Rais wa Urus Vladmir Putin atuma meli ya makombora kufanya mafunzo katika bahari ya Atlantiki

Katika mkutano wa video Putin alisema meli hiyo ilikuwa na silaha za hypersonic za Zircon.

Moja kwa moja

  1. David Gold: Mwenyekiti mwenza wa West Ham United afariki baada ya kuugua kwa muda mfupi

    w

    Mwenyekiti mwenza wa klabu ya West Ham United David Gold amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 86 baada ya kuugua kwa muda mfupi, Shabiki mkubwa wa Hammers, klabu hiyo ilisema aliaga dunia "kwa amani" Jumatano asubuhi akiwa na mchumba wake na binti zake kando yake.

    Gold, ambaye awali alikuwa mwenyekiti na mmiliki mwenza wa Birmingham City, alikua mwenyekiti mwenza wa West Ham na David Sullivan mnamo 2010.

    "Nimehuzunika sana kusikia habari hizi," alisema meneja David Moyes. "Kwa niaba ya wachezaji wote na wafanyakazi wangu kwenye uwanja wa mazoezi, ningependa kutoa rambirambi zetu za dhati kwa familia ya David Gold katika wakati huu mgumu sana.

    "Bw Gold alikuwa mgeni wa mara kwa mara wa Rush Green na kila mara alikuwa chanzo cha kuungwa mkono na kunitia moyo sana mimi na wachezaji. Ilikuwa wazi kwamba alikuwa na mapenzi ya dhati kwa klabu na alikuwa mfuasi wa kweli moyoni mwake. "Alipendezwa sana na watu wanaofanya kazi nyuma ya pazia na alikuwa na hamu kila wakati kusaidia kwa njia yoyote anayoweza. alisema

    David alikuwa na uhusiano wa muda mrefu na The Hammers, baada ya kukua na kucheza katika uwanja wa Green Street, na aliwakilisha klabu katika ngazi ya chini.

    Muda wake katika klabu hiyo ulisimamia uhamisho wake wa kwenda London Stadium, pamoja na kushuka daraja na baadaye kupandishwa kwenye Ligi Kuu na kucheza Ligi ya Europa. Nje ya soka, Gold pia alikuwa mwenyekiti wa mnyororo wa reja reja Ann Summers na hapo awali alikuwa akimiliki kampuni ya majarida ya watu wazima na huduma ya shirika la anga.

  2. Rais wa Urus Vladmir Putin Atuma Meli ya makombora Kufanya Mafunzo Katika Bahari ya Atlantiki

    r

    Rais Vladmir Putin siku ya Jumatano aliongoza uzinduzi wa meli ya kivita iliyo na makombora mapya ya kivita ya hypersonic kwenye safari ya mafunzo kwenye Bahari ya Atlantiki, Hindi na Mediterania.

    Katika mkutano wa video na waziri wa ulinzi Sergei Shoigu na Igor Krokhmal, kamanda wa frigate, Putin alisema meli hiyo ilikuwa na silaha za hypersonic za Zircon.

    "Wakati huu meli ina mfumo wa hivi karibuni wa makombora ya hypersonic - Zircon - ambayo haina mfano," Putin alisema. "Ningependa kuwatakia wafanyakazi wa meli mafanikio katika huduma yao kwa manufaa ya nchi yetu".

    "Lengo kuu la ujumbe huo litakuwa kukabiliana na vitisho kwa Urusi na kusaidia amani na utulivu wa kikanda pamoja na nchi marafiki," Shoigu alisema. "Katika mazoezi, kutakuwa na mafunzo kwa wafanyakazi juu ya kupeleka silaha za hypersonic na makombora ya masafa marefu," alisema.

    Shoigu aliongeza kuwa makombora ya hypersonic, yanayojulikana kama Tsirkon au Zircon, yanaweza kushinda mfumo wowote wa ulinzi wa kombora.

    Makombora hayo yanaruka mara tisa ya kasi ya sauti na yana masafa ya zaidi ya kilomita 1,000, Shoigu alisema.

