Dhehebu la kufunga hadi kufa: Polisi Kenya yachunguza kutoweka kwa watoto sita
Polisi nchini Kenya wanachunguza kutoweka kwa watoto sita katika kile kinachoweza kuwa uhusiano na ibada ya njaa katikakijiji cha Shakahola ambayo inadaiwa kusababisha vifo vya zaidi ya watu 400 miaka miwili iliyopita.
Muhtasari
- Dhehebu la kufunga hadi kufa: Polisi Kenya wanachunguza kutoweka kwa watoto sita
- Hakuna manusura katika ajali ya ndege iliyowabeba watu 48 mashariki mwa Urusi
- Mamlaka ya uangalizi ya polisi nchini Kenya yasema polisi walitumia nguvu kupita kiasi katika maandamano
- Aliyekuwa mkuu wa shirikisho la soka Afrika ya Kati afungwa jela kwa uhalifu wa kivita
- Watu 12 wameokolewa kwenye mgodi ulioporomoka Mashariki mwa DRC
- Mwanaume wa India akamatwa kwa kubuni balozi bandia
- Msaidizi aliyemshutumu Kanye West kwa unyanyasaji wa kijinsia 'mafichoni', wakili anasema
- Waandishi wa habari Gaza wako katika hatari ya kukumbwa na njaa - taarifa ya pamoja
- Mabaki yapatikana baada ya ndege iliyobeba watu 48 kuanguka Urusi
- Mwanamke aliyepatikana na hatia ya kumng'ata mwanaume ulimi aombwa msamaha
- Wanawake wa Australia washinda haki ya kuishtaki Qatar Airways kwa kuvuliwa nguo wakichunguzwa
- Wanajeshi wa Thailand na Cambodia wafyatuliana risasi mpakani
- Timu ya IAEA itazuru Iran lakini haitafika katika vituo vya nyuklia
Moja kwa moja
Na Asha Juma
Habari za hivi punde, Mchezaji maarufu wa mieleka Hulk Hogan afariki

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Hulk Hogan katika Kongamano la Kitaifa la Republican huko Wisconsin mwaka jana Hulk Hogan, Mchezaji wa mieleka mahiri na mwenye kelele ambaye aliwafanya watu wengi kupenda mchezo wa mieleka katika miaka ya 1980, huku akiwa mmoja wa watu mashuhuri wanaotambulika katika kizazi chake, amefariki Alhamisi, akiwa na umri wa miaka 71.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kifo cha Hogan kilithibitishwa na promota Eric Bischoff, mshirika wake katika ligi ya mieleka ya Real America Freestyle iliyozinduliwa hivi majuzi . TMZ iliripoti kwamba wahudumu wa matibabu walitumwa nyumbani kwake huko Clearwater, Florida, baada ya simu ya dharura kupigwa kwa ajili ya matibabu ya "mshtuko wa moyo."
"The Hulkster" aliongoza WrestleMania mara nane, huku pambano lake la kukumbukwa zaidi katika tukio la WWE (shindano la mieleka) likifanyika mwaka 1987 dhidi ya Andre the Giant mwenye uzani wa pauni 520.
Dhehebu la kufunga hadi kufa: Polisi Kenya wanachunguza kutoweka kwa watoto sita

