EU, Mexico zakosoa pendekezo la Trump la ushuru wa 30%
Moja kwa moja
Na Lizzy Masinga
Mfungwa atoroka akiwa kwenye begi la mfungwa mwenzake Ufaransa, maafisa wasema
Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanaume mmoja ametoroka jela ya Ufaransa kwa kujificha kwenye begi la mfungwa mwenzake aliyekuwa akitoka gerezani baada ya kumaliza kifungo chake, maafisa waliambia vyombo vya habari vya eneo hilo.
Idara ya magereza imeanzisha uchunguzi baada ya mwanaume huyo kutoroka kutoka gereza la Lyon-Corbas kusini-mashariki mwa Ufaransa siku ya Ijumaa, kulingana na shirika la utangazaji la BFMTV.
"Alitumia fursa ya mfungwa mwenzake aliyekuwa anaondoka baada ya kumaliza kifungo, kwa kujificha kwenye mizigo yake na kutoka nje", idara ya magereza ilisema katika taarifa kwa shirika la habari la AFP.
Vyombo vya habari vya Ufaransa vimeripoti kuwa mfungwa aliyetoroka alikuwa akitumikia vifungo kadhaa na pia alikuwa anachunguzwa katika kesi inayohusishwa na uhalifu wa kupangwa.
Mwezi uliopita, Chama cha Wanasheria wa Lyon kilieleza wasiwasi kuhusu msongamano wa watu katika gereza la Lyon-Corbas.
Kufikia tarehe 1 Mei 2025, karibu watu 1,200 walifungwa katika gereza hilo, ambalo linaweza kuchukua watu 678, BFMTV ilikuwa imeripoti.
Mapigano makali yanaendelea El-Fasher nchini Sudan
Chanzo cha picha, Hassan Lali / BBC
Mapigano makali yanaendelea El-Fasher nchini Sudan, mji mkuu wa mwisho katika eneo la Darfur ambao bado uko chini ya udhibiti wa jeshi.
Wanajeshi pamoja na wapinzani wao, Vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) wote wanadai kupiga hatua muhimu, huku raia wakiendelea kuumia katika vita.
Jeshi la Sudan linasema kuwa lilizuia shambulizi lingine la RSF lililoanza siku ya Ijumaa, likidai kwamba lilisababisha 'hasara kubwa' kwa kundi hilo na kuongeza kuwa wanajeshi wanadhibiti maeneo yote muhimu ya kijeshi huko Al Fasher.
Lakini RSF inapinga hili, ikisisitiza kuwa vikosi vyake vinadhibiti makao makuu ya polisi, soko kuu la mifugo, na kwamba wanasonga mbele kuelekea uwanja wa ndege.
Mashambulizi haya mapya yanajiri baada ya wiki kadhaa za mashambulizi ya mizinga mikubwa na ndege zisizokuwa na rubani za RSF, hali ambayo imezidisha mzozo wa kibinadamu kwa raia huko El-Fasher.
Wakazi wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, dawa, na makazi salama.
Juhudi za kusitisha mapigano zilizosimamiwa na Umoja wa Mataifa zimekwamba.
El-Fasher imekuwa ikizingirwa na RSF tangu Mei mwaka jana. Kundi hilo limekuwa likishutumiwa kwa ukatili mkubwa dhidi ya raia huku likijaribu kuimarisha udhibiti wake kwa eneo la Darfur.
Balozi wa Tanzania nchini Cuba Humphrey Polepole ametangaza kujiuzulu kwenye nafasi hiyo, akisema hatua hii imetokana na “matukio ya hivi karibuni ya wazi ya kukiuka misingi, utamaduni na desturi za Chama cha Mapinduzi (CCM)”.
Katika barua kwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyochapisha katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Polepole ametilia doa mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya chama hicho huku taifa hilo likijiandaa kwa uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.
Mbunge huyo wa zamani wa kuteuliwa ambaye pia aliwahi kuhudumu kama balozi wa Tanzania nchini Malawi amesema kauli maarufu ya CCM ya “Chama kwanza mtu baadaye” inafanyika vinginevyo.
