Tetemeko la Ardhi Uturuki: Juhudi za uokoaji zinaendelea huku idadi ya waliokufa wakifika zaidi ya 20,000

Idadi ya vifo kutoka nchi zote mbili ilitarajiwa kuongezeka kwani mamia ya majengo yaliyoporomoka katika miji mingi yamekuwa makaburi ya watu waliokuwa wamelala wakati tetemeko hilo lilipotokea.

Moja kwa moja

  1. Mpaka hapa tumefika mwisho wa matangazo ya moja kwa moja ya ukurasa wetu wa BBC Swahili, Shukrani

  2. Urusi yaitaka Sudan kutatua changamoto zake za kisiasa

    m

    Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi, Sergey Lavrov, amekutana na watawala wa kijeshi wa Sudan na kuitaka nchi hiyo kutatua changamoto zake za kisiasa ndani ya nchi bila kile alichokitaja kama "majaribio ya kuwafundisha Wasudani jinsi ya kufanya mambo yao".

    Nchi hiyo imekuwa katika migogoro ya kisiasa tangu majenerali walipowaondoa viongozi wa kiraia wanaoungwa mkono na nchi za Magharibi wa serikali ya mpito mnamo Oktoba 2021.

    Urusi na Sudan pia zimekuwa katika mazungumzo kuhusu kufungua kituo cha jeshi la majini nchini Sudan karibu na Bahari nyekundu.

    Bw Lavrov amesema mpango huo sasa unasubiri kuidhinishwa, lakini Sudan kwa sasa inakabiliwa na mzozo wa kisiasa wa muda mrefu.

    Wanadiplomasia wa nchi za Magharibi walikutana na watawala wa kijeshi kabla ya ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Urusi, na kupokea uhakikisho wa kujitolea kwa baraza hilo kwa makubaliano yaliyokusudiwa kusababisha serikali ya mpito ya kiraia.

    Lakini Bw Lavrov amekosoa uungaji mkono wao kwa mchakato huo.

    Pia aliwashutumu viongozi wa Magharibi kwa kumfuatilia anapozuru bara la Afrika.

    Hii ni safari yake ya tatu ndani ya miezi sita pekee.

    Bara linaona maslahi mapya kutoka kwa mataifa yenye nguvu duniani ambayo yanatafuta kuongeza ushawishi wao.

    Soma zaidi:

    • Mizizi ya Urusi barani Afrika inavyokuzwa kwa safari ya Lavrov nchini Mali
    • Ukraine yajiandaa kwa mashambulizi mapya ya Urusi baadaye mwezi Februari
  3. Malawi yakumbwa na kipindupindu kibaya zaidi kuwahi kutokea- WHO

    m

    Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa Malawi inapitia mlipuko mbaya zaidi wa kipindupindu kuwahi kutokea.

    Watu zaidi ya 1,200 wamekufa kutokana na kipindupindu katika mwaka uliopita.

    Ni wilaya mbili tu ndio hazijaathirika kati ya Wilaya zote 29.

    Kumekuwa na kampeni kubwa mbili za chanjo, lakini, kutokana na uhaba wa vifaa, watu wamepewa dozi moja tu ya kumeza badala ya mbili zilizopendekezwa.

    Shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa limesema juhudi zinaendelea kuboresha usafi wa mazingira na upatikanaji wa maji safi kwa kutumia klorini ya nyumba hadi nyumba katika maeneo yaliyoathirika.

    Inasema kumekuwa na ongezeko la milipuko ya kipindupindu duniani kote, jambo ambalo limesababisha uhaba wa chanjo.

    Soma zaidi:

    • Kipindupindu: Ugonjwa rahisi kuupata, rahisi kuukwepa na rahisi kukuua
  4. Tazama: 'Walimzika kaka yangu bila sisi kuwepo'

    Maelezo ya video, Tetemeko la ardhi Uturuki: 'Walimzika kaka yangu bila sisi kuwepo'

    Baada ya tetemeko kubwa la ardhi kukumba Uturuki, baadhi ya watu wamekuwa wakisafiri kote nchini humo kuwafikia wapendwa wao waliokumbwa na janga hilo, au kuchukua miili yajamaa zao.

    Mwandishi wa BBC Selin Girit aliungana na baadhi yao katika safari hiyo kwa zaidi ya saa 30 kuelekea mji wa Maras, ambao ulikuwa karibu na kitovu cha tetemeko la ardhi la pili siku ya Jumatatu.

