Rais mpya wa Nigeria asafiri hadi Paris na London 'kupumzika'

Safari za mara kwa mara za rais mteule ng'ambo zinaendelea kuzua uvumi kuhusu afya yake.

Moja kwa moja

  1. na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo, tukutane tena hapo kesho majaaliwa.

  2. Meta yazuiwa kuwafuta kazi wasimamizi wa maudhui wa Facebook nchini Kenya

    j
    Maelezo ya picha, Facebook imepewa siku saba kujibu hoja ya kisheria ya mahakama

    Mahakama katika mji mkuu wa Kenya Nairobi, imeizuia kampuni ya Meta, ambayo ni kampuni mama ya facebook, kuwafuta kazi wasimamizi wake wa maudhui huku wakisubiri kusikilizwa kwa kesi ya kupinga hatua ya kufutwa kwao kazi.

    Mahakama ya kazi pia imeizuia Meta na kampuni yake yaajira, Sama, kuwaajiri wasimamizi wengine wa kuchukua nafasi ya wale waliofutwa kazi.

    Shitaka hilo liliwasilishwa na wasimamizi wa maudhui ya Facebook 43 nchini Kenya , waliokuwa wameajiriwa na Sama kwa niaba ya Meta. Wanadai kwamba shughuli ya kuwasimamisha kazi inayofanyika ni kinyume cha sheria.

    Wazimamizi waliiambia mahakama kwamba wamepewamaelezo ‘’tofauti na ya ‘’kukanganya "ya kuwataka waache kazi, limeripoti gazeti la Daily Nation.

    Takriban wasimamizi 260 wa maudhui walitarajiwa kufutwa kazi, kulingana na vyombo vya habari nchini Kenya.

    Meta na Sama wamepewa siku saba wawe wametoa jibu kuhusu ombi hilo

    Kesi hiyo itasikilizwa tarehe 28 Machi.

  3. Israel yapitisha sheria mpya kumlinda Waziri Mkuu kutong'olewa madarakani

    israel

    Bunge la Israel limepitisha sheria mpya itakayozuia waziri mkuu kutangazwa kuwa hafai kushika wadhifa huo na mwanasheria mkuu. Inachukuliwa kuwa uamuzi huo ni kwa maslahi ya kiongozi aliyeko madarakani, Benjamin Netanyahu, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi.

    Sheria hiyo ni sehemu ya mpango tata wa serikali yake ya mrengo wa kulia kuweka mipaka ya mamlaka ya mahakama, jambo ambalo limesababisha maandamano ya miezi kadhaa.

    Maelfu ya waandamanaji walikusanyika katikati mwa Tel Aviv na kufunga barabara kuu kadhaa. Bendera kubwa ya Israeli na bendera yenye tangazo la uhuru pia iliwekwa juu ya ukuta katika Jiji la Kale la Jerusalem.

    Israel

    Mkutano wa hadhara unapangwa jioni katika kitongoji cha Orthodox Tel Aviv cha Bnei Brak, ambapo kuna msaada mkubwa kwa serikali.

    Kabla ya tukio hilo, waandamanaji waliweka viti na meza, zikiwa zimezungukwa na bendera za Israel, na kuwaalika wanajamii kukutana nao kwa mazungumzo ya maridhiano kuhusu mabadiliko ya sheria yaliyopangwa. Kulikuwa na mazungumzo makali.

    Picha ziliibuka kwenye mitandao ya kijamii za mmoja wa viongozi wa maandamano hayo ambaye ni daktari akiwa amelala chini akiwa na damu baada ya kugongwa na gari. Lakini waandaaji baadaye walisema kuwa ilikuwa ajali, sio kitendo cha makusudi.

    Sheria mpya ambayo ilipitisha kwa kura 61 kwa 47 katika bunge lenye viti 120 kufuatia mjadala mkali wa usiku kucha, inafanya kuwa vigumu zaidi kumuondoa waziri mkuu aliyepo madarakani kinyume na matakwa yao.

    Maandamano yameendelea kuongezeka tangu Bw Netanyahu aliporejea mamlakani mwishoni mwa mwaka jana, akiongoza muungano wa mrengo wa kulia, wa kitaifa katika historia ya Israel na kuahidi kukandamiza mamlaka ya mahakama.

