Filin: Kwa nini kombora hili jipya la Urusi ni tishio?

.
    • Author, Ilya Abishev
    • Nafasi, Mchambuzi wa Masuala ya Kijeshi, BBC ya Kirusi
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Kuanzia mwishoni mwa majira ya kiangazi ya mwaka 2026, Urusi itaanza kutumia kombora la masafa marefu la Filin kuishambulia Ukraine; kombora dogo kiasi na huenda likawa na gharama ndogo, lakini lenye uwezo mkubwa wa kuvutia kulingana na sifa zilizotangazwa. Ni tishio kwa Ukraine na mataifa mengine.

Taarifa kamili kuhusu kombora hilo bado hazijapatikana. Hadi sasa, picha ya sehemu iliyoharibika ya kombora la Filin linalodaiwa kutunguliwa imechapishwa mtandaoni. Taarifa za jumla kuhusu muundo wake, mifumo ya kielektroniki na injini yake pia zilitolewa na Wizara ya Ulinzi ya Ukraine tarehe 22 Oktoba.

Wataalamu wa kijeshi wanakubaliana kwamba makombora ya Filin, iwapo Urusi itaweza kuanza kuyazalisha kwa wingi, yanaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa shinikizo dhidi ya mfumo wa ulinzi wa anga wa Ukraine.

Je tunajua nini kuhusu silaha hii mpya iliyozalishwa kwenye viwanda vya kijeshi vya Urusi, na kombora hili lina hatari gani kwa Ukraine na mataifa mengine hasimu na Urusi?

Sifa za jumla za kombora

Kwa mujibu wa taarifa za kijasusi za Wizara ya Ulinzi ya Ukraine, kombora la Filin lilitengenezwa na Taasisi ya Molniya inayoshughulika na masuala ya utafiti wa na uzalishaji wa silaha iliyopo Moscow, ambayo ni sehemu ya Shirika kubwa la Silaha za Makombora za Kimbinu.

Filin ni kombora dogo la masafa marefu linalotumia injini ya turbojet, ambalo hurushwa kutoka kwenye jukwaa la ardhini kwa kutumia kifaa cha awali cha kuongeza msukumo wakati wa kulifyatua.

Kombora hilo lina kasi ya juu inayofikia kilomita 800 kwa saa, masafa ya takribani kilomita 1,200 na linaweza kuruka katika mwinuko wa chini sana, chini ya mita 200, hadi kilomita sita.

Umbali huo ni zaidi ya umbali wa kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza au Dar es Salaam mpaka Nairobi ambo ni chani ya kilomita 1,200

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa kawaida, takwimu hizi ni uwezo wa juu uliotangazwa na si matokeo ya majaribio huru yaliyofanyika katika mazingira halisi ya safari ya angani.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, Filin inapatikana ikiwa na aina mbili za vichwa vya vita, vyenye uzito wa kilo 50 na kilo 100.

Tofauti na aina ya ndege zisizo na rubani za Gran, ambazo zimebadilika hatua kwa hatua kutoka ndege zinazotumia injini za pistoni na kuruka katika mwinuko mdogo hadi silaha za mashambulizi za kasi kubwa zinazotumia injini za turbojet, Filin ilibuniwa tangu mwanzo kama kombora la masafa marefu.

"Nimetabiri kwa muda mrefu kwamba adui yetu katika siku zijazo hatategemea Shahid (droni) zinazotumia injini za jet," anaandika Sergey Beskrestenov, mshauri wa rais wa Ukraine anayejulikana kwa jina la "Flash".

"Zina kasi zaidi na uwezo mkubwa zaidi wa kubadilisha mwelekeo, zinaweza kuruka katika mwinuko mdogo na kubeba kichwa cha kivita chenye uzito mkubwa zaidi kuliko Shahid. Hazihitaji maeneo maalumu ya kurushia ndege zisizo na rubani, nyingi zinaweza kurushwa kutoka kwenye helikopta na ndege zisizo na rubani, na muhimu zaidi, zinaweza kutengenezwa kwa kutumia vipuri vinavyotengenezwa nchini Urusi."