  5. Kesi ya noti mpya Nigeria yapuuziwa, Mwanasheria Mkuu wa Nigeria asema

    m

    Mwanasheria Mkuu wa Nigeria Abubakar Malami ameiomba Mahakama ya Juu kutupilia mbali kesi iliyowasilishwa na magavana watatu wa majimbo ambayo yamesitisha kuanzishwa kwa noti mpya za naira.

    Ofisi ya mwanasheria mkuu inasema kuwa Mahakama ya Juu haina mamlaka ya kutoa uamuzi kuhusu masuala ambayo kesi hiyo inaibua.

    Kukiwa na uchaguzi muhimu ujao, Festus Okoye, Kamishna wa Kitaifa wa shirika la uchaguzi la Nigeria Inec, aliiambia BBC kuwa hii haitaathiri uchaguzi mkuu na "tarehe zilizowekwa na tume kwa ajili ya kuendesha uchaguzi mkuu zimewekwa na ni thabiti."

    Mwezi Novemba mwaka jana, Benki Kuu ya Nigeria ilibuni upya noti za naira 200, 500, na 1,000 kwa lengo la kuzuia mfumuko wa bei unaoongezeka, uhifadhi wa fedha na bidhaa ghushi.

  6. Watu wanne wakwama kwenye kifusi baada ya mgodi kuporomoka Kenya

    m

    Wachimba migodi wanne wamenaswa kwenye vifusi baada ya mgodi wa dhahabu kuporomoka Magharibi mwa Kenya.

    Tukio hilo la saa moja asubuhi liliwaacha wafanyikazi 12 wa ufundi wakiwa wamenaswa kwa saa kadhaa.

    Wachimba migodi wanane waliokolewa leo asubuhi baada ya saa kadhaa za kuchimba vifusi na wako katika hali nzuri.

    Mamlaka iliyotembelea eneo la tukio, ilisema wachimbaji hao walikuwa wakitafuta dhahabu katika mgodi wa zamani.

    Kamishna wa Kaunti ya Kakamega Bw John Ondego alizua wasiwasi kuhusu shughuli hizo katika kaunti hiyo akisema ni kinyume cha sheria kwa vile hazijaidhinishwa na serikali ya kaunti hiyo.

    “Wanachofanya ni kuhatarisha maisha yao na watu wengi hapa wengi wao ni vijana ambao wanafanya kazi hii. Kutokana na tatizo la ukosefu wa ajira, watu wanafanya kila wawezalo kijikimu kimaisha ,” alisema Kamishna wa Kaunti.

    Alionya kuwa shughuli za usiku katika vichuguu vya uchimbaji madini hazitaruhusiwa katika kaunti.

    Shughuli za uokoaji zinaendelea kuwanusuru wachimbaji wanne waliosalia kutoka kwenye kifusi.

    Matukio ya migodi kuporomoka yamekithiri katika maeneo ya Magharibi mwa Kenya huku kukiwa na kumbukumbu za kutokea kwa amana za dhahabu.

    Shughuli za uchimbaji madini ni chanzo cha maisha kwa idadi kubwa ya watu huku wengine wakipoteza maisha wakitafuta bidhaa hiyo ya thamani.

    Mnamo mwaka 2021, kampuni ya uchunguzi ya Shanta Gold iliripoti ugunduzi wa amana kubwa ya dhahabu katika kaunti ya magharibi, wakati serikali inapanga kujenga kiwanda cha kusafisha dhahabu katika eneo hilo.

  7. Uganda kuwatoza faini madereva wasio na mahali pa kuweka taka kwenye gari

    m

    Shirika la usimamizi wa mazingira nchini Uganda linasema litaanza kutoza faini kuanzia mwezi Aprili kwa madereva wanaoendesha magari ya kibinafsi bila ya kuwa na chombo cha kuhifadhia takataka.

    Wahalifu watakabiliwa na faini ya juu zaidi ya hadi shilingi 6,000,000 za Uganda ($1,630), kwa mujibu wa mpango wa adhabu uliotangazwa Jumatano.

    Waendeshaji magari wanaokataa kulipa faini watakabiliwa na mashtaka na kifungo au faini itakayoamuliwa na mahakama, shirika hilo lilisema katika taarifa.

    Hivi sasa mabasi ya abiria yanayosafiri umbali mrefu nchini humo yanalazimika kuwa na chombo cha takataka.

