AFCON 2025: Nani bingwa? Morocco au Senegal, Mahakama kuamua leo

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
- Author, Ian Williams
- Nafasi, BBC Sport Afrika
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Fainali ya AFCON 2025 kati ya Morocco na Senegal, iliyochezwa Januari mwaka huu, sasa inaelekea kupata mshindi wake wa mwisho mahakamani badala ya uwanjani.
Mahakama ya juu zaidi inayoshughulikia masuala ya sheria za michezo inatarajiwa kutoa uamuzi wake Jumanne kuhusu rufaa ya Senegal, ambayo inapinga uamuzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wa kuinyang'anya timu hiyo ubingwa na kuipa Morocco ushindi wa mabao 3-0.
Senegal ilikuwa imetangazwa mshindi baada ya kuifunga Morocco bao 1-0 katika fainali iliyochezwa Rabat, lakini CAF ilibatilisha matokeo hayo mwezi Machi, ikidai kuwa Senegal ilikiuka kanuni za mashindano.
Shauri hilo lilisikilizwa mapema Oktoba, huku pande hizo mbili zikisubiri uamuzi wa mwisho ambao utaamua ni nchi gani itakayobeba taji la AFCON 2025.
Nini kilitokea katika fainali ya AFCON 2025?
Mashabiki wapatao 66,000 walijaza Uwanja wa Prince Moulay Abdellah nchini Morocco, wakishuhudia wenyeji wakisaka ubingwa wao wa kwanza wa AFCON tangu mwaka 1976.
Hata hivyo, fainali hiyo iligeuka kuwa ya vurugu na malumbano katika dakika za mwisho za mchezo, baada ya muda wa kawaida kumalizika bila timu yoyote kupata bao.
Senegal ilidhani imepata bao muhimu kupitia Ismaila Sarr, lakini furaha yao ilikatizwa baada ya mwamuzi Jean-Jacques Ndala kupuliza filimbi, kabla ya uamuzi mwingine wa kutoa penati kwa Morocco.
Hali ilizidi kuwa mbaya dakika ya 98 baada ya mwamuzi kukagua picha za VAR na kuthibitisha penati hiyo kwa Morocco.
Wachezaji wa Senegal walipinga vikali uamuzi huo, huku kocha Pape Thiaw akiwaongoza baadhi yao na maofisa wa timu kutoka uwanjani na kuelekea vyumba vya kubadilishia nguo. Wakati huohuo, mashabiki walikabiliana na maafisa wa usalama, hali iliyosababisha mchezo kusimama kwa muda.
Mchezo uliendelea baadaye, lakini Morocco ilishindwa kutumia nafasi ya kupata ushindi baada ya Brahim Diaz kukosa penati dakika ya 124, aloyejaribu kupiga mtindo wa Panenka ambao ulidakwa kirahisi na kipa Edouard Mendy.
Katika dakika za nyongeza, Pape Gueye aliifungia Senegal bao lililoipa ushindi wa 1-0 na kutwaa ubingwa wa pili wa Afrika katika historia yake.
Hata hivyo, furaha ya Senegal haikudumu kama ilivyotarajiwa.
Kwa nini CAF ilibatilisha matokeo ya fainali?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mara baada ya mchezo, Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) liliwasilisha malalamiko CAF, likidai kuwa Senegal ilikiuka kanuni za mashindano kwa kuondoka uwanjani kabla mchezo haujakamilika.
Kanuni ya 82 ya mashindano, inayohusu kujiondoa kwa timu, inaeleza kuwa timu inayokataa kucheza au kuondoka uwanjani kabla ya mchezo kumalizika rasmi, bila ruhusa ya mwamuzi, inaweza kuchukuliwa kuwa imepoteza mchezo na kuondolewa kwenye mashindano.
Mwezi Machi, kamati ya CAF inayoshughulikia masuala ya kinidhamu ilisikiliza malalamiko hayo na kuipoka ubinhwa Senegal na kuiipa Morocco ushindi wa mabao 3-0.
Hata hivyo, uamuzi huo ulizua mjadala kuhusu mamlaka ya mwamuzi kusimamisha mchezo na kama kitendo cha wachezaji kuondoka uwanjani kilitosha kuhalalisha kubatilishwa kwa matokeo.
Baadhi ya watu, akiwemo aliyekuwa ofisa wa CAF, wamehoji kama ni mwamuzi pekee mwenye mamlaka ya kusimamisha kabisa mchezo katika mazingira kama hayo.
Shirikisho la Soka la Morocco lilisisitiza kuwa kanuni za mashindano zinapaswa kutekelezwa ipasavyo.
Kwa upande wake, Shirikisho la Soka la Senegal lilipinga uamuzi huo, likiuelezea kuwa hauna haki, haujawahi kutokea na ni kinyume cha sheria, kabla ya kuwasilisha rufaa.


