  4. Rais mpya wa Nigeria asafiri hadi Paris na London 'kupumzika'

    Rais wa Nigeria

    Rais mteule wa Nigeria Bola Tinubu amesafiri hadi Ufaransa na Uingereza "kupumzika" na kupanga mpango wa mpito kabla ya kuapishwa kwake tarehe 29 Mei.

    Tunde Rahman, msemaji wa Bw Tinubu, katika taarifa yake Jumatano alisema rais mteule aliondoka nchini Jumanne.

    Kulingana na Bw Rahman, rais mteule baadaye ataadhimisha Hijja nchini Saudi Arabia.

    "Rais mteule aliamua kupumzika baada ya kampeni na msimu wa uchaguzi wenye shughuli nyingi kupumzika Paris na London, kujiandaa kwenda Saudi Arabia kwa Umrah (Hajj Ndogo) na mfungo wa Ramadhani unaoanza Alhamisi," Bw Rahman alisema.

    Aliongeza kuwa Bw Tinubu anatarajiwa kurejea nchini "hivi karibuni".

    Safari za mara kwa mara za rais mteule ng'ambo zinaendelea kuzusha uvumi kuhusu afya yake.

    Alifanya safari kadhaa ambazo hazijatangazwa hadi Uingereza na Ufaransa kabla ya kampeni kuanza mnamo 2022.

    Pia anakabiliwa na vita vya kisheria kuhusu ushindi wake katika uchaguzi wa rais wa mwezi uliopita.

    Maelezo zaidi:

  5. Marekani inapaswa kuheshimu mamlaka ya Uganda juu ya mswada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja

    Mbunge John Musira aliondoka bungeni Jumatatu akiwa amevalia gauni linalounga mkono sheria ya kupinga mapenzi ya jinsia moja
    Maelezo ya picha, Mbunge John Musira aliondoka bungeni Jumatatu akiwa amevalia gauni linalounga mkono sheria ya kupinga mapenzi ya jinsia moja

    Mbunge wa Uganda alipiga kura kuunga mkono mswada unaowalenga watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja ameambia BBC kwamba iwapo Marekani itaondoa ufadhili wake kufuatia hatua hiyo itakuwa sawa na "mauaji ya kimbari ya kisasa".

    Serikali ya Marekani imesema kunaweza kuwa na madhara ikiwa mswada huo utatiwa saini na Rais Yoweri Museveni kuwa sheria.

    Mbunge Charles Ayume - daktari - aliambia kipindi cha Newsday cha BBC kwamba Marekani ilitoa ufadhili muhimu kusaidia mambo muhimu ya kuokoa maisha kama vile malaria na VVU.

    Kukomesha programu hizi itakuwa sawa na "mauaji ya kimbari ya kisasa", Dk Ayume alisema.

    Akijibu ukosoaji wa Marekani wa mswada huo uliopitishwa na wabunge Jumanne, Dkt Ayume alisema kuwa uhuru wa Uganda unapaswa kuheshimiwa.

    Aliongeza kuwa kuna mambo aliyoyapinga Marekani, lakini hataki kuingilia siasa za nchi hiyo.

    Kulingana na mswada huo, watu wanaojitambulisha kuwa wapenzi wa jinsia moja nchini Uganda wanakabiliwa na tisho la kufungwa maisha ya jela.

    Pia inajumuisha adhabu ya kifo katika baadhi ya matukio. Dk Ayume alisema katika kuunga mkono hatua hiyo, alikuwa akiwakilisha maoni ya wapiga kura wake.

    Soma:

  6. EU yalaani sheria ya Uganda dhidi ya sheria ya LGTBQ

    Umoja wa Ulaya (EU) umeelezea wasiwasi wake kuhusu Bunge la Uganda kupitisha mswada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja.

    Katika taarifa yake, EU ilisema kuwa inapinga hukumu ya kifo katika hali zote.

    Imeongeza kuwa kuharamishwa kwa mahusiano ya jinsia moja ni kinyume na sheria za kimataifa za haki za binadamu.

    "Umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana na mamlaka ya Uganda na mashirika ya kiraia ili kuhakikisha kwamba watu wote, bila kujali mwelekeo wao wa kijinsia na utambulisho wa kijinsia, wanahudumiwa kwa usawa, kwa utu na heshima," taarifa hiyo iliendelea kusema.