    Lakini ni hitaji jipya la chombo cha taka katika magari ya kibinafsi ambalo limepata usikivu wa Waganda, huku wengi wakiuliza kama kulikuwa na kiwango fulani cha kile kinachozingatiwa kama pa kuwekea taka.

    "Mradi tu unatumia kitu ambacho hakiruhusiwi kuweka takataka zako, unapaswa kuwa sawa. Mifuko ya plastiki imepigwa marufuku," Naomi Karekaho, msemaji wa shirika hilo, aliiambia BBC.

    Alisema shirika hilo litachukua ufafanuzi wa kile kinachozingatiwa kama chombo cha taka katika marekebisho yanayofuata.

    "Kati ya adhabu zote za uvunjaji wa mazingira ambazo tulitangaza hii inaonekana kuwa imevutia watu wengi. Labda ni msisimko mkubwa wa kuwa na chombo cha taka kwenye gari," aliongeza.

  8. Wanandoa waliobadili jinsia wapata mtoto

    ZIYA PAVAL/INSTAGRAM

    Wanandoa waliobadili jinsia kutoka jimbo la kusini mwa India la Kerala, ambao picha zao za ujauzito zilienea katika habari za kimataifa, wamemkaribisha mtoto wao kwa "machozi ya furaha".

    Ziya Paval alisema mpenzi wake Zahad alikuwa amejifungua mtoto huyo Jumatano asubuhi.

    Bi Paval aliweka habari hiyo kwenye Instagram, akiweka picha ya mtoto huyo ambaye alizaliwa karibu mwezi mmoja uliopita.

    Waliambia BBC kwamba Bw Zahad na mtoto huyo, ambaye hawajataja jina na jinsia yake, walikuwa sawa.

    Bi Paval na Bw Zahad, ambaye anatumia jina moja pekee, wamesema ilikuwa ndoto yao kuwa wazazi.

    Wenzi hao walikuwa wamesitisha matibabu yao ya homoni wakati wa ujauzito.

    Mimba yao ilionekana kuwa ni adimu nchini India kwa sababu "hakuna mtu mwingine ambaye amejiita mzazi wa kibaolojia katika jamii ya watu waliobadili jinsia tunavyojua", wenzi hao waliambia BBC mapema wiki hii.

    ZIYA PAVAL/INSTAGRAM

    Wawili hao walikuwa katika hatua tofauti za mabadiliko ya kijinsia walipoamua kupata mtoto mwaka mmoja na nusu uliopita.

    Kisha walikuwa wamesitisha matibabu yao ya homoni kwa ushauri wa daktari.

    Siku ya Jumatano, walipokuwa wakishiriki picha ya mtoto huyo, wenzi hao wa ndoa walisema wanashukuru kwa maombi na uungwaji mkono kutoka kwa watu wao wa karibu.

    Tangu kutangazwa kwa mtoto huyo kuzaliwa, pongezi zimemiminika kwa wanandoa hao kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii.

    Bw Zahad, mhasibu, alisema alipanga kurejea kazini baada ya miezi miwili huku Bi Paval akimtunza mtoto.

    Soma zaidi:

    • Kerala: Wanandoa waliobadili jinsia ambao picha zao za ujauzito zilisambaa
  9. Rais wa Eritrea apuuzilia mbali ripoti za uhalifu wa kivita Ethiopia

    Rais wa Eritrea Isaias Afwerki amepuuzilia mbali ripoti za madai ya uhalifu wa kivita uliofanywa na wanajeshi wake wakati wa vita Kaskazini mwa Ethiopia.

    Katika kauli adimu kuhusu vita hivyo vilivyoanza Novemba 2020, Afwerki alisema madai hayo ni sehemu ya kampeni ya upotoshaji habari iliyofanywa na wakosoaji wa makubaliano ya amani yaliyofikiwa kati ya serikali ya Ethiopia na vikosi vya Tigray kwa ajili ya usitishaji wa kudumu wa uhasama katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

    Pia alikataa kujibu maswali kuhusu ni lini wanajeshi wa Eritrea wataondoka kikamilifu katika eneo la Tigray.

    Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanadai wanajeshi wa Eritrea wamefanya ukatili Kaskazini mwa Ethiopia ambao ni pamoja na kuua raia wasio na silaha, kuwabaka wanawake na uporaji mkubwa wa mali za umma na za kibinafsi.