    Urusi, China na Marekani kwa sasa ziko kwenye mbio za silaha za hypersonic na kila mmoja anataka kuwa na silaha bora zaidi.

  3. Muandaaji wa tamasha la muziki Uganda ashitakiwa kwa watu kukanyagana Mwaka mpya

    m

    Muandaaji wa tamasha la muziki nchini Uganda ameshtakiwa kwa makosa tisa ya uzembe kufuatia vifo vya watu 10 katika mkesha wa mwaka mpya, mjini Kampala.

    Abbey Musinguzi alifikishwa mahakamani siku ya Jumanne jioni.

    Licha ya kwamba, Bwana Abbey alikanusha mashtaka yote, aliwekwa rumande katika gereza la Luzira.

    Muandaaji huyo anadaiwa kusababisha mkanyagano katika eneo la Freedom City Mall alipofunga maduka na kuacha lango moja tu kwa zaidi ya watu 20,000 kutoka.

    Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 52 alikamatwa siku ya Jumatatu.

    Wakili wake anadai mteja wake analengwa kwa sababu anajulikana kuwa mfuasi wa kiongozi wa upinzani wa Jukwaa la Umoja wa Kitaifa Robert Kyagulanyi, anayejulikana pia kama Bobi Wine.

    Wakati huohuo, polisi wamewahoji watu zaidi akiwemo mmiliki wa jengo hilo kurekodi taarifa juu ya tukio hilo baya.

    Soma zaidi:

    • Aliyenusurika kwenye tukio la kukanyagana asimulia
  4. Watu tisa wauawa katika milipuko miwili ya magari Somalia

    w

    Takriban watu tisa wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mashambulio mawili ya mabomu yaliyotegwa kwenye gari katikati mwa Somalia siku ya Jumatano, shirika la habari la AFP linaripoti likimnukuu afisa wa usalama wa eneo hilo.

    Afisa huyo alisema washambuliaji walitumia magari yaliyosheheni vilipuzi kufanya shambulio hilo katika mji wa Mahas.

    Wanamgambo wameendelea kufanya mashambulizi katikati na kusini mwa Somalia licha ya hivi karibuni wanajeshi wa serikali wakisaidiwa na vikosi vya Umoja wa Afrika na wanamgambo wa eneo hilo kutwaa tena maeneo yaliyokuwa yametekwa na kundi la al-Shabab.

  5. Msumbiji kuingia katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

    m

    Msumbiji imechukua nafasi ya Kenya katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne ikihaidi kutoa kipaumbele katika vita dhidi ya ugaidi.

    Nchi hiyo itahudumu katika baraza hilo kama mwanachama asiye wa kudumu kwa miaka miwili ijayo.

    "Tutakabiliana sana na ugaidi," alisema balozi wa Msumbiji katika Umoja wa Mataifa, Pedro Comissário.

    Msumbiji imekuwa ikipambana na waasi wa Kiislamu katika jimbo lake la kaskazini la Cabo Delgado kwa muda wa miaka mitano iliyopita.

    Mzozo huo umesababisha zaidi ya watu milioni moja kuyahama makazi yao na wengine karibu 4,000, kuuawa kwa mujibu wa takwimu rasmi.

    Bw Comissário alisema nchi hiyo pia itasisitiza mabadiliko katika Baraza la Usalama ili kushughulikia "wasiwasi wa Afrika".

    "Ni muhimu kuzingatia mageuzi ya Baraza la Usalama ili kutoa ufumbuzi kwa vitu ambavyo Afrika inavihitaji kutoka katika eneo ambalo limekumbwa na dhuluma za kihistoria. Hatuna mwanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama,” akasema Bw Comissário.

    Baraza la Usalama lina wanachama watano wa kudumu - Marekani, Urusi, Ufaransa, Uingereza na China - na wanachama 10 wasio wa kudumu.