    Siku ya Jumanne, Wabunge wa Uganda walipitisha sheria ambayo inafanya kuwa haramu kutambuliwa kama LGBTQ, na ambayo inaagiza adhabu ya kifo katika kesi za unyanyasaji wa watoto wa jinsia moja au shambulio dhidi ya watu wengine walio hatarini.

    Pia inaweka maisha ya kifungo kwa biashara ya watoto kwa madhumuni ya kuwahusisha watoto katika vitendo vya ushoga.

    Siku ya Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema kuwa sheria hiyo mpya iliyopitishwa inakwenda kinyume na haki za kimsingi za binadamu na kuitaka serikali kutazama upya utekelezaji wake.

    Wanaharakati wa mashinani na mashirika ya haki za binadamu yamehoji kuwa sheria ina uwezekano wa kuwa na athari zaidi ya watu wanaojitambulisha kuwa wachache wa kingono, na kuathiri maeneo kama vile vyombo vya habari, utoaji wa huduma za afya na haki ya faragha.

    Mswada huo hauwi sheria ya uendeshaji hadi Rais Yoweri Museveni atakapoutia saini.

    Maelezo zaidi:

  7. Waziri Mkuu wa Ethiopia amteua mkuu wa TPLF kama rais wa Tigray

    Getachew Reda ataongoza utawala wa mpito wa Tigray hadi uchaguzi ufanyike
    Maelezo ya picha, Getachew Reda ataongoza utawala wa mpito wa Tigray hadi uchaguzi ufanyike

    Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amemteua mwanachama mwandamizi wa chama cha Tigray People’s Liberation Front (TPLF) Getachew Reda kuwa mkuu wa utawala wa mpito ulioanzishwa katika eneo la kaskazini la Tigray.

    TPLF, ambayo ilipigana vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka miwili dhidi ya serikali ya shirikisho, ilimteua Bw Getachew wiki jana.

    Maelfu ya watu walikufa katika mapigano hayo na mzozo huo ukazua mzozo mkubwa wa kibinadamu.

    Pande zote zimeshutumiwa kutekeleza uhalifu wa kivita na utawala wa Marekani.

    Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya amani ambayo TPLF na serikali ya muunga walikuwa wametia saini nchini Afrika Kusini.

    Utawala wa muda wa jimbo hilo utakuwa katika nafasi yake hadi uchaguzi wa kikanda ufanyike chini ya usimamizi wa tume ya uchaguzi.Tarehe bado haijawekwa.

    Baraza la wawakilishi wa Watu wa Ethiopia hapo jana Jumatano liliondoa TPLF katika orodha ya magaidi.

  8. Ikulu ya Marekani yaionya Uganda kuhusu mswada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja

    Bunge la Uganda

    Marekani imeelezea wasiwasi wake kuhusu mswada unaopinga mahusiano ya kimapenzi ya watu wa jinsia moja uliiopitishwa bungeni Uganda siku ya Jumanne wiki hii.

    Msemaji wa ikulu ya Marekani, Karine Jean-Pierre, ameutaja mswada huo kama hatua kali zaidi iliochukuliwa kokote duniani dhidi ya jamii ya wapenzi wa jinsia moja, watu waliobadili jinsia na wale wanaoshiriki mapenzi kinyume na maumbile yao yaani LGBTQI.

    Ameongeza kuwa sheria hiyo itatia dosari hadhi ya Uganda duniani

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema rasimu ya sheria hiyo inakandamiza haki za kimsingi za binadamu na ameitaka serikali ya Uganda kutathmini upya kabla ya kuitekeleza.

    Mswada huo uliopitishwa bungeni Jumanne usiku unasema mtu yeyote anayejitambulisha kama LGBTQ anaweza kukabiliwa na kifungo cha muda mrefu gerezani. Wanaharakati wa mashirika yanayounga mkono haki za wachache wanaweza pia kufungwa jela.

    Sheria hiyo inakwenda mbali zaidi kuliko sheria zilizopo Uganda zinazopiga marufuku mapenzi ya jinsia moja.

    Kamishna wa haki za binaadamu katika Umoja wa mataifa, Volker Türk, ametoa wito kwa rais wa Museveni wa Uganda aitie saini mswada huo kuwa sheria.