    Rais Afwerki alikuwa akizungumza nchini Kenya kufuatia mkutano wa pande mbili na mwenzake William Ruto.

    Bw Isaias alichukua mamlaka wakati wa uhuru mwaka 1993, lakini nchi hiyo haijawahi kufanya uchaguzi wa kitaifa huku wakosoaji wakimtuhumu kwa kuwafunga jela watu wanaopinga utawala wake.

  10. Tetemeko la ardhi Uturuki na Syria: Miili yapatikana wakati wa utafutaji timu ya mpira wa wavu

    Wanafunzi

    Miili mitatu imepatikana huku waokoaji nchini Uturuki wakitafuta miili zaidi ya kundi la wachezaji wa mpira wa wavu wa shule katika jengo la hoteli iliyoporomoka jkufuatia tetemeko la ardhi lililotokea Jumatatu.

    Miili ya walimu wawili na mwanafunzi ilipatikana katika Hoteli ya Isias huko Adiyaman, walisema maafisa wa eneo la kaskazini mwa Cyprus linalodhibitiwa na Uturuki.

    Kundi la watu 39 - ikiwa ni pamoja na timu za wavulana na wasichana - wanasemekana walikuwa kwenye jengo hilo wakati lilipoanguka.

    Matetemeko hayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu kusini mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria.

    Wanariadha hao walikuwa wamesafiri hadi Adiyaman kutoka Chuo cha Famagusta Turkish Maarif, wakiandamana na walimu na wazazi.

    Vyombo vya habari vya Uturuki na Cypriot viliwanukuu maafisa wakisema kwamba miili ya walimu wawili waliopoteza maisha ilipatikana siku ya Jumatano - na kwamba idadi ya waliofariki imeongezeka hadi watatu baada ya mwili wa mwanafunzi wa darasa la nane kupatikana.

    Idadi ya waliojeruhiwa imethibitishwa na waandishi wa BBC Uturuki.

    Juhudi za utafutaji na uokoaji zinaendelea kwenye tovuti, ambapo familia za wachezaji zimekusanyika.

    Maelezo zaidi:

  11. Kenya: Serikali yakanusha kuwatuma polisi kumkamata waziri wa zamani

    Kithure Kindiki

    Waziri wa mambo ya ndani nchini Kenya Kithure Kindiki amekanusha madai kwamba maafisa wa polisi walitumwa kumkamata waziri wa zamani wa mambo ya ndani Fred Matiang'i nyumbani kwake usiku wa Jumatano.

    Katika taarifa kwa vyombo vya habari Bw. Kindiki alisema madai hayo ni ya uwongo.

    "Tumepokea ripoti za vyombo vya habari kuhusu madai ya uvamizi wa makazi ya waziri waziri wa zamani wa mambo ya ndani Dr. Fred Matiang’i’ na watu wasiyojulikana jana usiku'.

    “Mawakili wa Dkt. Matiangi na baadhi ya wanasiasa waliozungumza kutoka eneo la tukio walidai kuwa watu hao walikuwa maafisa wa polisi waliotumwa kumkamata aliyekuwa Katibu wa Baraza la Mawaziri.

    "Madai haya ni ya uongo mtupu. Hakuna afisa wa polisi au ajenti yeyote wa usalama kutoka taasisi au idara yoyote ya Serikali aliyetumwa nyumbani kwa Dk. Matiang'i kumkamata, kumnyanyasa au kuingilia haki zake za Kikatiba kwa namna yoyote ile," Kindiki alisema.

  12. Aliyekua waziri wa mambo ya ndani Kenya Fred Matiang'i afika mahakamani kuzuia kukamatwa na polisi

    w

    Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Kenya Fred Matiang'i ameenda mahakamani kwa madai ya kuvamiwa na polisi usiku wa manane nyumbani kwake eneo la Karen.

    Mapema leo Alhamisi, mawakili wa Matiangi waliripoti kwamba polisi walijaribu kumkamata mteja wao kinyume cha sheria.

    Mawakili hao walidai kuwa baadhi ya maafisa wa polisi watiifu kwa Waziri huyo wa zamani walimdokezea kuhusu kukamatwa kwake na hivyo kusababisha atoe tahadhari.

    "...nimepokea taarifa za kuaminika kutoka kwa maafisa wa polisi wa Kenya kwamba wako chini ya maagizo ya moja kwa moja kumkamata kiholela kwa nia ya kufikishwa mahakamani kwa sababu za kisiasa".

