa na utulivu katika ghasia hizo siku ya Jumanne, huku Ukraine ikisema kwamba shambulio la Urusi kwenye kituo cha umeme katika mji wa kusini wa Kherson limewaacha watu 45,000 bila umeme.

    Urusi pia ilidai kuteka kijiji kingine cha Kiukreni, huko Rozlyiv katika mkoa wa Donetsk.

    Unaweza kusoma;

  4. Ghadhabu nchini Somalia baada ya mwanamume kukiri kuwa alioa mtoto wa miaka minane

    h
    Maelezo ya picha, Tukio hilo limezusha maandamano katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu

    Kuna hisisa za Ghadhabu nchini Somalia baada ya mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minane, ambaye alikuwa ametoweka kwa miezi sita, kupatikana akiishi na mwanamume aliyesema kuwa ni mumewe.

    Msichana huyo aliripotiwa kutoweka na familia yake katika eneo lililojitangazia uhuru wake la Puntland Septemba mwaka jana.

    Miezi kadhaa baadaye, taarifa ziliibuka kuwa baba yake msichana huyo aliruhusu mtoto huyo aolewe na mtu mzima aliyeitwa Sheikh Mahmoud.

    Vikosi vya usalama viliizingira nyumba ya mwanamume huyo wiki iliyopita na kulazimisha kuingia ndani baada ya kujifungia chumbani na msichana huyo.

    Tukio hilo limezua hasira kwenye mitandao ya kijamii na maandamano ya umma katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

    Pia imeibua mijadala mipya kuhusu sheria za ulinzi wa mtoto, kwani kwa sasa hakuna umri wa chini kabisa wa kisheria wa kuolewa.

    "Kinachoshangaza zaidi kuliko mkasa wenyewe ni madai ya kutekwa nyara na ukweli kwamba familia yake haikuwa na habari kuhusu aliko kwa miezi kadhaa," Fadumo Ahmed, mwenyekiti wa kundi linaloongoza la kutetea haki za wanawake wa Somalia, aliiambia BBC.

    "Tunaamini taasisi zinazohusika kuchukua hatua za kisheria zinazofaa na zinazohitajika."

    Kulingana na mjomba wa mtoto huyo mwenye umri wa miaka minane, alichukuliwa kutoka nyumbani kwake katika jiji la Bosaso Septemba iliyopita na jamaa wa kike. Jamaa huyu alisema alikuwa akimsindikiza mtoto huyo safarini kwenda kuonana na mjomba mwingine.

    Lakini miezi kadhaa baadaye, video iliibuka mtandaoni, ikimuonyesha msichana huyo akisoma Quran.

    Familia yake baadaye ilianzisha utafutaji wa mtoto - haijulikani kwa nini hawakufanya hivi mapema.

    Waligundua alikuwa katika eneo la Carmo, akiishi na Sheikh Mahmoud.

    Sheikh Mahmoud awali alisema alikuwa akimfundisha msichana huyo Quran pekee. Lakini baada ya malalamiko ya kisheria kuwasilishwa, alibadilisha kauli yake, akisema alimuoa msichana huyo kwa idhini ya baba yake.

    Alipoulizwa na BBC jinsi alivyohalalisha kuoa mtoto wa miaka minane, Sheikh Mahmoud alisema kwamba tamaduni za Mtume wa Uislamu Muhammad, pamoja na zile za Shafi'i, ziliruhusu ndoa za utotoni.

    Baada ya BBC kuhoji hoja yake - ikitoa upinzani kutoka kwa wasomi wengi wa Kiislamu wa Somalia - Sheikh Mahmoud alishikilia kuwa hataiacha ndoa hiyo.

  5. Wanne wauawa katika shambulizi la Israel huko Beirut

    Athari za mashambulizi

    Shambulio la anga la Israel katika vitongoji vya kusini mwa Beirut limewaua watu wanne, wizara ya afya ya Lebanon imesema, na kuweka shinikizo zaidi katika usitishwaji wa mapigano kati ya Israel na kundi linalojihami la Lebanon Hezbollah.

    Shambulio hilo pia lilijeruhi watu saba, wizara ya afya ilisema.

    Shambulio hilo lilikuwa la pili kwenye eneo la Dahieh, ambapo Hezbollah imekuwa na uwepo mkubwa, katika siku za hivi karibuni, licha ya makubaliano ya amani yaliyoanza kutekelezwa mnamo Novemba.

    Jeshi la Israel limesema limemlenga askari wa Hezbollah ambaye aliisaidia Hamas kupanga mashambulizi dhidi ya raia wa Israel.