    Makundi ya kutetea haki za binadamu na wanasiasa wa upinzani wamesema mswada huo unashinikiza chuki dhidi ya watu walio katika mahusiano jinsia moja na dhidi ya watu waliobadili jinsia zao.

    Uganda ni mojawapo ya nchi zaidi ya thelathini za Afrika ambazo tayari zimepiga marufuku mapenzi ya jinsia moja.

    Chini ya sheria iliyopendekezwa, marafiki, familia na wanajamii watakuwa na wajibu wa kuripoti watu walio katika mahusiano ya jinsia moja kwa mamlaka.

    Vitendo vya wapenzi wa jinsia moja tayari ni haramu katika nchi hiyo ya Afrika mashariki. Lakini mswada huo unalenga kwenda mbali zaidi na kuwafanya watu kuwa wahalifu kwa msingi wa utambulisho wao wa kijinsia.

    Maelezo zaidi:

  9. Virusi vya Marburg Tanzania: Kenya yachukua tahadhari

    m

    Wizara ya afya ya Kenya imeongeza ufuatiliaji kwenye mpaka wake na Tanzania kufuatia kugunduliwa kwa Ugonjwa wa Virusi vya Marburg.

    Mkurugenzi Mkuu Dk.Patrick Amoth amewashauri wananchi kutoa taarifa za ongezeko lisilo la kawaida la watu wanaougua homa kali na waliosafiri hivi karibuni nchini Tanzania.

    "Watu kama hao wanashauriwa kuripoti mara moja katika kituo cha afya kilicho karibu ili kufanyiwa tathmini na uchunguzi." Dk Amoth alisema katika taarifa yake.

    Mlipuko wa ugonjwa huo nchini Tanzania umeripotiwa mkoani Bukoba ambako kuna safari nyingi za watu kati ya Kisumu, magharibi mwa Kenya na eneo hilo.

    Karibu watu 161 wamefuatiliwa na wanachunguzwa. Maafisa pia wanawafuatilia watu wengine.

    Kati ya watu wanane waliopatikana na ugonjwa huo, watano wamekufa.

    Wanne kati yao wanatoka katika familia moja.

    WHO inasema ugonjwa wa Virusi vya Marburg unaua kwa wastani nusu ya walioambukizwa. Virusi hupitishwa kutoka kwa popo wa matunda na huenea kati ya wanadamu kupitia majimaji ya mwili.

    Ingawa hakuna chanjo au matibabu, wale wanaogunduliwa nayo hupewa maji kwa mdomo au kwa njia ya mishipa kwani madaktari hutibu dalili maalum za mgonjwa.

  10. Wakenya watahadharishwa kuhusu ulaji wa nyama ya nguruwe na kuku katika maduka makubwa

    m

    Taasisi ya Utafiti wa magonjwa ya binadamu nchini Kenya Kenya (KEMRI), kwa ushirikiano na Shirika la Kulinda Wanyama duniani, na Kituo cha Utafiti wa Mikrobiolojia, imewatahadharisha Wakenya kuhusu nyama ya nguruwe na kuku inayouzwa katika maduka makubwa.

    Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na watafiti hao, nyama inayouzwa kwenye maduka hayo ilikuwa na viwango vya bakteria walio sugu kwa dawa hivyo kuwa na madhara kwa walaji.

    Zaidi ya mwaka mmoja, sampuli zilikusanywa kutoka maduka makubwa katika miji mitano, ambayo ni Nairobi, Kisumu, Nakuru, Nanyuki, na Eldoret, na majaribio yalifanywa katika taasisi ya serikali.

    Utafiti huo ulibaini kuwa hali hii inaweza kuongezeka na kuwa janga la kimya kwa kuwa watu ambao wameathirika na ugonjwa huo wanaugua lakini dawa zilizopo haziwezi kuwatibu. Bakteria sugu kwa dawa.

    Zaidi ya hapo, kulingana na Victor Yamo, mwanasayansi anayeshughulikia Ulinzi wa Wanyama Ulimwenguni, shida huanzia shambani wakati mkulima anaweka nguruwe na kuku kwenye mazingira machafu.

    Amesema ni muhimu kutekeleza viwango vya juu vya usafi wa chakula na usafi wa mazingira wakati wote wa usambazaji, haswa wakati wa kuchinja na ufungaji, ili kuzuia kuingizwa kwa bakteria kwenye chakula na kuenea kwa vimelea vya chakula.