    Soma zaidi:

    • Vita vya Ukraine: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni nini na linafanya kazi vipi?
    • Samia Suluhu: Tanzania kuhudhuria Kikao cha Umoja wa Mataifa kuna tafsiri gani?
  6. Mamlaka ya dawa na chakula nchini Marekani yaruhusu vidonge vya kutoa mimba kuuzwa madukani

    m

    Kwa mara ya kwanza maduka ya dawa ya rejareja nchini Marekani yanaweza kuuza vidonge vya kutoa mimba, chini ya mabadiliko ya sheria mpya na utawala wa Biden.

    Wagonjwa wanaweza kupata vidonge vya kutoa mimba(mifepristone) - ambayo ni salama na yenye ufanisi katika kutoa mimba kutoka kwa mtoa huduma wa afya.

    Maelezo ya matumizi bado yanahitajika chini ya sheria mpya, lakini wagonjwa sasa wanaweza kuchukua vidonge hivyo dukani au kutumiwa kwa njia ya barua.

    Hatua hiyo inaweza kuongeza kasi ya utoaji mimba kwa kutumia dawa.

    Vidonge vya kutoa mimba vimekuwa vikitafutwa zaidi kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Juu wa mwaka jana uliobatilisha haki ya shirikisho ya kutoa mimba, huku mataifa kadhaa yakipiga marufuku au kuzuia vikali upatikanaji wa utoaji mimba.

    Zaidi ya nusu ya utoaji mimba nchini Marekani tayari unafanywa kwa tembe badala ya upasuaji, kulingana na Taasisi ya Guttmacher inayounga mkono.

    Mwezi Disemba mwaka 2021, Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) ilisema itaondoa kabisa hitaji la wagonjwa kupata dawa kibinafsi kupitia mtoa huduma ya afya, kama sehemu ya hatua yake inayotokana na janga.

    Siku ya Jumanne, FDA ilitoa taarifa mpya katika tovuti yake na mahitaji mapya, ikisema dawa hiyo "inaweza kutolewa na maduka ya dawa yaliyoidhinishwa au chini ya usimamizi wa daktari aliyeidhinishwa".

    Danco Laboratories na GenBioPro, kampuni mbili za Marekani zinazotengeneza dawa hiyo, zilithibitisha kwa taarifa tofauti kwamba wakala huo ulikuwa umewafahamisha kuhusu uamuzi wake.

    Hatua hiyo imesifiwa kama "hatua muhimu" mbele na Chuo cha Madaktari wa uzazi cha Marekani na Madaktari wa Magonjwa ya Wanawake.

    Soma zaidi:

    • Kliniki za utoaji mimba zimeanza kufungwa baada ya uamuzi wa Mahakama ya Juu
    • Utoaji mimba nchini Marekani - nini kinafanyika?
  7. Jeremy Renner: Muigizaji wa Avengers awashukuru mashabiki wake baada ya kugongwa na jembe la kuondoa theluji

    m

    Muigizaji wa Marekani Jeremy Renner amewashukuru mashabiki wake kwa kumpa pole baada ya kujeruhiwa vibaya na jembe la theluji.

    Aliweka picha ya uso wake wenye makovu kwenye Instagram, Renner alisema "hayuko vizuri kwa sasa hawezi hata kuandika".

    Nyota huyo wa Avengers alipelekwa hospitalini Jumapili baada ya ajali hiyo nje ya nyumba yake huko Reno, Nevada.

    Renner aliangukiwa na jembe lake la theluji, ambalo lina uzani wa karibu 14,330lb (6,500kg) - mara tatu ya uzito wa gari - polisi wa eneo hilo alisema.

    Alipata majeraha kifuani na majeraha ya mifupa, msemaji wake alisema Jumatatu.

    Wakati huo alikuwa katika hali nzuri lakini katika uangalizi maalum wa wauguzi.

    Katika mtandao wa Instagram akiwa kwenye kitanda cha hospitalini Jumanne jioni, Renner mwenye umri wa miaka 51, aliandika: "Asanteni nyote kwa maneno yenu ya fadhila. Siko vizuri sasa nashindwa kuandika. Lakini ninatuma salamu za upendo kwenu wote.