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Watu zaidi ya 400 waliripotiwa kufa Shakahola miaka miwili iliyopita Polisi nchini Kenya wanachunguza kutoweka kwa watoto sita katika kile kinachoweza kuwa uhusiano na ibada ya njaa ambayo inadaiwa kusababisha vifo vya zaidi ya watu 400 miaka miwili iliyopita.
Kamishna wa kusini mashariki mwa Kaunti ya Kilifi, Josphat Biwott, ameiambia BBC kwamba polisi waliwapata wazazi wa watoto hao katika nyumba karibu na Msitu wa Shakahola, ambao ulipata umaarufu duniani kote kama eneo la vifo vya watu wengi.
Alisema wazazi hao, waliotajwa katika vyombo vya habari vya Kenya kama Jairus na Lilian Otieno, pamoja na watu wengine wawili akiwemo msichana kijana, walikuwa katika hali dhaifu walipowekwa chini ya ulinzi na hawakusema chochote kuhusu watoto wao walipo.
Waligunduliwa baada ya polisi kuvamia nyumba hiyo Jumamosi ya "familia inayoshukiwa kuwa na msimamo mkali wa kidini," kulingana na ripoti ya polisi ambayo BBC iliipata.
Polisi pia walipata mafuvu mawili ya binadamu na mwili wa mtu asiyejulikana, anayeaminika kufa hivi karibuni.
Bw Biwott alisema bado hakuna ushahidi thabiti wa uhusiano na ibada ya Shakahola, lakini suala hilo lilikuwa linachunguzwa na polisi walikuwa wameomba ruhusa ya kufukua makaburi yanayoshukiwa katika mali hiyo.
Televisheni ya Citizen ya Kenya iliripoti kuwa familia hiyo ilitoroka kutoka Shakahola mnamo 2023, lakini Bw Otieno aliamua kurejea eneo hilo mwezi Machi na mkewe na watoto.
Jamaa wa karibu alikiambia kituo cha televisheni kwamba Bw Otieno alikuwa amemthibitishia watoto hao walikuwa wamekufa.
Mathia Shipeta, kutoka shirika la haki za binadamu la Haki Africa, aliiambia BBC shirika lake linaamini kuwa watu wengine wapatao 47 wanaweza kuwa wamepotea na wangeweza kufa kutokana na njaa.
Josphat Biwott, kamishna wa kaunti, alisema polisi wanaweza tu kuthibitisha katika hatua hii watoto sita waliopotea. Maafisa walikamata watu saba na uchunguzi unaendelea.
Kesi hiyo inakuja huku kukiwa na kesi ya watu 95 wanaodaiwa kuhusishwa na kile kinachoitwa mauaji ya Shakahola, akiwemo kiongozi wa ibada, aliyejitangaza mchungaji Paul Mackenzie.
Bw Mackenzie alikamatwa Aprili 2023 na kushtakiwa kwa mauaji bila kukusudia kwa vifo vya wafuasi wake 429.
Inadaiwa aliwaambia waumini wa kanisa lake wangefika mbinguni haraka zaidi ikiwa wataacha kula.
Bw Mackenzie anakanusha makosa na amekana hatia.
Unaweza pia kusoma:
Hakuna manusura katika ajali ya ndege iliyowabeba watu 48 mashariki mwa Urusi

Chanzo cha picha, Russian transport prosecutor
Maelezo ya picha, Ndege hiyo ilianguka katika eneo la kijijini lenye miti 16km kutoka uwanja wa ndege wa Tynda Maafisa wa Urusi wanasema watu 48 wamefariki wakati ndege ya shirika la ndege la Angara ilipoanguka katika msitu mkubwa katika eneo la mashariki la Amur.
Ndege ya Antonov An-24, iliyokuwa na abiria 42 na wafanyakazi sita, ilikuwa imeondoka Blagoveshchensk karibu na mpaka wa China na kutoweka kwenye skrini za rada ilipokuwa ikikaribia uwanja wa ndege wa Tynda, maafisa walisema.
Helikopta ya anga ya Urusi kisha ikaona moshi unaofuka kutoka kwa ndege kwenye mlima wa mbali takriban kilomita 16 kutoka Tynda.
Gavana wa eneo la Amur Vasily Orlov alisema watoto watano walikuwa miongoni mwa waliokuwemo na kutangaza siku tatu za maombolezo.
Ndege hiyo aina ya An-24 ilikuwa katika hatua ya mwisho ya safari kutoka Khabarovsk kusini-mashariki mwa Urusi.
Mamlaka ya uangalizi ya polisi nchini Kenya yasema polisi walitumia nguvu kupita kiasi katika maandamano