    Alilinganisha hali hiyo na janga, ambapo maisha milioni tatu yalipotea. Yamo amesema ikiwa hali hiyo itaendelea, watu wasiopungua milioni 10 wanaweza kufariki dunian kila mwaka.

    Mnamo 2019, mwandishi wa habari Dennis Okari alifichua jinsi maafisa wa maduka makubwa wasio waaminifu wanavyotumia kemikali kuongeza muda wa matumizi ya bidhaa za nyama.

  11. Homa ya Marburg: Wageni wanaoingia na kutoka Tanzania kuchunguzwa

    mm

    Kufuatia tangazo la kuzuka kwa maradhi ya Marburg katika eneo la Kagera nchini Tanzania kuathiri eneo hilo kaskazini magharibi mwa taifa hilo , serikali imeanza kuweka mikakati ya kuudhibiti ugonjwa huo.

    Kupitia taarifa iliyowekwa saini na katibu mkuu wa kudumu wa wizara ya afya Dkt.Seif Shekalaghe na kutumwa kwa vyombo vya habari, wasafiri wote wanaotoka katika eneo hilo watalazamika kujaza fomu iliyopo mtandaoni ya uchunguzi wa maradhi hayo.

    Vilevile agizo hilo ambalo linatekelezwa mara moja linasema kwamba watu wote walio katika orodha ya wale walioshikana na waathiriwa wa ugonjwa huo watachunguzwa mara kwa mara na kuzuiwa kuondoka katika maeneo waliotengewa.

    Pia wasafiri wote nchini humo watalazimika kuchunguzwa viwango vyao vya joto katika viwanja vya ndege, bandarini na maeneo yoyote ya usafiri huku wale watakaopatikana na viwango vya juu vya joto wakizuiwa kusafiri nje au ndani ya nchi hadi pale watakapomaliza muda wao wa kuchunguzwa na kupewa kibali cha kusafiri.

    Yafuatayo ni maagizo yaliotolewa na serikali.

    1. Wasafiri wote wanaoondoka na wa ndani kutoka mkoani Kagera watatakiwa kujaza Fomu ya Mtandaoni ya Ufuatiliaji wa Msafiri kupitia:

    mm

    2. Watu wote katika orodha ya ufuatiliaji wa anwani wanapaswa kufuatiliwa mara kwa mara na kuzuiwa kuondoka katika maeneo yao yaliotengwa

    3. Katika hatua yoyote ya kuingia (uwanja wa ndege, kivuko cha ardhini au bandari), joto la mwili litaangaliwa kwa wasafiri wote. Watu wote walio na hali ya homa wanapaswa kuzuiwa kusafiri ndani na nje ya nchi hadi watakapomaliza muda wa ufuatiliaji na kupewa kibali cha kusafiri na Mamlaka ya Afya ya Bandari.

    4. Wasafiri wote watapewa kadi za taarifa za afya zenye namba ya 199 na kushauriwa kujifuatilia na kuripoti dalili zozote za MVD. Wale walio na dalili zitapimwa na kutibiwa katika vituo vya afya vilivyoteuliwa vya serikali.

    5. Wakiwa nchini, wasafiri wote wa kimataifa wanapaswa kuzingatia Maambukizi, Hatua za Kuzuia na Kudhibiti kama vile usafi wa mikono, kutoshikana kimwili na Mtu mwengine , ripoti ishara au dalili yoyote kwa kutumia nambari ya bila malipo ya 199

    6. Wasafirishaji wanapaswa kuzingatia Kinga na Udhibiti wa Maambukizi ikiwa ni pamoja na usafi wa mikono na matumizi ya sanitizer.

    7. Wasafiri wote wanapaswa kuzingatia hatua za kuingia, kutoka na uchunguzi wa ndani kutekelezwa nchini.

    Soma zaidi:

    • Ijue kwa undani homa ya Marburg iliyoua watano mkoani Kagera
  12. Wabunge: Wapenzi wa jinsia moja hawana nafasi Uganda

    Bunge la Uganda limepitisha sheria mpya ambayo itawafanya watu wanaojitambulisha kuwa wapenzi wa jinsia moja kuwa ni kosa na unaweza kutumikia kifungo cha miaka 10 jela.

