COP31: Washindwa kuafikiana kuhusu matumizi ya mafuta, gesi na makaa ya mawe
Mazungumzo ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, COP31, yamekwama baada ya Umoja wa Ulaya (EU) na wawakilishi wengine kukataa rasimu ya makubaliano iliyowasilishwa katika mkutano huo unaofanyika Antalya, Uturuki.
Mwakilishi wa EU, Darragh O’Brien, amesema maamuzi yaliyopendekezwa hayafikii kiwango cha hatua zinazohitajika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Pia amezishutumu baadhi ya nchi zinazozalisha mafuta kwa kile alichokiita kuteka nyara mazungumzo hayo.
Rasimu ya nne ya makubaliano iliwasilishwa leo, lakini haikutaja matumizi ya nishati za mafuta, gesi na makaa ya mawe. Hilo limekuwa moja ya matakwa muhimu ya EU katika mazungumzo hayo.
Rais wa COP31, Murat Kurum, amesema wajumbe hawajaafikiana kuhusu rasimu hiyo ya nne na kwamba hakutakuwa na rasimu nyingine mpya.
Kutokana na mvutano huo, mkutano wa COP31 sasa umeingia katika historia kama mkutano wa muda mrefu zaidi wa COP, huku wajumbe wakiendelea kujaribu kufikia makubaliano ya pamoja kuhusu hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.