“Kwa kuwa siwezi kuendelea kuwa sehemu ya uongozi usiohamasika na utii wa misingi ya Katiba ya nchi na chama, haki, maadili, utu na uwajibikaji wa wananchi, nimeamua kwa hiari yangu kujiuzulu nafasi yangu ya uongozi na utendaji serikalini,” alisema Polepole, akiongeza kuwa ataendelea kuwa mwanachama wa kawaida wa CCM.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makala, amekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni kuwa baadhi ya makada wa chama hicho wameenguliwa katika hatua za awali za mchakato wa kuwania ridhaa ya kugombea ubunge.
Kuhusu barua ya Polepole amesema kama kweli barua hiyo ni ya kweli basi hayo ni maoni yake binafsi, ni ridhaa yake na mawazo yake na kuwa kama alivyokiri kuwa ataendelea kuwa mwanachama wa CCM, basi anatambulika kuwa mwanachama wa chama hicho.
Humphrey Polepole ni nani?
Humphrey polepole amekuwa mwanasiasa maarufu kwa takriban miaka 10 kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania Malawi mwaka 2022. Alikulia katika Umoja wa Vijana wa CCM.
Alianza kujulikana zaidi mwaka 2012 alipoteuliwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete kuwa mjumbe wa Tume ya Katiba mpya, iliyoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba na kumaliza kazi yake mwaka 2014.
Mwaka 2016 Rais John Magufuli alimteua Polepole kuwa Mkuu wa wilaya ya Musoma, mkoani Mara, alikohudumu kwa miezi michache kisha kuhamishiwa Ubungo Dar es Salaam kwa nafasi hiyo hiyo ya ukuu wa wilaya na kuhudumu kwa miezi michache pia.
Umaarufu wake uliongezeka alipoteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, nafasi ambayo kimsingi ni ya kuwa msemaji wa chama.
Anafahamika kwa kutetea sera na utendaji wa CCM na serikali ya Rais Magufuli, hata pale kulipokuwa na utata mkubwa wa masuala kama vile tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu, utekaji, kuwaweka watuhumiwa mahabusu kwa muda mrefu na wengine kufunguliwa kesi nzito za uhujumu uchumi na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu wa 2020. Rais Samia alipoingia madarakani Machi 2021, Polepole hakukaa kwa muda mrefu kwenye nafasi ya usemaji kwani aliondolewa kisha kuteuliwa kuwa Mbunge kabla ya kuteuliwa balozi nchini Malawi.
Anajulikana pia kwa kauli tata au ahadi za CCM na serikali ambazo hazikuwa kutekelezwa, kama vile ujenzi wa barabara za juu (fly overs) katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Hadi sasa barabara za juu zimejengwa nne katika maeneo ya Ubungo, Tazara, Chang'ombe na makutano ya barabara za Mandela na Kilwa.
Wakati fulani baada ya kuondolewa kwenye usemaji wa CCM aliwahi kunukuliwa kwenye mahojiano akisema CCM kumejaa watu wahuni wanaofanya matendo mabaya kama fitina, zengwe na uchawi, dhidi ya watu 'walionyooka' kama yeye na kudai hawezi kupatwa na uchawi hata shetani anamuogopa. Linalongojewa sasa ni kuona mustakabali wake kisiasa baada ya kujiuzulu ubalozi na nafasi nyingine za umma.
Watoto wauawa wakichota maji katika shambulio la Israel huko Gaza, maafisa wasema
Chanzo cha picha, Getty Images
Watu kumi, wakiwemo watoto sita, wameuawa katika shambulizi la anga la Israel wakati wakisubiri kuchota maji katikati mwa Gaza siku ya Jumapili, maafisa wa huduma ya dharura wamesema.
Miili yao ilitumwa katika Hospitali ya al-Awda ya Nuseirat, ambayo pia ilihudumia watu 16 waliojeruhiwa, saba kati yao wakiwa watoto, kwa mujibu wa daktari mmoja katika kituo hicho.