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka huru ya uangalizi wa shughuli za polisi nchini Kenya (IPOA), inasema maafisa wa polisi walikiuka viwango vya polisi vya katiba wakati wa maandamano manne tofauti yaliyofanyika kote Kenya mwezi Juni na Julai.
Katika ripoti mpya, shirika la uangalizi linasema liliorodhesha vifo sitini na vitano na zaidi ya raia mia tatu walijeruhiwa wakati waandamanaji walipopambana na polisi.
Makundi ya kutetea haki za binadamu yamelaani majibu ya serikali, yakishutumu mamlaka kwa kuruhusu na wakati mwingine kuhimiza matumizi ya nguvu mbaya dhidi ya waandamanaji.
Hasira ya umma imekuwa ikiongezeka, hasa baada ya video kuibuka mwezi uliopita ikionyesha afisa wa polisi akimpiga risasi mchuuzi wa barabarani usoni wakati wa maandamano.
Mwanamume huyo baadaye alikufa hospitalini na afisa huyo ameshtakiwa.
Unaweza pia kusoma:
Aliyekuwa mkuu wa shirikisho la soka Afrika ya Kati afungwa jela kwa uhalifu wa kivita

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Edouard Ngaïssona alichaguliwa katika kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka la Afrika mnamo Februari 2018. Mkuu wa zamani wa shirikisho la soka la Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Patrice-Edouard Ngaïssona, amepatikana na hatia ya kutenda uhalifu wa kivita 28 na uhalifu dhidi ya ubinadamu na majaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Alishtakiwa, pamoja na Alfred Yekatom, kwa kuratibu mashambulizi dhidi ya idadi ya Waislamu nchini humo mwaka 2013-14.
Yekatom alipatikana na hatia ya mashtaka 20. Majaji hao walitoa uamuzi wao baada ya kesi iliyodumu kwa takriban miaka minne iliyohusisha mashahidi zaidi ya 170 na karibu vipengele 20,000 vya ushahidi.
Ngaïssona alihukumiwa miaka 12 na Yekatom miaka 15.
Ghasia zimeikumba CAR kwa muda mrefu wa muongo mmoja uliopita, lakini makubaliano ya hivi majuzi ya amani yalisababisha kuvunjika kwa makundi mawili ya waasi mwezi huu.
CAR ilitumbukia katika machafuko mwaka wa 2013 wakati waasi wengi wa Kiislamu kutoka kundi la Séleka waliponyakua mamlaka katika nchi hiyo yenye Wakristo wengi.
Kundi la wanamgambo wengi wa Kikristo, wanaoitwa anti-Balaka, walisimama kukabiliana na Séleka baada ya Rais wa wakati huo François Bozizé kuondolewa madarakani.
Ngaïssona na Yekatom walitiwa hatiani kwa makosa mengi ya uhalifu, yakiwemo mauaji, mateso na kutesa kundi la kidini.
Mwendesha mashtaka aliweka madai ya mfumo wa amri, akisema Ngaïssona alitoa pesa na maagizo kwa vikundi vya anti-Balaka mnamo 2013 na 2014.
Watu 12 wameokolewa kwenye mgodi ulioporomoka Mashariki mwa DRC

Maelezo ya picha, Gavana wa Kivu Kusini Patrick Busu wa Ngwi Nshombo Gavana wa Kivu Kusini Patrick Busu wa Ngwi Nshombo anasema watu 12 wameokolewa hadi sasa kutoka kwa mgodi ulioanguka huko Lomera, Mashariki mwa DRC mwishoni mwa wiki.
Operesheni za uokoaji bado zinaendelea, lakini idadi ya majeruhi bado haijulikani.
"Bado tunajaribu kubaini ni wangapi wamepotea," gavana alisema wakati wa ziara kwenye eneo hilo Jumatano.
Tukio hilo lilitokea katika mgodi wa dhahabu wa Lomera ambapo mamlaka sasa inasema makadirio ya wachimbaji 4,786 wanafanya kazi katika hali mbaya na hatari.