    Kwa hivyo, Matiang'i aliiomba mahakama kutoa maagizo ya kuwazuia polisi kumkamata au kumfungulia mashtaka.

  13. Kagame amshutumu Tshisekedi kwa ‘kutoheshimu mikataba ya amani’

    w

    Rais wa Rwanda Paul Kagame amemshutumu mwenzake wa Congo Felix Tshisekedi kwa kutoheshimu makubaliano kadhaa ya kushughulikia mzozo wa DR Congo.

    Mvutano kati ya majirani wa eneo la Maziwa Makuu ya Afrika unaendelea kuongezeka huku DR Congo ikiishutumu Rwanda kwa kuvamia eneo lake "lililojificha kama waasi wa M23".

    Katika hotuba yake kwa mashirika ya kidiplomasia nchini Rwanda Jumatano usiku, Bw Kagame alimkosoa Bw Tshisekedi kwa kushindwa kushughulikia suala la ndani la Congo na kuilaumu Rwanda.

    Mamlaka ya Kinshasa haijajibu matamshi ya Bw Kagame.

    "Mtu huyu amevunjia heshima mikataba mingi aliyofanya na watu...ikiwa ni pamoja na hata mara ya mwisho mjini Bujumbura", Bw Kagame alisema. "Tunajadili mambo hadharani, alishiriki, tuliandika taarifa, kuwapa watu yale tuliyojadili na njia ya kusonga mbele.

    Taarifa hiyo inasomwa, lakini siku inayofuata taarifa iliyo kinyume inasomwa Kinshasa.” Aliongeza.

    Mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika mashariki mwishoni mwa juma lililopita mjini Bujumbura, Burundi, ulielekeza "kusitishwa mara moja", "kujiondoa kwa makundi yote ya kigeni" na haja ya "mazungumzo kati ya pande zote".

    Siku moja baadaye, msemaji wa serikali ya Congo alisema "wanatii" tu makubaliano ya Novemba huko Luanda kumaliza mzozo huu.

    Rais Kagame alisikitishwa na kwamba suala la waasi linaendelea "kurudi nyuma kwa takriban miongo mitatu" sasa licha ya Umoja wa Mataifa kuwa na "zaidi ya walinda amani elfu kumi" waliotumwa kushughulikia hilo.

    TH
  14. Thechikottukavu Ramachandran: Tembo 'muuaji' anayependwa na kuhofiwa sana

    Tembo

    Tembo mwenye utata 'muuaji' katika jimbo la kusini mwa India la Kerala amerejea kwenye vichwa habari baada ya kukodishwa kwa kiasi kikubwa cha fedha kilichoweka rekodi ili kushiriki katika tamasha la kila mwaka.

    Mwandishi wa BBC Kihindi Imran Qureshi anaeleza kwa nini mnyama huyo mwenye umri wa miaka 57 huamsha hisia na huruma.

    Thechikottukavu Ramachandran mara nyingi huitwa tembo mfungwa ambaye niu mrefu zaidi nchini India, madai ambayo ni vigumu kuthibitisha.

    Jambo lisilo na shaka ni kwamba yeye ni mrefu wa futi 10.53 (3.2m), anayethaminiwa, na kuvutia sana kuliko wenzake.

    Ramachandran, ambaye anamilikiwa na shirika la Thechikkottukavu katika wilaya ya Thrissur, ni mmoja kati ya mamia ya tembo waliofungwa huko Kerala ambao hukodishwa kwenye sherehe na programu zingine.

    Ana maelfu ya watu wanaompenda - ukurasa wa mashabiki kwenye Facebook ambao huchapisha picha na video mara kwa mara huwa na wafuasi 122,000 - na huvutia umati mkubwa wa watu kwenye hafla anazokuwepo.

    Lakini pia anajulikana kwa ubaya - wakosoaji wanasema anaonyesha mienendo ya vurugu na wanadai kuwa ameua watu wasiopungua 13 na tembo wenzake wawili katika miongo minne iliyopita.

    Tembo

    Maafisa wa Thechikkottukavu, hata hivyo, wanasema kuwa Ramachandran hakuwa sababu ya moja kwa moja ya vifo hivi, ambavyo vilitokea zaidi kutokana na mkanyagano uliozuka baada ya kuchukizwa kutokana na kelele kubwa na chokochoko zingine kwenye hafla zilizokuwa zikiendelea.