    Musa Ecweru, Mbunge wa Wilaya ya Amuria, alihutubia wabunge, akisema wapenzi wa jinsia moja "hawatakuwa na nafasi nchini Uganda".

    Angalia video hii fupi:

    Maelezo ya video, Wabunge Uganda : Wapenzi wa jinsia moja hawana nafasi Uganda
  13. WHO yataja Tanzania, Zambia, Zimbabwe na Afrika Kusini kama nchi zilizoathirika na kipindu pindu

    mm

    Shirika la Afya duniani limesema kuwa ugonjwa wa kipindupindu umeenea duniani kote, haswa barani Afrika na hali imekuwa mbaya zaidi tangu tathmini yake ya mwisho ya mwezi Februari mwanzoni.

    Nchi nne mpya sasa zinaripoti kuwa na kesi za ugonjwa huo ambazo ni Tanzania, Zambia, Zimbabwe na Afrika Kusini na kufanya jumla kuwa nchi 24.

    Milipuko iliyoenea inabaki kuwa Malawi na Msumbiji, na Somalia.

    Upungufu wa chanjo ya kipindupindu ya kunywa na huduma za afya kuwa na uwezo mdogo wa kukabiliana na hali inayozidi kuwa mbaya.

    Soma zaidi:

    • Kipindupindu: Ugonjwa rahisi kuupata, rahisi kuukwepa na rahisi kukuua
  14. Afrika Kusini kushauriana na Urusi kuhusu hati ya ICC ya kukamatwa kwa Putin - TASS

    m

    Shirika la habari la TASS limeripoti ikimnukuu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Afrika Kusini Naledi Pandor kwamba mamlaka ya nchi hii itafanya mashauriano na Urusi kuhusiana na hati ya kukamatwa kwa Vladimir Putin, ambayo ilitolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya Hague (ICC).

    Mwezi Agosti, mkutano wa BRICS (Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini) utafanyika Durban, Afrika Kusini. Hapo awali, mamlaka za Afrika Kusini ziliwaalika viongozi wa mataifa yote ya jumuiya hiyo, akiwemo Putin, kwenye mkutano huo.

    Wiki iliyopita, ICC ilitoa hati ya kukamatwa kwa Putin na mtoto wake Maria Lvova-Belova, akiwashuku kwa uhalifu wa kivita wakati wa uvamizi wa Ukraine.

    Waendesha mashitaka wa mahakama wanasema huenda walihusika katika kuhamishwa kwa watoto wa Ukraine.

    Tofauti na Urusi, Afrika Kusini imeidhinisha Mkataba wa Roma, ambao una maana kwamba unalazimika kuzingatia maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ikiwa ni pamoja na kukamatwa kwa Putin.

    m

    Kwa mujibu wa TASS, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini alisema kuwa suala la hati hiyo litajadiliwa na Urusi.

    "Tutasoma masharti ya sheria zetu, na, inaonekana, tutakuwa na majadiliano katika baraza la mawaziri , pamoja na wenzetu nchini Urusi ili kuamua jinsi ya kuendelea," Naledi Pandor alisema baada ya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sri Lanka ,Ali Sabri.

    Siku ya Jumanne, msemaji wa Putin, Dmitry Peskov aliwaambia waandishi wa habari kwamba Kremlin "bado haijatoa uamuzi" kuhusu safari ya rais kwenda nchini Afrika Kusini.

    Soma zaidi:

    • Mahakama ya kimataifa ya ICC yatoa hati ya kukamatwa kwa rais Vladmir Putin wa Urusi
  15. Waislamu waanza kufunga Ramadhan

    m

    Waislamu wameanza kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhan siku ya Alhamisi duniani kote baada ya mwezi kuandama majira ya jioni siku ya Jumatano.

    Nchini Kenya, Naibu Kadhi Mkuu Sheikh Sukyan Hasan nchini Kenya alitangaza kuonekana kwa mwezi katika baadhi ya Kaunti za Mandera, Wajir na Tana River siku ya Jumatano Jioni.

    Ramadhan ambao ni mwezi wa tisa wa kalenda ya Kiislamu, unachukuliwa kuwa mtakatifu zaidi na Waislamu.