    Hakujawa na majibu kutoka kwa Hezbollah. Rais wa Lebanon Joseph Aoun alilaani shambulio hilo na kulitaja kuwa onyo hatari.

  6. Zimbabwe 'yafungwa' kutokana na miito ya maandamano

    .
    Maelezo ya picha, Mamlaka ilikuwa imeonya kwamba maandamano yoyote hayatavumiliwa

    Maandamano ya kitaifa yaliyokusudiwa kumshinikiza Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa kujiuzulu yaligeuka kuwa kizuizi huku raia wakiamua kukaa pembeni badala ya kuingia barabarani huku kukiwa na ulinzi mkali.

    Ni waandamanaji wachache tu walioshiriki katika maandamano hayo yaliyopangwa, yakiongozwa na kundi la maveterani wa kivita wasioridhika ambao wamemshutumu Mnangagwa kwa ufisadi na kutaka kung'ang'ania madaraka, na wakatawanywa na polisi.

    Kufuatia ripoti za idadi ndogo ya waliojitokeza kupiga kura, kiongozi wa waandamanaji Blessed Geza aliwataka Wazimbabwe "wasiwe waoga" kwenye chapisho kwenye X.

    Mnangagwa alikua rais mwaka 2017 kufuatia mapinduzi dhidi ya kiongozi wa muda mrefu Robert Mugabe na kwa sasa anahudumu muhula wake wa pili na wa mwisho.

    Geza, ambaye anataka Makamu wa Rais Constantine Chiwenga achukue nafasi ya Mnangagwa, hapo awali alitoa wito kwa Wazimbabwe "kujaa barabarani" katika harakati za mwisho za kumshinikiza rais kujiuzulu.

    Video nyingi zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii siku nzima na katika moja, polisi wanaweza kuonekana wakitumia vitoa machozi kutawanya umati uliokusanyika kwenye uwanja wa Rais Robert Mugabe mjini Harare.

    Katika nyingine, mwanamke anaelezea juhudi za polisi kukabiliana na kile kinachoonekana kama "maandamano ya amani" huku akiapa "hatuendi popote, tutabaki hapa".

    "Nina umri wa miaka 63 na maisha ni magumu...ninawatunza wajukuu wangu kwa sababu watoto wangu hawana uwezo wa kumudu," muandamanaji aliyetumia magongo pia aliambia shirika la habari la Citizens Voice Network.

    "Tunataka Jenerali [Constantine] Chiwenga kuchukua nafasi," aliongeza.

  7. Mhalifu wa kivita aliyepatikana na hatia Thomas Lubanga atangaza kundi jipya la waasi mashariki mwa Kongo

    .
    Maelezo ya picha, Thomas Lubanga

    Mhalifu wa kivita aliyepatikana na hatia nchini Uganda ametangaza vuguvugu jipya la waasi lililo na nia ya kuiangusha serikali katika jimbo la Ituri mashariki mwa Kongo, na kusababisha tishio jingine la usalama katika eneo hilo lililokumbwa na vita.

    Kuundwa kwa kundi la Azimio la Mapinduzi (CPR) na Thomas Lubanga, mzaliwa wa Ituri, kunajiri wakati jeshi la Kongo linakabiliwa na msukumo usio na kifani wa waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda mashariki mwa Kongo.

    Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilipata hatia ya kwanza dhidi ya Lubanga mwaka 2012 kwa tuhuma za kuwaajiri watoto askari na kumhukumu kifungo cha miaka 14 jela.

    Aliachiliwa mwaka wa 2020, na Rais Felix Tshisekedi alimteua kwenye kikosi kazi kuleta amani Ituri.

    Lakini mwaka 2022 alichukuliwa mateka kwa muda wa miezi miwili na kundi la waasi, ambalo analaumu serikali, na sasa yuko nchini Uganda.

    Katika majibu yaliyoandikwa kwa maswali kutoka Reuters, Lubanga alisema CPR ina wahusika wa kisiasa na kijeshi, wakiwemo watu wenye silaha katika maeneo matatu ya Ituri.

    Kuleta amani katika eneo hilo "kunahitaji mabadiliko ya mara moja katika utawala na serikali", alisema, ingawa aliongeza kuwa kundi hilo halijaanzisha operesheni za kijeshi.

    Haijulikani ni wapiganaji wangapi ambao Lubanga anawadhibiti.