Walioshuhudia wanasema ndege isiyo na rubani ilirusha kombora kwa umati wa watu waliokuwa wamepanga foleni wakiwa na mitungi karibu na gari la maji katikati ya kambi ya wakimbizi ya al-Nuseirat.
BBC imetuma ombi kwa jeshi wa Israel kuzungumzia kisa hiki. Picha ambazo hazijathibitishwa zilichapishwa mtandaoni baada ya shambulizi hilo zikionyesha watoto waliokuwa na damu pamoja na miili, huku watu wakipiga kelele za hofu na kuonyesha kukata tamaa.
Wakazi walikimbilia eneo la tukio na kuwasafirisha waliojeruhiwa kwa kutumia magari ya kibinafsi na mikokoteni ya punda. Shambulio hilo limekuja huku mashambulizi ya anga ya Israel katika ukanda wa Gaza yakiongezeka.
Msemaji wa Shirika la Ulinzi la Raia la Gaza amesema kuwa Wapalestina wengine 19 waliuawa siku ya Jumapili, katika mashambulizi matatu tofauti dhidi ya majengo ya makazi katikati mwa Gaza na pia Gaza City.
Israel ilianzisha kampeni ya kijeshi huko Gaza kujibu shambulio la Hamas la kuvuka mpaka wake tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 kuchukuliwa mateka.
Takriban watu 57,882 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kwa mujibu wa wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas.
Idadi kubwa ya wakazi wa Gaza wamelazimika kuhama makazi yao mara kadhaa. Zaidi ya 90% ya nyumba zinakadiriwa kuharibiwa.
Mifumo ya huduma za afya, maji, na usafi wa mazingira imeporomoka, na kuna uhaba wa chakula, mafuta, dawa na makazi.
Wiki hii, kwa mara ya kwanza katika muda wa siku 130, lita 75,000 za mafuta ziliruhusiwa kuingia Gaza, kiwango ambacho kiko "hakitoshi kabisa kwa mahitaji ya kila siku ya watu wa ukanda huo pamoja na shughuli muhimu za misaada ya kiraia", Umoja wa Mataifa ulisema.
Siku ya Jumamosi, mashirika tisa ya Umoja wa Mataifa yalionya kwamba uhaba wa mafuta Gaza umefikia "viwango vya chini kabisa", na ikiwa mafuta yataisha, itaathiri hospitali, mifumo ya maji, mifumo ya usafi wa mazingira na vituo vya kuoka mikate.
"Hospitali tayari zimekosa mwanga, ziko gizani, vyumba vya uzazi, watoto wachanga na wagonjwa mahututi vinashindwa kufanya kazi, na magari ya kubeba wagonjwa hayaendi tena," UN ilisema.
Jaji azuia utawala wa Trump kuwakamata 'kiholela' wahamiaji
Chanzo cha picha, Getty Images
Jaji wa California ameamuru utawala wa Trump ukomeshe kuwazuia 'kiholela' watu wanaodhaniwa kuwa nchini Marekani kinyume cha sheria.
Uamuzi huo ulitolewa katika amri ya zuio la muda iliyotolewa dhidi ya serikali siku ya Ijumaa, ambayo pia inazuia maafisa wa uhamiaji kuwanyima watu kupata mawakili.
Kesi hiyo ilipelekwa katika kesi iliyofunguliwa na wahamiaji watatu, waliokamatwa katika kituo cha mabasi cha Pasadena wakitafuta kazi, na raia wawili wa Marekani waliokuwa wakishikiliwa, mmoja wao akiripotiwa kuonesha kitambulisho.
Idara ya Usalama wa Ndani ilijibu agizo la jaji katika chapisho la mtandao wa kijamii, ikimtuhumu kwa "kudhoofisha utashi wa watu wa Marekani".
Maagizo ya dharura ya Jaji Maame Frimpong ni hatua ya muda wakati kesi ikiendelea. Katika agizo lake, Jaji Frimpong alisema kulikuwa na "ushahidi mwingi" wa kuunga mkono kwamba maafisa wamekuwa wakifanya "doria za kuzunguka-zunguka", zinazofafanuliwa kama "kuwakusanya watu kiholela bila msingi", alisema.