Angalau uzalishaji wa sehemu kuu za kombora la Filin unafanyika ndani ya Urusi. Kombora hilo linatumia injini ndogo ya turbine ya gesi aina ya R-500, inayotengenezwa na kampuni ya Urusi ya Reynolds.

Injini hiyo hiyo pia imewekwa kwenye kombora la kushambulia kutoka angani hadi ardhini aina ya S-71K "Kaver", pamoja na silaha ya kuongozwa inayorushwa kutoka angani aina ya S-71M "Monochrome". Silaha hizo mbili zilitengenezwa na Shirika la Usanifu wa Ndege la Sukhoi na hivi karibuni zimeanza kutumika ndani ya jeshi la Urusi.

Tofauti na mifumo hiyo, baadhi ya mifumo ya zamani ya Urusi, kama matoleo ya jet ya Gran na Bandrov, hutumia injini za China ambazo huainishwa na kusambazwa kama bidhaa za matumizi ya kiraia.

Kombora la Filin lina tishio gani?

Lina uwezo wa kuruka katika mwinuko wa chini sana. Kombora la masafa marefu linaloweza kubadilisha mweleleo kulingana na maumbile ya ardhi linaweza kutokea ghafla katika eneo linaloweza kuonekana moja kwa moja na rada za ardhini. Hali hii hupunguza muda wa kulitambua, kusambaza taarifa kuhusu shabaha na kulitungua.

Lina kasi kubwa kuliko ndege zisizo na rubani zenye "gharama kubwa". Kasi iliyotangazwa ya kilomita 800 kwa saa inalifanya Filin kuwa ngumu sana kulengwa na ndege zisizo na rubani za kutungua makombora ambazo zina mwendo wa polepole zaidi.

Filin ina kichwa kikubwa cha kivita chenye uzito wa hadi kilo 100. Ingawa uzito huo ni mdogo ukilinganishwa na vichwa vya vita vya makombora makubwa zaidi ya kusafiri, ni karibu mara mbili ya uzito wa kichwa cha vita cha Garan. Hii inalipa uwezo mkubwa wa kushambulia miundombinu, maghala, maeneo ya uzalishaji na shabaha nyingine.

Lina uwezo wa kustahimili mawimbi ya kielektroniki. Kwa mujibu wa taarifa za kijasusi za Ukraine, kombora hilo linatumia moduli maalumu kwa njia ya satelaiti aina ya Kumta yenye chaneli 16 na inayostahimili jaribio la ukwamishaji wa mawimbi. Pia lina mfumo wa ndani (inertial navigation system), ambao hupunguza uwezekano wa kuathiriwa na vifaa vya kivita vya kielektroniki.

Inawezekana kulitengeneza kwa gharama ndogo. Matumizi ya mifumo iliyotengenezwa kwa vifaa mchanganyiko, teknolojia ya uchapishaji wa 3D katika baadhi ya vipuri na kutumia mifumo ileile ya kielektroniki vinaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uzalishaji wa kombora hilo.

Hata hivyo, hili bado halithibitishi kwamba Filin ni kombora la gharama ndogo kweli au kwamba kwa sasa linazalishwa kwa maelfu. Lakini linaeleza kwa nini linatajwa kama silaha inayoweza kutumika katika mashambulizi ya mara kwa mara na kwa kiwango kikubwa.

Ni njia zipi za kukabiliana na kombora la Filin?

.
Maelezo ya picha, Inawezekana kulitungua kombora la Filin, lakini kwa gharama gani?

Filin ni gumu kufuatiliwa na ndege zisizo na rubani za kutungua makombora, lakini kasi yake haizidi kasi ya mifumo mingi ya kisasa ya ulinzi wa anga. Mifumo ya makombora ya kujilinda dhidi ya mashambulizi ya angani na ndege za kivita zina uwezo wa kukabiliana na aina yoyote ya kombora la masafa marefu. Hata hivyo, ili kuhakikisha utungaji wake unafanikiwa, kunahitajika mfumo wa ulinzi wa anga wenye tabaka nyingi na unaofikia eneo kubwa na kwa kina zaidi.

Ndege za kivita zinaweza kutungua makombora ya masafa marefu yakiwa bado mbali. Lakini hata pale yanapotunguliwa, operesheni hizo zinaweza kuwa na gharama kubwa iwapo makombora adimu, kama vile AIM-9 Sidewinder, yatatumika dhidi ya kila lengo ambalo huenda lenyewe ina gharama ndogo.