    Wataalamu wa Umoja wa Mataifa mwaka jana walimshutumu kwa kuhamasisha wapiganaji kusaidia wanamgambo wa ndani na M23

  8. Iran yamuita afisa mkuu wa ubalozi wa Uswizi baada ya vitisho vya makubaliano ya nyuklia ya Trump

    .
    Maelezo ya picha, Ayatollah Ali Khamenei

    Tehran ilimuita afisa mkuu wa ubalozi wa Uswizi mjini Tehran, unaowakilisha maslahi ya Marekani nchini Iran.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, alisema kwenye ukurasa wake wa Twitter: Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, zinaituhumu Iran kwa kutaka kupata silaha za nyuklia.

    Tehran inakanusha kabisa shutuma hizi, ikisisitiza kwamba shughuli zake za nyuklia ni za kiraia tu, haswa katika sekta ya nishati.

    Baada ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Iran na Marekani kukatika mwaka 1980, nchi hizo mbili zilianza kuwasiliana kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupitia ubalozi wa Uswizi mjini Tehran.

    Kwa upande wake, Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alionya Jumatatu kuhusu jibu kali iwapo nchi yake itashambuliwa, kufuatia tishio la Rais wa Marekani Donald Trump la "kuishambulia Iran" ikiwa haitaafikia makubaliano nayo kuhusu mpango wake wa nyuklia.

    "Wanatishia kuleta madhara... lakini kama hilo litatokea, hakika watapata 'jibu thabiti' kutoka kwa Iran," Khamenei alisema wakati wa hotuba yake ya Eid al-Fitr.

    Katika mahojiano siku ya Jumamosi, Trump alisema Iran itashambuliwa kwa mabomu iwapo haitaafikiana kuhusu mpango wake wa nyuklia.

    Aliongeza, "Ikiwa hawatafanya makubaliano, kutakuwa na mlipuko," kulingana na NBC News, ambayo ilisema pia alitishia kuiadhibu Iran kwa kile alichokiita "ushuru wa pili."

    Ingawa Khamenei hakumtaja Trump kwa uwazi, hotuba yake ilionekana kujibu vitisho ambavyo rais wa Marekani ametoa katika siku za hivi karibuni.

    Trump alikariri tishio lake kwa Iran siku ya Jumapili, akisema itapigwa bomu ikiwa haitakubali pendekezo lake la mazungumzo kama ilivyoainishwa katika barua aliyotuma kwa uongozi wa Iran mapema Machi, akiipa Tehran muda wa miezi miwili kufanya uamuzi.

    Kauli za Trump zinaonyesha kuongezeka baada ya kutishia siku zilizopita kwamba "mambo mabaya sana yatatokea kwa Iran" ikiwa itakataa kujadili makubaliano mapya ya nyuklia.

  9. Miili ya wanajeshi watatu wa Marekani waliotoweka yapatikana Lithuania

    .
    Maelezo ya picha, Inasemekana ilichukua kama saa mbili na magari kadhaa mazito ya kijeshi na ujenzi kuliondoa gari la M88A2 Hercules kutoka kwa matope

    Miili ya wanajeshi watatu wa Marekani, waliotoweka kwa siku sita, imepatikana kwenye kwenye matope karibu na mji wa PabradÄ— nchini Lithuania, ambapo walikuwa wakishiriki katika mazoezi ya kijeshi, Jeshi la Marekani limethibitisha.

    Vikosi vya uokoaji bado vinamtafuta mwanajeshi wa nne. "Askari tuliowapoteza katika mkasa huu hawakuwa wanajeshi tu - walikuwa sehemu ya familia yetu...

    Lakini msako haujakamilika hadi kila mtu atakapokuwa nyumbani", alisema Meja Jenerali Christopher Norrie katika taarifa iliyotolewa na Jeshi la Marekani la Ulaya na Afrika.

    Ujumbe huo tata wa utafutaji na uokoaji umejumuisha Jeshi la Marekani na Jeshi la Wanamaji, pamoja na Vikosi vya Wanajeshi vya Lithuania na Poland katika juhudi ambazo zimehitaji "rasilimali nyingi", ilisema taarifa hiyo.

    Wanajeshi hao wanne walitoweka asubuhi ya tarehe 25 Machi walipokuwa wakifanya mazoezi katika M88A2 Hercules - gari kubwa la kivita ambalo limeundwa kurejesha vifaru vilivyoharibika na magari mengine kutoka kwenye uwanja wa vita.

    Walikuwa "wakishiriki katika misheni ya kukarabati na kuvuta gari la kimbinu lisiloweza kuendeshwa" walipopotea, ilisema taarifa hiyo.

    Gari la wanajeshi hao lilipatikana likiwa limezama karibu na mpaka na Belarus mapema tarehe 26 Machi. Kulitoa kwenye matope ilikuwa kazi ngumu.