    Ruka Instagram ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa Instagram ujumbe

    Tukio hilo la kusikitisha lilitokea baada ya dhoruba kutokea mwaka mpya na kuacha karibu futi 3 za theluji ardhini, Mamlaka ya Kaunti ya Washoe Darin Balaam ilisema katika mkutano na waandishi wa habari.

    Soma zaidi:

    • Theluji yaathiri maisha Marekani
    • Theluji nchini Pakistani: Mtu aliyekwama chini ya Theluji kwa saa kadhaa asimulia alichokiona
  8. Mama na binti yake wahukumiwa kwa kuuza viungo vya miili ya wafu

    th

    Mmiliki wa zamani wa Chumba cha kuhifadhu maiti na mama yake wamehukumiwa kifungo cha jela huko Colorado baada ya kupasua mamia ya miili na kuuza sehemu za mwili.

    Waendesha mashtaka walisema Megan Hess, 46, na Shirly Koch, 69, walikata maiti 560 na kuuza viungo vya miili bila idhini kati ya 2010 na 2018.

    Wanawake wote wawili walikiri makosa ya ulaghai mapema mwaka huu.

    Hess atafungwa jela 20, huku Koch akihukumiwa miaka 15 jela.

    Kulingana na waendesha mashtaka huko Colorado, wawili hao mama na binti walivuna sehemu za miili, na wakati mwingine miili mizima katika na kuviuza .

    Hess - ambaye aliendesha biashara ya Jumba la Mazishi la Sunset Mesa katika mji wa Montrose - alitoza familia hadi $1,000 (£834) kwa uchomaji maiti ambao haukufanyika na badala yake kuikabidhi miili hiyo kama michango bila malipo , waendesha mashtaka walisema.

    "Wanawake hawa wawili waliwadhulumu wahasiriwa ambao waliwageukia wakati wa huzuni," Leonard Carollo, ajenti maalum wa FBI anayesimamia Denver, alisema katika taarifa.

    "Lakini badala ya kutoa mwongozo, wanawake hawa wenye pupa walisaliti imani ya mamia ya wahasiriwa na kukata viungo vya wapendwa wao’

    Kesi hiyo ilichochewa na uchunguzi wa Reuters, ambao ulisababisha FBI kuvamia nyumba hiyo mwaka wa 2018. Ni kinyume cha sheria nchini Marekani kuuza viungo, lakini uuzaji wa viungo vya mwili kwa sasa haudhibitiwi na sheria ya shirikisho ya Marekani.

    Taarifa za waathiriwa waliojawa hisia zilitawala kikao cha hukumu cha Jumanne.

    "Wakati Megan alipoiba moyo wa mama yangu, alivunja moyo wangu," alisema Nancy Overhoff, kulingana na Denver Post. Erin Smith alisema: "Tumekuja leo kusikia pingu zikikazwa."

    Akiielezea kama "kesi ya kuhuzunisha zaidi ambayo nimewahi kukumbana nayo kwenye benchi", Jaji Christine Arguello aliamuru wanawake hao wawili wafungwe gerezani mara moja.

  9. Bunge la Marekani latumbukia kwenye mzozo baada ya Kevin McCarthy kupoteza kura za uspika

    m

    Katika siku yenye vituko vya kisiasa ambavyo havikuonekana katika Bunge la Congress kwa karne, kiongozi wa Republican Kevin McCarthy alirudia kushindwa katika nia yake ya kuchaguliwa kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani.

    Bunge liliahirishwa bila ya kuwa na spika siku ya Jumanne usiku - mara ya kwanza tangu mwaka 1923 ambapo walishindwa kuchagua kiongozi baada ya kura ya awamu ya kwanza kugonga mwamba.

    Kuanza kwa bunge jipya kulipaswa kuwa ushindi kwa Chama cha Republican kwani kilichukua udhibiti wa baraza la chini la bunge kufuatia uchaguzi wa Novemba.