Uamuzi huo wa Jaji Frimpong unakuja wakati utawala wa Trump ukizidisha juhudi zake za kukabiliana na wahamiaji haramu, haswa katika jimbo la California, ngome ya chama cha Democratic.
Hospitali ya Gaza yasema watu 24 waliuawa karibu na eneo la misaada
Chanzo cha picha, Reuters
Hospitali ya Nasser kusini mwa Gaza imesema watu 24 wameuawa karibu na eneo la kusambaza misaada.
Wapalestina waliokuwepo katika eneo hilo walisema wanajeshi wa Israel walifyatulia risasi watu walipokuwa wakijaribu kupata chakula siku ya Jumamosi.
Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) lilisema "hakuna watu wanaojulikana waliojeruhiwa" kutokana na moto wa IDF karibu na eneo hilo.
Kando na hilo, afisa wa kijeshi wa Israel alisema risasi za onyo zilipigwa ili kuwatawanya watu ambao IDF iliamini kuwa ni tishio.
Madai ya pande zote mbili hayajathibitishwa. Israel hairuhusu mashirika ya habari ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na BBC, kuingia Gaza.
Picha zilizoonekana na BBC baadaye Jumamosi zilionesha kile kilichoonekana kuwa idadi ya mifuko ya miili katika ua wa hospitali ya Nasser ikiwa imezungukwa na wauguzi na watu waliovalia nguo zilizotapakaa damu.
Katika video nyingine, mwanaume mmoja alisema watu walikuwa wakingoja kupata usaidizi walipofyatuliwa risasi kwa dakika tano.
Video hizo hazijathibitishwa na BBC. Reuters ilisema ilizungumza na mashahidi ambao walielezea watu kupigwa risasi kichwani.
Shirika la habari pia liliripoti kuona miili imefungwa kwa sanda nyeupe katika hospitali ya Nasser.
Kumekuwa na ripoti karibu kila siku za watu kuuawa na Israel walipokuwa wakitafuta chakula huko Gaza.
EU, Mexico zakosoa pendekezo la Trump la ushuru wa 30%
Chanzo cha picha, Getty Images
Umoja wa Ulaya (EU) na Mexico zimeelezea kusikitishwa na
tishio la Rais wa Marekani Donald Trump la kutoza ushuru wa asilimia 30 kwa
bidhaa zinazotoka nje kuanzia tarehe 1 Agosti.
Mexico ilikosoa kile ilichokiita "mkataba usio wa
haki" wa Trump na kusisitiza uhuru wake hauwezi kujadiliwa, wakati mkuu wa
EU, Ursula von der Leyen akitishia kuchukua "hatua sawia", ikiwa
itahitajika. Wote wawili walisema wanataka kuendelea kufanya mazungumzo na
Marekani.
Trump ameonya kuwa atatoza ushuru mkubwa zaidi wa bidhaa
kutoka nje ikiwa mmoja wa washirika wa biashara wa Marekani wataamua kulipiza
kisasi.
Wiki hii Trump pia alitangaza ushuru mpya kwa bidhaa kwa Japan,
Korea Kusini, Canada na Brazil kuanzia mwezi ujao.
Katika barua iliyotumwa siku ya Ijumaa kwa Rais wa Tume ya
Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, Trump aliandika: "Tumekuwa na miaka
ya kujadili uhusiano wetu wa kibiashara na Umoja wa Ulaya, na tumehitimisha
kwamba lazima tuondokane na upungufu huu wa muda mrefu, na unaoendelea wa
biashara, unaosababishwa na ushuru wako, na usio wa ushuru, sera na vikwazo vya
biashara."
''Uhusiano wetu umekuwa, kwa bahati mbaya, mbali na
maelewano," barua hiyo iliongeza.
Katika barua zake kwa Umoja wa Ulaya na Mexico, Trump
alionya kwamba iwapo mshirika wa kibiashara atalipiza kisasi ushuru wake dhidi
ya Marekani, atajibiwa kwa kuongeza ushuru kwa asilimia zaidi ya 30.