    Wanaharakati wa haki za wanyama wanasema kuwa Ramachandran, ambaye jicho lake la kushoto halioni, hapaswi kulazimishwa kushiriki katika hafla za umma.

    Wiki iliyopita, kamati 35 za hafla zilishiriki katika mnada wa kunadi uwepo wake kwenye sherehe zao - Sree Vishwanatha kutoka Thrissur ilishinda kwa kutoa rupia 675,000 sawa na dola $8,175), zabuni iliyoweka rekodi.

    "Watu zaidi huja kwenye hafla kama Ramachandran yupo. Ndio maana huwa anasakwa sana," anasema Bijoy PB, rais wa Thechikkottukavu trust, akiongeza kuwa shauku imeongezeka sana baada ya utulivu wa sherehe kutokana na janga kubwa la Covid.

  15. Kutopatikana kwa huduma Twitter je watumiaji wamevuka kikomo cha 'tweet' kwa siku?

    Tweet

    Baadhi ya watumiaji wa Twitter hawakuweza kutumia mtandao huo Jumatano baada ya mtandao huo kupata matatizo ya kiufundi.

    Wamiliki wa akaunti walipokea ujumbe unaosema: "Umevuka kikomo cha kila siku cha kutuma Twitter."

    Tajiri Elon Musk amepunguza wafanyakazi wa Twitter katika miezi michache iliyopita tangu alipounua Oktoba mwaka jana kwa $44bn (£36.5bn).

    Mwezi uliopita bosi wa Tesla na SpaceX alisema Twitter ilikuwa na wafanyakazi wapatao 2,300 - ambao ni pungufu zaidi kutoka karibu 8,000 alipochukua umiliki.

    Kwa miezi kadhaa wataalam wamekuwa wakionya kwamba upunguzaji mkubwa kama huo wa wafanyakazi unaweza kusababisha maswala ya kiufundi, ingawa bado haijabainika ikiwa kupunguzwa kwa idadi ya watu ndio chanzo cha kukatika kwa mtandao huo Jumatano.

  16. Kombe la Dunia la Klabu: Al Ahly ya Misri yapoteza kwa Real Madrid katika nusu fainali

    . Vinicius Jr aliifungia Real Madrid bao la kuongoza dhidi ya Al Ahly ya Misri katika mchezo wa nusu fainali mjini Rabat.
    Maelezo ya picha, Vinicius Jr aliifungia Real Madrid bao la kuongoza dhidi ya Al Ahly ya Misri katika mchezo wa nusu fainali mjini Rabat.

    Harakati za Afrika za kufuzu kwa fainali ya tatu ya Kombe la Dunia la Vilabu zilimalizika baada ya mabingwa wa Ulaya, Real Madrid kuwalaza Al Ahly ya Misri mabao 4-1 katika nusu fainali siku ya Jumatano.

    Safu ya ulinzi ya Al Ahly ilifanya vyema huku Vinicius Jr akitangulia kufunga dakika tatu kabla ya kipindi cha mapumziko huku Federico Valverde akifunga bao la kuongoza mara baada ya kipindi cha mapumziko.

    Mashetani Wekundu waliweka shinikizo kali katika goli la Real Madrid , na shinikizo hiyo ilizaa matunda pale Eduardo Camavinga alipomuangusha Hussein El Shahat ndani ya eneo la hatari.

    Ali Maaloul wa Tunisia alifunga penalti hiyo na kufanya matokeo kuwa 2-1 katika dakika ya 65.

    Al Ahly iliendeleza juhudi za kusawazisha na Mohamed Afsha alikosa bao la wazi pale alipopsalia na mlinda lango wa mabingwa hao wa Uhispania huku Hussein El Shahat na mchezaji wa akiba Percy Tau wote wakifanya usumbufu katika safu ya ulinzi ya Real Madrid.

    Naye Mohammed El Shenawy aliwanyima mabingwa hao mara 14 wa Uropa bao la tatu kwa kuokoa penalti ya Luka Modric katika dakika ya 87.

    Lakini Rodrygo na mchezaji wa akiba Sergio Arribas walihakikisha Real Madrid wanapata ushindi wa mechi hiyo dakika za lala salama baada ya kuipatia ushindi mnono timu yao.