Kulingana na gavana huyo, machine ya kuchima mgodi ililipua moaj ya mashimo ya mgodi Jumamosi usiku, na kusababisha mashimo mengine 18 kuanguka, na kuwazika wachimbaji wengi chini ya ardhi.
Tangu wakati huo ameamuru njia zoteza kuingia kwenye migodi zilizoathiriwa kufungwa, uamuzi uliofanywa kwa kushauriana na uongozi wa vuguvugu tawala la M23/AFC ambalo linadhibiti eneo hilo.
"Tumefunga mahandaki yote vilivyohusika katika kuanguka ili kuzuia upotezaji zaidi wa maisha," Nshombo alisema. "Shughuli za uchimbaji madini zitaanza tena mara tu hali ya usalama itakapohakikishwa."
Mwanaume wa India akamatwa kwa kubuni balozi bandia

Chanzo cha picha, ANI
Kitengo cha Noida cha Polisi Maalum wa Uttar Pradesh nchini India kilimkamata mwanamume mmoja huko Ghaziabad mnamo Jumanne, Julai 22, kwa madai ya kuunda ubalozi bandia.
Mshukiwa huyo anasemekana kuwa alikuwa akiwasiliana na watu kwa madai kuwa ni balozi wa nchi zinazoitwa Westarctica, Saborga, Paulvia, na Lodonia.
Sushil Ghule, mmoja wa kikosi kilichomkamata mtu huyo alisema: "Alikuwa akiwasiliana na watu wanaodai kuwa balozi wa West Arctica, Saborga, Paulvia, Lodonia na 'nchi' nyingine zinazofanana na hizo. Nyenzo nyingi za kutiliwa shaka zilipatikana kwake. Magari yaliyopatikana kwa jina lake yalikuwa na nambari za kidiplomasia, ambazo hazikuwa na uhalali wa kisheria kutoka kwa mashirika ya serikali."
Polisi walisema kuwa mwanamume huyo, Harshvardhan Jain, alikuwa akiishi katika nyumba ya kukodi katika eneo la Kavi Nagar huko Ghaziabad, ambapo alikuwa akifanya kazi kwa siri katika ubalozi huo bandia.
Msaidizi aliyemshutumu Kanye West kwa unyanyasaji wa kijinsia 'mafichoni', wakili anasema

Chanzo cha picha, Getty Images
Msaidizi wa zamani wa Kanye West ana hofu na bado yuko mafichoni baada ya kuwasilisha madai ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya rapa huyo wa Marekani, wakili wake ameiambia BBC.
Lauren Pisciotta, 36, ambaye alianza kufanya kazi na West mnamo 2021, alifungua kesi ya kwanza dhidi yake mnamo Juni 2024 akidai kuwa alinyanyaswa kijinsia na kufuatilia maisha yake kwa lazima.
Katika madai yaliyowasilishwa alimshutumu West, ambaye pia anajulikana kama Ye, kwa biashara ya ngono, kuvizia, kushambulia na kubaka.
West anakanusha madai yake , ambayo anaiita "hadithi ya kubuni".
Kesi hiyo ya madai inatazamiwa kurejea mahakamani nchini Marekani mwezi ujao, lakini wakili wa Bi Pisciotta anasema mteja wake kwa sasa yuko mafichoni na "anaogopa".
Akiongea na BBC, Arick Fudali alisema kuwa Bi Pisciotta sasa amefuta sehemu kubwa ya uwepo wake kwenye mtandao na sasa "anakaa tu na kujificha - akiacha kesi hii isikike".
Aliongeza: "Inasikitisha sana - amepitia mengi. Anateseka na amekuwa akiteseka tangu aanze kufanya kazi kwa Mr West."
Bi Pisciotta alianza kufanya kazi na West mwaka wa 2021 na alifungua kesi yake ya kwanza dhidi ya rapa huyo mnamo 3 Juni 2024 akidai unyanyasaji wa kijinsia, uvunjaji wa mkataba na kusitisha isivyofaa.
Unaweza pia kusoma:
Waandishi wa habari Gaza wako katika hatari ya kukumbwa na njaa - taarifa ya pamoja