Aidha, kwa makombora ya masafa marefu yanayoweza kuruka katika mwinuko mdogo sana, ni vigumu na hatari kutumia njia rahisi zaidi, kama vile mizinga ya ndege.

Njia moja inayoweza kutumika ni mifumo ya Marekani ya aina ya APKWS, ambayo hubadilisha maroketi ya kawaida yasiyo na mfumo wa kuyaelekeza kuwa silaha zenye usahihi mkubwa.

Mifumo ya makombora ya ulinzi wa anga ya Jeshi la Ukraine pia ina uwezo wa kulenga makombora ya aina ya Filin. Hata hivyo, katika hali hii pia, gharama za silaha zinazotumika na vikwazo vya upatikanaji wake vina umuhimu mkubwa.

Uendelezaji na uzalishaji wa mifumo ya ulinzi wa anga ya masafa mafupi, yenye gharama ndogo na inayoweza kuzalishwa kwa wingi, umekuwa mojawapo ya maeneo muhimu zaidi katika maendeleo ya mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga.

Mifumo hiyo inajumuisha makombora mepesi ya kutungua shabaha pamoja na mifumo ya mizinga ya kupambana na ndege yenye uwezo wa kurusha kwa kasi kubwa na kutumia teknolojia ya kulipuka kwa mpangilio maalumu, kama vile Skynex na Skyranger, zinazotengenezwa na kampuni ya ulinzi ya Ujerumani ya Rheinmetall.

Mifumo hiyo ina ufanisi na gharama nafuu, ikiwemo katika tabaka la mwisho la ulinzi. Hata hivyo, inahitaji shabaha kutambuliwa kwa wakati na kuwepo kwa mazingira yanayofaa kwa ajili ya kufyatua silaha hizo.

Ili kukabiliana na mashambulizi ya makombora yanayoruka katika mwinuko mdogo, ni muhimu rada kushirikiana, kupokea taarifa za tahadhari kuhusu vitisho vya angani kutoka nje na kuhakikisha taarifa zinasambazwa haraka baina ya vikosi na vikosi vingine. Kadiri shabaha inavyotambuliwa mapema, ndivyo uwezekano wa kuitungua unavyoongezeka.

Tishio hili jipya ni kubwa kiasi gani?

Kuwepo kwa sampuli za majaribio na kutangazwa kwa uwezo wa kombora la Filin hakumaanishi moja kwa moja kwamba Urusi ina uwezo wa kuendelea kurusha makombora hayo kwa idadi kubwa.

Taarifa za kijasusi kutoka Wizara ya Ulinzi ya Ukraine imebaini uwepo wa vipuri vilivyotengenezwa nje ya Urusi katika mifumo ya kielektroniki ya Filin, vikiwemo vipuri 35 vya Marekani na 22 vya China. Hii inaonyesha kuwa sekta ya ulinzi ya Urusi bado inategemea vipuri vya kielektroniki kutoka nje, ingawa haimaanishi moja kwa moja kwamba usambazaji wa vipuri hivyo unaweza kusitishwa kwa urahisi.

Jambo kubwa ambalo bado halijafahamika ni gharama halisi ya kutengeneza Filin, kiwango cha uzalishaji wake na mara ngapi itatumika. Kwa Ukraine, hatari kubwa ni uwezekano wa kombora hilo kuzalishwa kwa wingi kama kombora la masafa marefu linaloweza kutua nchini humo.

Iwapo kombora hilo litakuwa na gharama ndogo ya uzalishaji na kutengenezwa kwa wingi, jeshi la Urusi linaweza kulitumia sambamba na makombora ya kawaida ya balistiki, pamoja na ndege zisizo na rubani. Hali hiyo italazimisha Ukraine kugawa rasilimali zake chache za ulinzi wa anga ili kukabiliana na aina nyingi zaidi za vitisho.

Lakini iwapo uzalishaji wa Filin utabaki kuwa mdogo, kombora hilo, licha ya kuwa tishio la ziada, si lazima libadilishe kwa ujumla hali ya vita vya angani.