    Al Ahly itacheza na Flamengo ya Brazil katika mchujo wa kuwania nafasi ya tatu, kabla ya Real Madrid kumenyana na Al Hilal ya Saudi Arabia katika fainali Jumamosi.

    Kocha wa Al Ahly, Marcel Koller alikasirishwa na kushindwa kwa timu yake, makosa waliofanya katika safu ya ulinzi na nafasi walizo kosa katika kipindi cha pili.

    Mchezaji mkongwe wa kimataifa wa Tunisia Ali Maaloul alizua matumaini ya kurejea Al Ahly kwa mkwaju wa penalti kipindi cha pili.
    Maelezo ya picha, Mchezaji mkongwe wa kimataifa wa Tunisia Ali Maaloul karibia aipatie matumaini Al Ahly kupitia mkwaju wa penalti kipindi cha pili.
  17. Rais Zelensky ataka ndege za kivita toka nchi za Magharibi ili 'kuwamaliza' Warusi

    Ukraine

    Kiongozi wa Ukraine amepeleka ombi lake la ndege za kivita kwa Ufaransa na Ujerumani baada ya kukutana na maafisa wa Uingereza.

    Rais Volodymyr Zelensky alikutana na viongozi wa nchi hizo mbili mjini Paris Jumatano jioni, ambapo waliahidi uungaji mkono unaoendelea kwa Ukraine.

    Emmanuel Macron wa Ufaransa na Olaf Scholz wa Ujerumani walirejea imani yao kwamba Urusi lazima ishindwe vita vinavyoendelea Ukraine.

    Bwana Zelensky atatoa maombi zaidi ya ndege atakapokutana na viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels leo siku ya Alhamisi.

    Anaamini kuwa ndege za kivita na makombora ya masafa marefu ni muhimu pamoja na vifaru vya Leopard 2 ambavyo mataifa ya Magharibi yamejitolea hivi karibuni kusaidia.

    Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa wanahabari Jumatano jioni na Bw Macron na Bw Scholz, Bw Zelensky alisema Ufaransa na Ujerumani zina uwezo wa "kubadilisha mchezo" katika vita dhidi ya Urusi kwa kuipatia Ukraine vifaru vya vita, ndege za kisasa za kivita na makombora ya masafa marefu.

    Alisema ugavi wa jeti hizo umejadiliwa, na akaonya kuwa kuna "muda mchache sana" wa kutoa silaha.

    Bw Macron alisema Ukraine inaweza kutegemea uungwaji mkono wa Ufaransa na kwamba nchi hiyo "imeazimia kuisaidia Ukraine kupata ushindi na kurejesha haki zake halali".

    Bw Scholz pia alisema: "Msimamo haujabadilika: Urusi lazima isishinde vita hivi." Ikiwa hiyo ina maana kwamba mataifa hayo mawili yanaweza kujitolea kusambaza ndege za kivita haiko wazi mpaka sasa.

    Rais wa Ufaransa na Kansela wa Ujerumani wamekuwa wakikosolewa kwa kuchelewa kuiunga mkono Ukraine hasa kwenye silaha wanazohitaji.

  18. Nyumba ya aliyekua waziri wa mambo ya ndani Kenya yazingirwa na maafisa, Polisi yakanusha hukusika

      • Author, Richard Kagoe
      • Nafasi, BBC News, Nairobi
    w

    Maafisa wameripotiwa kuvamia nyumba ya aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani wa Kenya Dr.Fred Matiang’i katika eneo la Karen jijini Nairobi. Awali iidaiwa kuwa polisi ndio wazingira nyumba hiyo, lakini mkuu wa polisi alikanusha kuhusika.

    Japhet Koome, mkuu wa polisi Kenya, alisema hakuna afisa wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi aliyetumwa kwa nyumba ya aliyekuwa waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang'i jana usiku'.

    Sababu ya operesheni hiyo haijulikani wazi.

    Wakili wa waziri huyo wa zamani Danstan Omari amethibitisha kuwa Dkt.Matiang'i amezuiliwa nyumbani kwake.

    Ameishutumu serikali kwa kujaribu kumtuhumu mteja wake kwa uwongo na kumtuhumu kwa madai ya uwongo.

    Kiongozi wa upinzani Raila Odinga na wanasiasa wengi wamefika nyumbani kwa waziri huyo wa zamani kwa mkesha wa usiku.