Chanzo cha picha, Getty Images
BBC News imetoa taarifa ya pamoja hivi punde na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters inayotoa wito kwa Israel "kuruhusu waandishi wa habari kuingia na kutoka Gaza".
Hii hapa taarifa kamili:
"Tuna wasiwasi mkubwa na waandishi wetu wa habari huko Gaza, ambao wanazidi kushindwa kupata chakula na familia zao. Kwa miezi mingi, waandishi hawa wa kujitegemea wamekuwa jicho la ulimwengu huko Gaza. Sasa wanakabiliwa na hali mbaya sawa na wale wanaoandika taarifa kuwahusu.
"Waandishi wa habari wanavumilia matatizo mengi katika maeneo ya vita. Tunasikitika sana kwamba tishio la njaa sasa ni mojawapo.
"Tunaziomba tena mamlaka za Israel kuruhusu waandishi wa habari kuingia na kutoka Gaza. Ni muhimu kwamba chakula cha kutosha kifikie watu wa huko."
Soma zaidi:
Mabaki yapatikana baada ya ndege iliyobeba watu 48 kuanguka Urusi

Chanzo cha picha, Rodion Kuznetsov
Huduma za uokoaji za Urusi zimepata mabaki ya ndege iliyotoweka takriban kilomita 16 kutoka eneo ilikokuwa ikienda mashariki mwa Amur.
Ndege ya shirika la ndege la Angara An-24, iliyokuwa na abiria 43 na wafanyakazi sita, ilikuwa imeondoka Blagoveshchensk karibu na mpaka wa China na kutoweka kwenye rada ilipokuwa ikikaribia uwanja wa ndege wa Tynda, maafisa wa dharura walisema.
Gavana wa eneo la Amur Vasily Orlov alisema "rasilimali zote muhimu" zimetumwa kutafuta ndege hiyo. Watoto watano walikuwa miongoni mwa waliokuwemo, aliongeza.
Muda mfupi baadaye wizara ya dharura ya Urusi ilisema helikopta ya anga ya Urusi iliona kipande cha ndege hiyo kilichokuwa kikiwaka moto.
Hakuna anayedhaniwa kuwa amenusurika, ripoti zinasema.
Kituo cha ulinzi wa raia cha Amur kilisema kuwa ndege hiyo ilipatikana kwenye mlima takriban kilomita 16 kutoka Tynda, shirika la habari la Tass liliripoti.

Chanzo cha picha, Emercom
Picha kutoka eneo la tukio zilionyesha mabaki ya ndege hiyo ikiwaka katika misitu minene.
Uchunguzi wa awali uliaangalia ama hitilafu za rubani katika hali mbaya ya hewa au hitilafu ya kiufundi, kulingana na maafisa wa dharura.
Ndege hiyo aina ya An-24 ilikuwa katika hatua ya mwisho ya safari kutoka Khabarovsk kusini-mashariki mwa Urusi.
Ndege aina ya An-24RV iliacha njia ilipotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Nizhneangarsk Julai 2019. Wahudumu wawili wa ndege hiyo waliuawa.
Mnamo 2011, Angara An-24 nyingine ilianguka kwenye mto Ob huko Siberia, na kuua abiria saba.
Soma zaidi:
Mwanamke aliyepatikana na hatia ya kumng'ata mwanaume ulimi aombwa msamaha

Chanzo cha picha, EPA
Waendesha mashtaka nchini Korea Kusini wameomba msamaha kwa mwanamke aliyepatikana na hatia kwa kujitetea wakati wa shambulio la ukatili wa kingono zaidi ya miaka 60 iliyopita.
Choi Mal-ja alihukumiwa kifungo cha miezi 10 jela na hukumu nyingine ya miaka miwili iliyocheleweshwa, kwa kumng'ata sehemu ya ulimi mshambuliaji wake alipodaiwa kujaribu kumbaka mwaka 1964, alipokuwa na umri wa miaka 18.
Akihamasishwa na vuguvugu la #MeToo nchini humo, Bi Choi, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 78, amefanya kampeni kwa miaka mingi kutaka hukumu yake ibatilishwe.
Kesi yake ilianza kusikilizwa tena katika jiji la Busan siku ya Jumatano, ambapo waendesha mashtaka waliomba radhi na kuomba mahakama ifutilie mbali hukumu yake ya hatia.
"Kwa miaka 61, serikali ilinifanya niishi kama mhalifu," Bi Choi aliambia wanahabari nje ya mahakama kabla ya kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Alisema anatumai vizazi vijavyo vinaweza kuishi maisha ya furaha bila unyanyasaji wa kijinsia.
Mwanzoni mwa kesi hiyo, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Busan Jeong Myeong-won alisema "tunaomba radhi".
"Tumesababisha kwa Choi Mal-ja, mwathirika wa uhalifu wa ngono ambaye alipaswa kulindwa, maumivu na uchungu usioelezeka."
Uamuzi wa mwisho umepangwa kufanyika Septemba 10, huku waangalizi wa kisheria wakitarajia mahakama kubatilisha hukumu ya Bi Choi.
Pia unaweza kusoma:
Wanawake wa Australia washinda haki ya kuishtaki Qatar Airways kwa kuvuliwa nguo wakichunguzwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanawake watano wa Australia ambao walivuliwa nguo na kuchunguzwa katika uwanja wa ndege wa Doha wameshinda haki ya kushtaki Qatar Airways baada ya kukata rufaa.
Wanawake hao waliamuriwa kushuka kwenye ndege na kukaguliwa iwapo walikuwa wamejifungua baada ya mtoto kupatikana akiwa ametelekezwa kwenye pipa la uwanja wa ndege mnamo mwaka 2020 - tukio ambalo lilizua ghadhabu duniani.
Jaji wa Australia mwaka jana aligundua shirika la ndege linalomilikiwa na serikali halingeweza kufunguliwa mashitaka chini ya sheria zinazosimamia usafiri wa kimataifa, na akasema tukio ambapo wafanyakazi wake waliingilia kati kiasi hicho lilikuwa "lisilo fikirika, lisilo na maana, fedheha, tukio lisiloweza kuamini kama linaweza kutokea, [na] uchungu".
Wanawake hao walikata rufaa, huku majaji wa mahakama wakisema kuwa hakimu mkuu alikosea kutupilia mbali kesi hiyo.
Wanawake hao watano walifungua kesi mwaka 2021, dhidi ya Qatar Airways, Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Qatar na waendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamad, kampuni inayoitwa Matar.
Walitaka kulipwa fidia kutokana na madai ya "kugusana kinyume cha sheria" na kifungo cha uwongo ambacho kilisababisha athari za afya ya akili ikiwa ni pamoja na msongo wa mawazo na kiwewe. Abiria wengine ambao walichunguzwa - ni pamoja na kutoka Uingereza na New Zealand – ambao hawakuwa sehemu ya kesi hiyo.
Soma zaidi:
Wanajeshi wa Thailand na Cambodia wafyatuliana risasi mpakani

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanajeshi wa Cambodia na Thailand wanafyatuliana risasi tangu asubuhi katika eneo la mpakani linalozozaniwa.
Pande zote mbili zimeshtumiana kwa kufyatua risasi ya kwanza.
Hii inafuatia uamuzi wa Thailand kumfukuza balozi wa Cambodia na kumwita balozi wake kutoka Phnom Penh baada ya kutokea kwa mlipuko wa bomu la ardhini uliomjeruhi mwanajeshi wa Thailand kando ya mpaka.
Kwa mujibu wa jeshi la Thailand, wanajeshi wao walifyatua risasi baada ya kukabiliana na kundi la wanajeshi wa Cambodia waliokuwa na silaha kwenye mpaka unaozozaniwa huku Wacambodia wakisema ni Wathailand ambao walifyatua silaha zao kwanza.
Sasa, wanakijiji katika eneo la mpakani mwa Thailand wameagizwa kuhama.
Hadi kufikia sasa, hakuna nchi inayoonekana kuwa tayari kurudi nyuma.
Lakini mzozo huu ulianza mwezi uliopita, baada ya mzee wa Cambodia, Hun Sen, kumwaibisha Waziri Mkuu wa Thailand Paetongtarn Shinawatra kwa kuvujisha mazungumzo ya simu kati yao kuhusu mpaka unaozozaniwa.
Hakuna anayejua kwa nini aliamua kufanya hivi.
Paetongtarn Shinawatra alisimamishwa kazi kama waziri mkuu na mahakama ya kikatiba nchini Thailand na serikali yake isiyopendwa na watu wengi haiwezi kumudu kuonyesha udhaifu wowote sasa katika kukabiliana na Cambodia.
Matokeo yake yamekuwa ni kuongezeka kwa vita vya maneno kati ya nchi hizo mbili, kusambaratika kwa biashara ya mpakani ambayo ina thamani ya mabilioni ya dola, na kuongezeka kwa hatari ya mapigano makubwa zaidi kati ya majeshi yao mawili.

Chanzo cha picha, Royal Thai Army/Facebook
Ubalozi wa Thailand watoa wito kwa raia kuondoka Cambodia
Wakati huo huo, ubalozi wa Thailand mjini Phnom Penh unawataka raia wa Thailand kuondoka nchini Cambodia kutokana na mapigano ya mpakani.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa Facebook, ubalozi ulisema kwamba raia wa Thailand walioko Cambodia wanapaswa kuondoka "mara moja" labda wawe na sababu za dharura za kuendelea kuwa huko.
Pia unaweza kusoma:
Timu ya IAEA itazuru Iran lakini haitafika katika vituo vya nyuklia

Chanzo cha picha, Askin Kiyagan/Anadolu Agency/Getty Images
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Kazem Gharibabadi, amesema kuwa, ujumbe wa masuala ya kiufundi kutoka Shirika la Nishati ya Atomiki (IAEA) hivi karibuni watazuru Tehran, lakini hawataruhusiwa kutembelea vituo vya nyuklia vya Iran.
Bw. Gharibabadi, ambaye yuko New York, alisema kuwa Iran imekubali ziara ya timu ya kiufundi ya IAEA mjini Tehran katika muda wa wiki mbili hadi tatu zijazo.
Shirika la habari la Reuters limenukuu Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki likisema kwamba Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Rafael Grossi, "anafanya mazungumzo kikamilifu na pande zote zinazohusika na suala la nyuklia ya Iran."
Inaonekana kuwa ziara hii imepangwa kwa muda kabla ya mkutano wa robo mwaka wa Baraza la Magavana, ambao umepangwa kushughulikia suala la nyuklia ya Iran tena mnamo mwezi Septemba.
Bwana Gharibabadi alisisitiza kuendelea kwa mpango wa nyuklia wa Iran na kuonya juu ya uchochezi unaofanywa na serikali za Ulaya na kuwa kurejeshwa kwa vikwazo na Baraza la Usalama dhidi ya Iran kutakabiliwa vikali nan chi hiyo.
Serikali tatu za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimeipa Iran hadi mwisho wa mwezi wa Agosti, takriban wiki tano kutoka sasa, kuingia katika makubaliano mapya ya nyuklia, au nchi hizi zitaanzisha tena vikwazo vya Baraza la Usalama.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi hapo siku za nyuma, aliwahi kusema kwamba maombi ya shirika la IAEA yatapitiwa upya hatua kwa hatua na Baraza Kuu la Usalama la Taifa.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo ya leo.