    Waumini wametakiwa kuungana wanapoanza saumu yao na kuepuka jambo lolote litakaloingilia mfungo wao.

    Soma zaidi:

    • Waislamu waanza kufunga Ramadhan
    • Ramadhan: Fahamu vyakula ambavyo waliofunga wanastahili kula au kutokula
    • Ni nani asiyepaswa kufunga mwezi wa Ramadhani?
  16. Ripoti ya uchunguzi yabaini uzembe wa marubani katika ajali ya Precision,Tanzania

    mm

    Tanzania imetoa ripoti ya pili ya ajali ya Ndege ya Precision Air iliyotokea tarehe 6 Novemba ,mwaka 2022 katika Ziwa Victoria, Bukoba, Mkoa wa Kagera na kusababisha vifo vya watu 19 na wengine 24 kuokolewa.

    Ndege ya Precision Air iliyokuwa inatoka Dar es Salaam kwenda Bukoba ilikuwa na watu 43 kati yao, 39 abiria, marubani wawili na wahudumu wawili.

    Ripoti ya awali ya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Shirika la Precision Air, ilitoka mwishoni mwa mwezi Novemba, 2022, na ilibainisha kuwa kulikuwa na ucheleweshwaji katika uokozi kwa jeshi la Wana maji kuchelewa kufika katika eneo la tukio.

    Vyombo vya habari nchini humo, vimeripoti kuwa ripoti mpya iliyotoka Jumatano imeelezea kuwa marubani wa ndege hawakuwa na tatizo la kiafya, ndege ilikuwa imeandikishwa kihalali, hali ya hewa ya katika uwanja wa Bukoba haikuwa nzuri, hali mbaya ya hewa iliathiri marubani kutekeleza jukumu lao.

    Vilevile marubani hawakuwa makini katika kufuata ishara za tahadhari zilizotolewa, ndege iligonga kwanza bawa lake la kushoto wakati ikianguka, pia ilianguka kwa kasi na kugonga sehemu ya mbele kwenye kina cha maji ya ziwa Victoria na vifaa vyote vya kuongozea ndege vilikuwa vinafanya kazi kwa kuzingatia matakwa ya rubani.

    Soma zaidi:

    • Precision Air: Kenya kuiruhusu kampuni ya ndege kutoka Tanzania licha ya mgogoro
  17. Refa asimamishwa kazi kwa kutumia simu ya shabaki kukataa goli

    m

    Mwamuzi wa Misri Mohamed Farouk amesimamishwa kazi kwa kutumia simu ya mtazamaji kukataa bao katika mechi ya ligi.

    Al-Nasr walidhani walikuwa wamefunga bao la kusawazisha dakika za lala salama wakiwa ugenini kwa Suez katika mechi ya ligi ya daraja la pili Ijumaa iliyopita.

    Hakuna mwamuzi msaidizi wa video (VAR) katika daraja la pili la Misri, lakini Farouk alitumia simu kutazama video ya marudio baada ya wenyeji kulalamika kuwa kuna mchezaji aliyeugusa mpira kwa mkono.

    Farouk kisha alifanya uamuzi wa kulikataa bao hilo. Shirikisho la Soka la Misri lilisema katika taarifa yake kwamba Vitor Pereira, ambaye alichukua nafasi ya Mark Clattenburg kama mkuu wa Kamati ya Waamuzi wa Misri mapema mwezi huu, aliamua kuwasimamisha kazi waamuzi wote kwa "muda usiojulikana".

    “Kamati iliamua kuchunguza tukio wakati Mohamed Farouk, mwamuzi wa mechi hiyo alipotumia simu ya mkononi kukagua picha za matukio ya mechi hiyo,” FA ya Misri iliongeza.

    Suez ilifunga bao la tatu muda mfupi baada ya bao lililokataliwa na kupelekea ushindi wa 3-1, zikiwa zimesalia dakika 15 za mapumziko.

    Farouk aliondoka uwanjani chini ya ulinzi wa polisi, huku kukiwa na maandamano ya wachezaji na viongozi wa Al-Nasr, ambao wametishia kumchukulia hatua za kisheria mwamuzi huyo kwa kukiuka kanuni.

  18. Hujambo...karibu katika matangazo ya moja kwa moja ya BBC Swahili leo ikiwa Alhamisi tarehe 23.03.2023