    Bw Odinga amekashifu kitendo hicho akitaja kuwa ni unyanyasaji na vitisho kutoka kwa serikali. Kundi la mawakili litaandamana na waziri huyo wa zamani hadi kituo cha polisi kilicho karibu zaidi siku ya Alhamisi asubuhi ili kurekodi taarifa.

    Dkt Matiang’i alikuwa waziri mwenye ushawishi katika baraza la mawaziri na mshirika mkuu wa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye aliandaa kampeni kubwa ya kumzuia Rais William Ruto asiingie mamlakani.

    Wafanyakazi wa usalama wanaohusishwa na watu mashuhuri akiwemo Dkt.Matiang’i ambaye alihudumu chini ya aliyekuwa Rais Kenyatta walipunguzwa kazi mapema Februari.

    Kenyatta na Ruto walitofautiana katika muhula wao wa pili madarakani kufuatia mapatano ya kisiasa kati ya rais huyo wa zamani na mpinzani wake mkuu Raila Odinga yaliyoashiria ‘kupeana mkono’ mwaka wa 2018.

  19. Tetemeko la ardhi Uturuki: Juhudi za uokoaji zinaendelea huku idadi ya waliokufa ikiwa ni zaidi ya 12,000

    w

    Idadi ya vifo kutoka nchi zote mbili ilitarajiwa kuongezeka kwani mamia ya majengo yaliyoporomoka katika miji mingi yamekuwa makaburi ya watu waliokuwa wamelala wakati tetemeko hilo lilipotokea.

    Katika mji wa Uturuki wa Antakya, makumi ya maiti, baadhi zikiwa zimefunikwa kwa blanketi na shuka na nyingine zikiwa kwenye mifuko ya miili, zilipangwa chini nje ya hospitali.

    Melek, 64, aliomboleza ukosefu wa timu za uokoaji. "Tulinusurika na tetemeko la ardhi, lakini tutakufa hapa kutokana na njaa au baridi."

    Wengi katika eneo la maafa walikuwa wamelala ndani ya magari yao au mitaani chini ya blanketi kwenye baridi kali, wakihofia kurejea kwenye majengo yaliyotikiswa na tetemeko hilo la kipimo cha 7.8 - ambalo lilikuwa baya zaidi nchini Uturuki tangu 1999 - na kwa tetemeko kubwa la pili saa chache baadaye.

    Idadi ya vifo iliyothibitishwa iliongezeka hadi 9,057 nchini Uturuki siku ya Jumatano, na nchini Syria ilipanda hadi angalau 2,950, kulingana na serikali na huduma ya uokoaji inayofanya kazi katika eneo linaloshikiliwa na waasi kaskazini magharibi.

    Maafisa wa Uturuki wanasema kuwa takriban watu milioni 13.5 waliathirika katika eneo linalochukua takriban kilomita 450 kutoka Adana magharibi hadi Diyarbakir mashariki. Nchini Syria, watu waliuawa hadi kusini kama Hama, kilomita 250 kutoka kitovu cha tetemeko.

    Baadhi ya waliofariki Uturuki walikuwa wakimbizi kutoka vita vya Syria. Mifuko ya miili yao ilifika mpakani kwa teksi, magari ya kubebea mizigo na kurundikana juu ya malori ya gorofa ili kupelekwa sehemu za mwisho za kupumzika katika nchi yao.

    Zaidi ya watu 298,000 wamekosa makazi na makazi 180 ya waliokimbia makazi yao yamefunguliwa, vyombo vya habari vya serikali ya Syria viliripoti, vikirejea maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa serikali, na ambayo hayashikiliwi na mirengo ya upinzani.

    Nchini Syria, juhudi za kutoa misaada zinatatizwa na mzozo ambao umegawanya taifa hilo na kuharibu miundombinu yake.

    Uwasilishaji wa msaada wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kupitia Uturuki kwa mamilioni ya watu kaskazini-magharibi mwa Syria unaweza kuanza tena Alhamisi baada ya operesheni ya muda mrefu kusitishwa na tetemeko hilo, maafisa wa Umoja wa Mataifa walisema

    .Katika mji wa Aleppo nchini Syria, wafanyakazi katika hospitali ya Al-Razi walimhudumia mtu aliyejeruhiwa ambaye alisema zaidi ya jamaa kumi na wawili akiwemo mama yake na babake waliuawa wakati jengo walilokuwamo lilipoporomoka.