    Wapiga mbizi wa Jeshi la Wanamaji wa Marekani waliletwa ili kuunganisha nyaya kwenye gari lililozama, na ilibidi watembee "kupitia matope, udongo wakiwa hawaonekani ", ilisema taarifa hiyo.

  10. Marekani inasema sheria inatumika sawa kwa 'wahusika wote' Gaza

    .
    Maelezo ya picha, Waombolezaji walikusanyika katika mazishi siku ya Jumatatu baada ya miili ya watu 15, wakiwemo wahudumu wa afya na mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa, kupatikana kwenye kaburi la pamoja, kulingana na UN.

    Marekani imesema inatarajia "wahusika wote walioko" huko Gaza kufuata sheria za kimataifa za kibinadamu lakini ilikataa kuthibitisha ikiwa ilikuwa ikifanya tathmini yake yenyewe kuhusu mauaji ya jeshi la Israel ya watu 15 - wahudumu wa afya, wafanyakazi wa ulinzi wa raia na afisa wa Umoja wa Mataifa.

    Alipoulizwa kuhusu mauaji hayo, msemaji wa idara ya serikali Tammy Bruce alisema: "Kila jambo linalotokea Gaza linatokea kwa sababu ya Hamas."

    Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu limesema magari matano ya kubebea wagonjwa, lori la zima moto na gari la Umoja wa Mataifa yalishambuliwa "moja kwa moja" tarehe 23 Machi na kwamba miili 15, wakiwemo wahudumu wa afya ambao bado wamevalia sare zao, walikuwa wamekusanywa na kuzikwa kwenye kaburi la pamoja.

    Jeshi la Israel limesema wanajeshi wake waliyafyatulia risasi magari yaliyokuwa yakienda kwa kutia shaka bila ya kuwasha taa wala ishara za dharura na kwamba afisa wa Hamas na wanamgambo wengine ni miongoni mwa waliouawa, lakini halikutoa maoni yoyote kuhusu maiti zilizokusanywa na kuzikwa.

    Sheria ya kimataifa ya kibinadamu inakataza kuwalenga raia na inataka ulinzi mahususi kwa maafisa wa matibabu.

    Marekani, msambazaji mkubwa wa silaha kwa Israel, pia inafungwa na sheria zake zinazokataza silaha zake kutumiwa na wanajeshi wa kigeni kinyume na sheria za kibinadamu.

  11. Urusi inasema 'inaendelea kushirikiana ' na Marekani baada ya Trump kusema 'ana hasira' na Putin

    .

    Urusi inasema bado "inashirikiana na Marekani" baada ya Rais Trump kusema "amekasirika" na "kukerwa" na Vladimir Putin.

    Katika jibu lake la kwanza kwa ukosoaji wa Trump kwa rais wa Urusi, Kremlin ilijaribu kupuuza mvutano kati ya viongozi hao wawili. "Tunaendelea kushirikiana na Marekani, kwanza kabisa, katika kujenga mahusiano yetu," msemaji, Dmitry Peskov, alisema.

    Alisema hakuna mipango ya mawasiliano ya simu kati ya Putin na Trump wiki hii, lakini kwamba Putin yuko tayari kwa mazungumzo yoyote "ikiwa ni lazima".

    Jaribio la kusuluhisha mambo lilijiri baada ya Trump kuliambia Shirika la Habari la NBC Jumapili kwamba alikasirishwa na Putin kwa kushambulia uaminifu wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, na kutishia kutoza ushuru wa 50% kwa nchi zinazonunua mafuta ya Urusi ikiwa Putin hatakubali kusitisha mapigano. Ilikuwa ni mabadiliko makubwa ya wito kwa rais wa Urusi.

    Maafisa wa Marekani na Urusi wamekuwa katika mazungumzo kwa wiki kadhaa kujaribu kufikia makubaliano ya kumaliza vita nchini Ukraine - ambapo mara nyingi Trump amekuwa akimkosoa Zelensky lakini si Putin.

    Lakini hasira ya Trump dhidi ya Putin ilichochewa wakati rais wa Urusi siku ya Ijumaa alipopuuza wazo la serikali ya mpito nchini Ukraine chini ya uungwaji mkono wa UN ambayo inaweza kuchukua nafasi ya Rais Zelensky.

    "Unaweza kusema kwamba nilikuwa na hasira sana, nilikasirika, wakati ... Putin alianza kukosoa kupata uaminifu wa Zelensky, kwa sababu hiyo haiendi katika eneo sahihi," Trump aliambia NBC News.

    "Uongozi mpya unamaanisha kuwa hakutakuwa na mpango wa kusitisha mapigano kwa muda mrefu," aliongeza.

  12. Natumai hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja