Wanamgambo wawaua zaidi ya watu 40 mashariki mwa DR Congo

Ni shambulio la hivi punde zaidi la kundi la Codeco, ambalo linadai kutetea maslahi ya wakulima wa Lendu.

Moja kwa moja

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri.

  2. Afrika Kusini: Chama cha ANC chamtimua Katibu Mkuu wa zamani Ace Magashule

    Makhashule
    Maelezo ya picha, Bw Magushule alionekana na wengi kama mshawishi mkuu wa kisiasa katika chama cha ANC.

    Chama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress (ANC) kimemfukuza chamani aliyekuwa Katibu Mkuu wake Ace Magashule wiki moja baada ya kamati ya nidhamu ya chama kumpata na hatia ya utovu wa nidhamu.

    Alishutumiwa kwa kujaribu kumsimamisha kazi Rais Cyril Ramaphosa kama kiongozi wa chama.

    Bw Magashule alipewa siku saba kujibu lakini katika taarifa ANC ilisema hakutuma "uwakilishi wowote kwa athari hiyo".

    Wakati fulani, Bw Magushule alionekana na wengi kama mshawishi mkuu wa kisiasa katika chama cha ANC na alikuwa mshirika mkubwa wa Rais wa zamani Jacob Zuma, ambaye Bw Ramaphosa alichukua nafasi yake mwaka wa 2018 kufuatia tuhuma nyingi za ufisadi - ambazo Bw Zuma anakanusha.

    Miaka miwili iliyopita, Bw Magashule alisimamishwa kazi na chama baada ya kushtakiwa kwa ufisadi - mashtaka ambayo anakanusha.

    Lakini Bw Magashule alisema hatua hiyo ni kinyume na katiba ya ANC akiongeza kwamba kwamba Rais Ramaphosa alisimamishwa kazi - hii ndiyo iliyosababisha mashtaka ya utovu wa nidhamu.

    Bw Magashule amedokeza kuwa huenda akaanzisha chama chake cha kisiasa.

  3. Rwanda:Meja wa zamani amtetea mshukiwa wa mauaji ya kimbari Beatrice Munyenyezi

      • Author, Yves Bucyana
      • Nafasi, BBC Swahili
    Beatrice Munyenyezi mahakamani
    Maelezo ya picha, Beatrice Munyenyezi mahakamani

    Mahakama Kuu ya Huye kusini mwa nchini hiyo leo imeanza kusikiliza mashahidi wanaomtetea Beatrice Munyenyezi, ambaye alitimuliwa na Marekani na kupelekwa nchini Rwanda mwaka 2021 kujibu mashtaka ya mauaji ya kimbari yanayomkabili.

    Shahidi mmoja aliyekuwa afisa wa jeshi ameiambia mahakama kwamba hajui jukumu lolote la Bi Beatrice Munyenyezi katika mauaji ya kimbari.

    Alishtakiwa kwa makosa mauaji ya kimbari na ubakaji wa wanawake-mashtaka ambayo anakanusha- Shahidi wa kwanza 'Meja' Cyriaque Habyarabatuma ambaye alikuwa mkuu wa kikosi cha jeshi la 'gendarmerie' katika jimbo la zamani la Butare mwaka 1994 aliiambia mahakama hiyo kwamba alimfahamu Beatrice Munyenyezi na kwamba hakujua jukumu lolote lake katika mauaji ya kimbari mwaka 1994.

    Munyenyezi anatuhumiwa kuhusika na mauaji ya Watutsi waliokuwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rwanda, kuhamasisha wanamgambo Interahamwe kuua, na kuhusika na ubakaji wa wanawake na wasichana waliouawa kwenye vizuizi vya barabarani karibu na alipokuwa akiishi katikati yam ji wa Butare na kwingineko.

    Munyenyezi mwenye umri wa miaka 53 amekanusha mashtaka yote yanayomkabili, akisema kuwa wakati wa mauaji ya kimbari alikuwa na ujauzito wa mapacha na hangeweza kufanya mauaji.

    Cyriaque Habyarabatuma ambaye alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa ya mauaji ya kimbari akiwa amevalia sare za wafungwa mbele ya majaji alisema kuwa hana uhusiano wowote na Munyenyezi.

    ‘Alikuwa mjamzito ' Alipoulizwa iwapo Munyenyezi aliingia katika kambi ya kijeshi ya ESO na kuchukua vifaa vya kijeshi, Habyarabatuma alisema kuwa "hakuna raia anayeweza" kufanya hivyo.

    Alimtetea Munyenyezi akisema kuwa kamwe raia hawezi kutoa amri kwa askari kufanya lolote kwenye vizuizi vya barabarani vilivyokuwa katika mji wa Butare, “haiwezekani”.

    "Mwaka 1994, najua alikuwa na mimba akiwa karibu kujifungua .Niliambiwa kwamba alijifungua mapacha, tulikuwa tunamuona kwani ‘mimba huwezi kuificha.’

    Upande wa mashtaka ulimuuliza Meja Habyarabatuma wakati alipoondoka katika mji wa Butare,akasema kwamba aliondoka tarehe 19 mwezi wa 4 kabla ya mauaji kupamba moto katika mji huo.

    Mashtaka mengine ambayo Munyenyezi alishitakiwa ni kuweka vizuizi na kuwepo katika moja ya vizuizi hivyo na kutoa amri za kupekua raia hasa Watutsi.

    Shahidi mwingine aliyesikilizwa ni 'Staff Sergent’' Emmanuel Rekeraho ambaye alikuwa anasimamia 'ulinzi wa raia' katika kikosi cha gendarmerie huko Butare ambaye pia alihusika na kuweka vizuizi katika jiji la Butare.

    ReKereho alisema kuwa hakukuwa na kizuizi huko Butare ambako kulikuwa na msichana au mwanamke, hivyo Munyenyezi hakuwahi kuwepo katika kizuizi chochote.kesi bado inaendelea wakisikilizwa mashahidi wa utetezi.

  4. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini Tanzania yakiri tatizo la ajira ya utotoni bado lipo

      • Author, Aboubakar Famau
      • Nafasi, BBC News, Dodoma
    Mohammed Khamis Hamad
    Maelezo ya picha, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini Tanzania Mohammed Khamis Hamad

    Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini Tanzania imesema licha ya a jitihada mbalimbali zilizowekwa kukabiliana na ajira ya watoto, bado visa vya watoto kufanyishwa kazi ngumu hasa katika maeneo ya kazi za ndani, mitaani na migodini vingalipo.

    Akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo jijini Dodoma, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Mohammed Khamis Hamad ameitaka serikali kushirikiana na wadau mbalimbali ili kudhibiti hali hiyo.

    Kauli hiyo, imetolewa wakati ambapo dunia inaadhimisha siku ya kupinga ajira kwa watoto.

    Tume hiyo pia imesema itaendelea kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ajira hizo kwa kupitia kauli mbiu ya mwaka huu inayosema, ”Haki ya Jamii kwa Wote, Kukomesha Ajira kwa Watoto.”

    ”Ajira hizi zimekuwa kichocheo cha ukatili dhidi ya watoto ambao baadhi yao hukosa masomo, kunyonywa kiuchumi, kwa kulipwa ujira mdogo na matatizo ya kiafya, hivyo kuathiri ukuaji wao,” amesema Makamu Mwenyekiti.

    Kwa mujibu wa Tume, miongoni mwa sababu zinazochangia kuendelea kuwepo kwa ajira hizo, ni pamoja na umaskini na jamii kukosa uelewa juu ya madhara ya kutumikisha watoto walio chini ya umri rasmi wa kufanya kazi.

    Hivyo, ili kukabiliana na baadhi ya changamoto hizo, Tume imetoa mapendekezo miongoni mwao ikiwa ni pamoja na kuitaka serikali kuendelea kuhamasisha hatua za kimataifa kufikia haki ya kijami na kuondoa ajira kwa watoto.

    Vilevile wazazi na walezi wametakiwa kuhakikisha wanawatunza watoto na kuwalinda ili kuwaepusha na ukatili wa ajira za utotoni.

    Tatizo la ajira kwa watoto sio changamoto nchini Tanzania pekee bali katika mataifa mingi duniani.ambalo linaonekana kuwa sugu nchini Tanzania na maeneo mengine.

    Duniani kwa ujumla, watoto takriban milioni 72 wanakadiriwa kuwa katika ajira za utotoni, huku milioni 31.5 kati yao wakiwa katika ajira hatarishi.

    Nchini Tanzania, nusu ya idadi ya watu wana umri chini ya miaka 18. Takwimu zinaonesha, takriban milioni 4.2 ya watoto wenye umri kati ya miaka 5 hadi 17 wameingia katika ajira za utotoni.

  5. Ligi ya Mabingwa Afrika: Al Ahly watwaa taji la 11 baada ya kushinda Wydad Casablanca

    TH

    Al Ahly ya Misri wametawazwa kuwa washindi wa Ligi ya Mabingwa Afrika - tena - baada ya kuifunga Wydad Casablanca.

    Siku ya Jumapili usiku, klabu iliyofanikiwa zaidi ya kandanda barani Afrika ilishinda taji la 11 la bara lililoongeza rekodi.

    Sare ya 1-1, na kusawazisha dakika za lala salama, iliwapa ushindi wa jumla wa 3-2 dhidi ya Wydad.

    Pande hizo zilikutana katika mechi moja mwaka jana, wakati Wydad ilipotwaa ubingwa kwa mara ya tatu.

    Mwaka huu, Wamisri walisafiri hadi Morocco wakiwa mbele kwa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza.

    Kabla ya kuanza kwa mchezo huo, wafuasi wa Wydad walipanga foleni kwa saa nyingi nje ya uwanja wa Mohamed V huko Casablanca.

    Umati huo wa watu 60,000 uliipatia timu yao uungwaji mkono kutoka uwanjani, wakipiga miluzi ya viziwi wakati Al Ahly walipokuwa kwenye mpira na kuwazomea wachezaji wao mbele walipopata mpira tena.

    Mwamuzi wa Ethiopia Bamlak Tessema aliwekwa chini ya shinikizo kubwa baada ya kufanya maamuzi - wachezaji kadhaa kutoka kila upande hata waliwasiliana naye kimwili mara kadhaa.

  6. MSF yaonya kuhusu wakimbizi wa Sudan 'walionaswa na kusahauliwa' Chad

    Mwanamke

    Maelfu ya wakimbizi wa Sudan mashariki mwa Chad huenda "wakakwama na kusahaulika" msimu wa mvua unapoanza, shirika la misaada la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) linasema.

    Maeneo yanayokaliwa na wakimbizihuenda yakatengwa, kwani mito inajaa maji na kufurika katika eneo linalozunguka, kulingana na MSF.

    Ghasia za hivi majuzi nchini Sudan zimefanya zaidi ya watu 100,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kukimbilia nchi jirani ya Chad.

    Baadhi yao wanaishi katika maeneo ambayo tayari yana idadi kubwa ya wakimbizi na yanaathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

    "Tunakabiliwa na mzozo juu ya nyingine," shirika la misaada lilisema katika taarifa.

    Linaongeza kuwa watu huenda wakaamua kurejea Sudan kukabiliana na ghasia zaidi huku hali nchini Chad ikizidi kuwa mbaya.

    MSF imetoa wito wa kuongezwa kwa juhudi za kimataifa za kushughulikia hali nchini Chad.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Wanamgambo wawaua zaidi ya watu 40 mashariki mwa DR Congo

    th

    Wanamgambo wa kundi linalojulikana kama Codeco (Cooperative for Development of the Congo) wametuhumiwa kufanya shambulio dhidi ya kambi ya wakimbizi wa ndani waliotoroka makazi yao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuwaua zaidi ya watu 40.

    Maafisa wa eneo hilo walisema kundi hilo lilivamia kambi ya Lala mapema Jumatatu, na kuwafyatulia risasi wakazi kabla ya kuchoma moto nyumba zao.

    Baadhi ya waliokuwa ndani walichomwa moto hadi kufa.

    Ni shambulio la hivi punde zaidi la kundi hilo, ambalo linadai kutetea maslahi ya wakulima wa Lendu.

    Maelfu ya watu wamekimbia vijiji vilivyoko karibu katika wiki za hivi karibuni kutafuta hifadhi katika mji wa Bule, ambako kuna walinda amani wa Umoja wa Mataifa.

    Maelezo zaidi:

    • Fahamu baadhi ya makundi ya waasi yanayoyumbisha amani ya DR Congo
    • DR Congo: Je taifa hili limelaaniwa na utajiri wake?
    • Mzozo wa DRC na Rwanda : M23, majirani na bahati mbaya ya DRC
  8. Aliyekuwa waziri mkuu wa Italia Silvio Berlusconi aaga dunia

    .
    Maelezo ya picha, Silvio Berlusconi

    Silvio Berlusconi, Waziri Mkuu wa zamani wa Italia ambaye alijiondoa kutoka kwa kashfa za ngono na tuhuma za ufisadi, amefariki akiwa na umri wa miaka 86.

    Alikufa katika hospitali ya San Raffaele huko Milan, kulingana na vyombo vya habari vya Italia.

    Mnamo Aprili alitibiwa maambukizi ya mapafu yaliyohusishwa na kisa ambacho hakikutajwa hapo awali cha leukemia ya muda mrefu.

    Tajiri huyo wa vyombo vya habari, Berlusconi aliingia ofisini kwa mara ya kwanza mwaka wa 1994 na aliongoza serikali nne hadi 2011.

    Aliongoza chama cha mrengo wa kati cha Forza Italia ambacho kiliingia katika muungano chini ya Waziri Mkuu Giorgia Meloni baada ya uchaguzi wa Septemba, wakati yeye mwenyewe alichaguliwa katika baraza la juu la Italia, Seneti.

    Akijibu habari hizo, Waziri wa Ulinzi wa Italia Guido Crosetto alisema kifo cha Berlusconi kiliacha "pengo kubwa".

    "Enzi imekwisha... Farewell Silvio," Bw Crosetto aliandika kwenye ujumbe wa tweeter, akiongeza kwamba "alimpenda" Berlusconi "sana".

    Kiongozi huyo wa zamani alikuwa akiugua aina adimu ya saratani ya damu, leukemia ya muda mrefu ya myelomonocyte, madaktari wa San Raffaele waliwaambia waandishi wa habari mapema mwaka huu.

    Kufikia sasa, hakuna uthibitisho rasmi wa chanzo cha kifo chake cha ghafla. Amekuwa na matatizo ya kiafya mara kwa mara tangu kuambukizwa Covid mnamo 2020.

    Alizaliwa mwaka wa 1936 huko Milan, Berlusconi alianza kazi yake ya kuuza vifaa vya usafi , kabla ya kuanzisha kampuni ya ujenzi.

    Aliendelea kuwa mmoja wa watu tajiri zaidi wa Italia, akitengeneza utajiri wake kupitia chaneli zake za TV.

    Alipata kutambuliwa kimataifa kama mmiliki wa klabu maarufu ya soka ya AC Milan - ambayo aliiokoa kutokana na kufilisika mwaka 1986 - kabla ya kuingia kwenye siasa.

    Silvio
  9. Rais wa Uganda aweka ujumbe Twitter baada ya tetesi za kuwa ICU na za kifo

    .

    Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameweka ujumbe kwenye mtandao wa Twitter jana na kusema kuwa bado anajitenga kufuatia uvumi wa mitandao ya kijamii kwamba amefariki kutokana na Covid-19.

    Museveni alipimwa na kukutwa na Covid-19 mnamo tarehe 7 Juni na akasema siku iliyofuata kwamba alikuwa akichukua "likizo ya lazima".

    "Salamu. Leo ni siku ya tano ya hali yangu ya corona. Jana usiku, nililala vizuri sana hadi saa kumi za usiku," kiongozi huyo wa Uganda alisema kupitia ujumbe mrefu kwenye Twitter.

    Aliwataka Waganda kwenda kupata chanjo ya Covid na ile ya nyongeza, haswa kwa wazee.

    Uvumi umeibuka kwenye Twitter katika siku chache zilizopita kwamba Museveni alihamishiwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi na baadaye kufariki kutokana na matatizo ya Covid.

    Shirika la Afya Ulimwenguni lilitangaza mwezi uliopita kwamba Covid haikuwa tena dharura ya tatizo la afya ulimwengu, lakini ilionya kwamba virusi hivyo vitaendelea kubadilika.

  10. Marekani, Saudi Arabia washtumu kurejea kwa ghasia nchini Sudan

    .
    Maelezo ya picha, Wakaazi waripoti mashambulizi ya anga na kurushiana risasi

    Marekani na Saudi Arabia zimeshtumu kuanzishwa tena kwa ghasia katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, ambapo wakaazi wameripoti mashambulizi ya anga na kukabiliana kwa silaha.

    Katika taarifa ya pamoja nchi hizo mbili zilibainisha kuwa jeshi la Sudan na Vikosi vya Rapid Support Forces vilidhibiti vikosi vyao wakati wa usitishaji mapigano wa masaa 24, na inasikitisha sana kwamba mapigano yalianza tena.

    Kikundi cha ujirani kinachounga mkono demokrasia kimesema makombora yametua katika makazi ya watu kusini mwa mji mkuu kufuatia kumalizika kwa muda wa usitishaji mapigano.

    Mkazi mmoja aliyeamshwa na sauti ya mapigano, alisema utulivu wa siku moja Jumamosi ni sawa na ndoto ambayo sasa imetoweka.

    Soma zaidi:

  11. Biden ashiriki hafla na watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja Ikulu

    .

    Rais wa Marekani Joe Biden aliandaa sherehe kubwa ya kujivunia katika historia ya Ikulu ya White House siku ya Jumamosi, akitaka hatua mpya za kulinda haki na usalama wa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja huku kukiwa na msururu wa kile alichokiita mashambulizi na sheria za "kutisha".

    Biden, Mwanademokrasia, alihimiza Bunge kupitisha "Sheria ya Usawa" ambayo ingerekebisha Sheria ya Haki za Kiraia ya 1964 ili kujumuisha jinsia zote na utambulisho wa kijinsia kwa ajili ya ulinzi dhidi ya ubaguzi wa rangi, dini, jinsia na asili ya kitaifa, na kupiga marufuku uvamizi wa kutumia silaha dhidi yao.

    Maelfu ya wageni walipiga picha akiwemo Katibu wa Uchukuzi Pete Buttigieg, mtu wa kwanza wa LGBTQ waziwazi kushikilia wadhifa wa Baraza la Mawaziri, na Katibu Msaidizi wa Afya na Huduma za Kibinadamu Admiral Rachel Levine, mtu wa kwanza aliyebadili jinsia wazi kuthibitishwa na Seneti.

  12. Ajali ya ndege Colombia: Mama aliwaambia watoto wamuache na waende kutafuta usaidizi

    .
    Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Colombia wanahudumia watoto hao wanne muda mfupi baada ya kupatikana

    Mama wa watoto wanne waliookolewa baada ya siku 40 kwenye msitu wa Amazon alikuwa hai kwa siku nne baada ya ndege yao kuanguka.

    Magdalena Mucutuy aliwaambia watoto wake waondoke wakatafute msaada huku akiwa amelala hana cha kufanya.

    Akizungumza na waandishi wa habari, baba wa watoto hao, Manuel Ranoque, alisema binti yake mkubwa alimwambia mama yao aliwataka "watoke nje" na kujiokoa.

    Ndugu hao wenye umri wa miaka 13, tisa, mitano na mmoja waliokolewa na kusafirishwa kwa ndege kutoka msituni siku ya Ijumaa.

    Walihamishiwa katika hospitali ya kijeshi katika mji mkuu wa taifa hilo Bogota.

    "Jambo moja ambalo [Lesly mwenye umri wa miaka 13] amenielewesha ni kwamba, kwa hakika, mama yake alikuwa hai kwa siku nne," Bw Ranoque aliwaambia wanahabari nje ya hospitali.

    "Kabla hajafa, mama yao aliwaambia kitu kama, 'Nyinyi nyinyi ondokeni hapa. Nyinyi mtaona baba yenu ni mtu wa aina gani, na atawaonyesha upendo wa aina ile ile ambao nimewaonyesha," alisema.

    Maelezo yamekuwa yakiibuka kuhusu wakati wa watoto hao msituni na uokoaji wao wa kimiujiza - ikiwa ni pamoja na mambo ya kwanza ambayo watoto walisema walipopatikana.

    Mfanyakazi wa uokoaji Nicolas Ordonez Gomes alikumbuka wakati walipogundua watoto hao.

    "Binti mkubwa, Lesly, akiwa na mtoto mdogo mikononi mwake, alikimbia kuelekea kwangu. Lesly alisema: 'Nina njaa,'" aliambia kituo cha matangazo ya umma RTVC.

    "Mmoja wa wavulana wawili alikuwa amelala chini. Aliinuka na kuniambia: 'Mama yangu amekufa.'"

    Alisema waokoaji walimjibu kwa "maneno mazuri, wakisema kwamba sisi ni marafiki, kwamba tulitumwa na familia".

    Bw Ordonez Gomes alisema mvulana huyo alijibu: "Nataka mkate na soseji."

    Katika picha zilizotolewa Jumapili za uokoaji wa watoto hao, ndugu hao wanne walionekana kudhoofika kutokana na wiki walizotumia kujihudumia nyikani.

    Bi Mucutuy na watoto wake walikuwa wakisafiri kwa ndege ya Cessna 206 kuelekea Araracuara, katika jimbo la Amazonas, hadi San José del Guaviare, tarehe 1 Mei wakati ilipotoa tahadhari kwa ajili ya hitilafu ya injini.

    Soma zaidi kisa hiki:

  13. Ukraine yatangaza ushindi wa kwanza katika vita vya kuikabili Urusi

    .

    Ukraine ilitangaza kurejesha makaazi yake ya kwanza tangu rais huyo akubali kwamba mashambulizi ya muda mrefu yaliyokuwa yameahidiwa yalikuwa yakiendelea.

    Wakati huo huo, Ukraine imeishutumu Urusi kwa kulipua bwawa dogo - kufuatia uvunjaji wa bwawa kuu la Kakhovka wiki moja iliyopita. Urusi bado haijatoa maoni.

  14. Michael Travis Leake, mwanamuziki wa Marekani, azuiliwa nchini Urusi

    .

    Mahakama ya Urusi imemzuilia raia wa Marekani Michael Travis Leake, mwanamuziki na mwanajeshi wa zamani wa paratrooper, kwa tuhuma za kutumia dawa za kulevya.

    Mahakama ya Khamovnichesky ya Moscow ilidai kuwa Bw Leake "alipanga uuzaji wa dawa za kulevya kwa vijana", AFP iliripoti.

    Hata hivyo, anakanusha mashtaka hayo.

    Televisheni ya serikali ya Urusi ilitangaza kanda ya kesi ya Bw Leake iliyomuonyesha akiwa amefungwa kwenye ngome ya chuma.

    Katika video tofauti iliyoshirikishwa mtandaoni, alisema "hakujua" kwa nini alizuiliwa.

    Huku akionekana kuchanganyikiwa, alisema haamini kuwa amefanya kile anachotuhumiwa, kwa sababu hajui ni mashtaka gani.

    The department was closely monitoring the case, the spokesperson added.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema wafanyakazi wa ubalozi walihudhuria kusikilizwa kwa kesi ya Bw Leake siku ya Jumamosi, 10 Juni.

    Idara ilikuwa ikifuatilia kesi hiyo kwa karibu, msemaji huyo aliongeza.

    Atazuiliwa rumande hadi tarehe 6 Agosti, AFP iliripoti.

    Bw Leake ni angalau Mmarekani wa tatu kuzuiliwa nchini Urusi katika miaka ya hivi karibuni huku kukiwa na mvutano mkali kati ya Washington na Moscow.

    Mwanamuziki na mtayarishaji wa muziki aliripotiwa kuishi nchini Urusi kwa miaka mingi, Bw Leake alikuwa mwanachama wa Lovi Noch, "bendi ya muziki ya Marekani" iliyoko Moscow.

    Chombo cha habari cha Marekani CNN kiliripoti kwamba alionekana kwenye kipindi cha usafiri cha Parts Unknown - kilichoandaliwa na mpishi marehemu Anthony Bourdain - kwa kipindi cha 2014 ambacho kilirekodiwa huko Moscow na St Petersburg.

    Darya Tarasova, ambaye alitayarisha kipindi hicho, aliiambia CNN kwamba Bw Leake alikuwa "mtangazaji" ambaye "alizungumza sana" na "aliyependa Urusi".

    Mara nyingi alifanya kazi na bendi za hapa, Bi Tarasova alisema.

    Vyombo vya habari vya Urusi viliripoti mapema kukamatwa kwake katika nyumba yake huko Moscow.

    Maafisa wa Marekani hapo awali waliishutumu Urusi kwa kuwalenga kimakusudi raia wa Marekani ili kuwakamata.

    Mnamo Machi, mamlaka ya Urusi ilimkamata mwandishi wa habari wa Marekani Evan Gershkovich, mwandishi wa Wall Street Journal, kwa mashtaka ya ujasusi.

    Bado anaendelea kuzuiliwa kabla ya kesi inayomkabili kusikilizwa.

    Mwishoni mwa mwaka jana, mchezaji wa mpira wa vikapu wa Marekani Brittney Griner, ambaye alifungwa nchini Urusi kwa mashtaka ya madawa ya kulevya, aliachiliwa kwa kubadilishana wafungwa kwa muuzaji silaha wa Kirusi Viktor Bout

    Mwanajeshi wa Marekani Paul Whelan anatumikia kifungo cha miaka 16 jela kwa makosa ya "kijasusi" - alihukumiwa kabla ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, ambako kumedhoofisha uhusiano kati ya Marekani na Urusi.

  15. Watu 10 wafariki dunia katika ajali ya basi la harusi Australia

    .
    Maelezo ya picha, Basi hilo lilipinduka wakati likigeuka kwenye mzunguko wa barabara usiku wa Jumapili

    Takriban watu 10 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 20 wamelazwa hospitalini baada ya basi la harusi kuanguka katika eneo la mvinyo nchini Australia.

    Abiria hao walikuwa wakirejea kutoka harusini katika kiwanda cha mvinyo Jumapili usiku wakati pale dereva wao alipopinduka kwenye eneo karibu na Greta huko Hunter Valley, New South Wales.

    Polisi wanasema wanachunguza chanzo cha ajali hiyo.

    Dereva wa basi hilo mwenye umri wa miaka 58 amekamatwa.

    Kaimu Kamishna Msaidizi wa Polisi Tracy Chapman alisema wageni walikuwa wakisafiri hadi Singleton "pengine kwa ajili ya malazi yao".

    Ajali hiyo ilitokea mwendo wa 23:30 saa za eneo - basi lilibingiria lilipokuwa likizunguka kwenye barabara kuu.

    Idadi ya waliofariki inaweza kuongezeka, huku abiria 25 wakipelekwa hospitalini - wawili kati yao wakisafirishwa kwa ndege kutoka kwenye ajali hiyo, Bi Chapman alisema.

    Aliongeza kuwa basi bado limelala upande na huenda kuna watu walionaswa kwa chini, na kreni italetwa kwenye eneo la tukio "katika hatua fulani" ili kuinua basi.

    Bi Chapman alisema kuna "taarifa za kutosha" kwa polisi kumfungulia mashtaka dereva wa kochi, ambaye pia alipelekwa hospitali na kutibiwa majeraha madogo. "Amekamatwa.

    Pia alisema kumekuwa na ukungu mkubwa katika eneo hilo wakati wa ajali hiyo.

  16. Gari lako litachukuliwa': Wanawake wa Iran wanakaidi sheria ya kuvaa hijab licha ya vitisho

    .
    Maelezo ya picha, Baadhi ya wanawake nchini Iran wanachagua kutofunika nywele zao kama sehemu ya maandamano yanayoendelea

    Wanawake nchini Iran wanakaidi majaribio mapya ya mamlaka ya kutumia teknolojia kutekeleza kanuni za mavazi za lazima ambazo zimekuwa zikilengwa katika kuendeleza maandamano kote nchini.

    Mnamo Aprili, mkuu wa polisi wa kitaifa Ahmad Reza Radan alitangaza kuanzishwa kwa programu ya "smart" inayohusisha kamera za uchunguzi ili kutambua wanawake wanaoshindwa kufunika nywele zao au kuvaa mavazi yasiyokubalika licha ya tishio la faini au kifungo.

    Alionya kuwa watakaopatikana wakivunja sheria ya kuvaa hijabu kwa mara ya pili watafikishwa mahakamani, magari yatakayobeba abiria wa kike wakiwa na nywele ambazo hazijafunikwa yatachukuliwa na kwamba biashara hizo zitafungwa.

    Hata hivyo, tangazo lake liliibua majibu ya dhihaka kwenye mitandao ya kijamii, huku wanawake wakichapisha picha na video zao wakiwa hawajavaa hijabu katika maeneo ya umma kote nchini.

    Ujumbe wa tahadhari kwa kusafiri bila kuvaa hijab

    Kwa miaka kadhaa, watu wameripoti kupokea jumbe za onyo kuhusu ukiukaji wa kanuni za mavazi ndani ya magari yao baada ya kutambuliwa na kamera za kudhibiti trafiki.

    Lakini hii ni mara ya kwanza kwa mamlaka kutishia kutaifisha magari au kutoza faini watu kwa hilo.

    "Nilipokea ujumbe zaidi ya mwezi mmoja uliopita ambao uliandika nambari yangu ya leseni baada ya kusafiri na marafiki zangu wa kike hadi jiji la Damghan. Hatukuwa tumevaa hijabu kwenye magari yetu," mwanamke mmoja aliambia BBC.

    Watu wengine wameripoti kupokea jumbe kama hizo, ambazo zinawaonya kuwa magari yao yatachukuliwa ikiwa wataonekana hadharani bila hijabu tena. Ujumbe huo pia unajumuisha viunganishi vya tovuti ambapo wanaweza kupinga kosa linalodaiwa.

    Mwanamume mmoja alisema alitumiwa ujumbe ulioorodhesha nambari ya leseni ya gari lake na eneo ambalo alikuwa ameendesha siku fulani, "lakini sikuwa na mwanamke wakati huo mahali hapo".

    "Nilikuwa peke yangu. Kamera zao sio sahihi sana," aliongeza.

    Mwanamume huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, alituma picha kwa BBC kuonyesha kuwa alikuwa na nywele ndefu.

    Wanaume pia wameripoti kwamba kufuatia tangazo la Aprili walipokea ujumbe kutoka kwa polisi ukisema: "Ndugu raia, ni muhimu kuheshimu na kuzingatia sheria ya hijabu."

    Walikejeli hatua hiyo, huku mwanamume mmoja akiandika kwenye Instagram:

    "Je, huu ndio ustadi wa teknolojia yenu?"

    Baadhi ya mawakili wameteta kuwa hatua hii mpya ya polisi na mahakama ni kinyume cha sheria.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya leo