    Badala yake, Bw McCarthy alikabiliwa na upinzani kutoka kwa safu yake mwenyewe na kuandika historia kwa sababu zote zisizo sahihi.

    Mbunge huyo wa California amepoteza kura tatu mfululizo za Spika mpaka sasa, na haijafahamika kama anaweza kupata ushindi wakati Bunge litakaporejea Jumatano kujaribu tena kupiga kura.

    Hata hivyo wataendelea kupiga kura hadi mtu apate kura nyingi.

    Na hata kama Bw McCarthy atapata ushindi, wachambuzi wanaonya, juu ya msukosuko uliopo Republican wenye msimamo wa wastani na wa mrengo wa kulia kwenye vita kati yao wenyewe kwa wenyewe.

    'Mazungumzo yalimfanya aonekane dhaifu'

    Wanachama wa Republican walipata udhibiti wa Bunge hilo kwa kura chache mnamo Novemba, Bw McCarthy alikuwa na kura chache tu zilizosalia katika nia yake ya kuwa Spika. Hilo liliruhusu kundi la Conservative la wenye msimamo mkali kuungana kupinga uteuzi wake.

    Mgawanyiko huo ulikuja kwa muda mrefu, kulingana na waangalizi wa Republican.

    "Kevin McCarthy hajatengeneza urafiki na baadhi ya makundi kwa muda, amejitengenezea maadui wengi," mtetezi mmoja wa chama cha Republican, ambaye aliomba jina lake lisitajwe ili azungumze kwa uwazi kuhusu kura zilizopigwa Jumanne.

    "Kuna watu hawampendi kwa sababu za kisiasa, na wengine kwa sababu za kibinafsi." Bw McCarthy aliingia katika mazungumzo na wapinzani wake - ambao wanamuona kama mtu wa kawaida na mwenye uchu wa madaraka.

    Wakati fulani, inasemekana alikubali kubadili kanuni za Bunge ili kurahisisha kumwondoa madarakani Spika aliyepo na kuwapa wapinzani wake kuangalia kwa ukubwa juu ya mamlaka yake.

    "Ukweli kwamba alikuwa akijadiliana na Republican wakati wote ulimfanya aonekane dhaifu sana hadi kufikia hatua ya kukata tamaa," mtetezi wa Republican alisema.

    Wapinzani wake wanahisi ujasiri Ubatili wa njia hiyo ulikuwa wazi siku ya Jumanne

    Soma pia:

    • Bunge la Congress Marekani latambua ndoa ya jinsia moja ili kuilinda dhidi ya mahakama
  10. Los Angeles kulipa dola milioni 20 kwa ardhi ya familia ya watu weusi

    m

    Los Angeles imekubali kulipa $20m (£16.7m) kwa ajili ya fukwe ambayo ilinyakuliwa kutoka kwa familia ya watu weusi miaka ya 1920 na kurejeshwa kwa warithi wao msimu huu wa joto.

    Fukwe ya Bruce ilinunuliwa mnamo 1912 kwa ajili ya kutengeneza eneo la mapumziko kwa watu weusi wakati ambao ubaguzi wa rangi ulikuwa umeenea.

    Fukwe hiyo ipo katika mji maarufu wa Manhattan Beach na ilichukuliwa kwa nguvu na baraza la mtaa mnamo 1924.

    "Wazao wa Bruce wangekuwa matajiri tayari ikiwa ardhi yao haingechukuliwa kamwe", alisema afisa wa LA akitangaza kuiuza.

    "Kushikiliwa kwa fukwe ya Bruce kwa karibu karne moja iliyopita ilikuwa dhuluma ambayo haikutendewa tu Willa na Charles Bruce lakini vizazi na vizazi vyao ambavyo kwa hakika wangekuwa mamilionea," alisema Janice Hahn, mwenyekiti wa Bodi ya Wasimamizi wa Kaunti ya LA.

    "Haya ni mapambano ambayo yamelenga kuinufaisha familia ya Bruce, na wanahisi kilicho bora kwao ni kuuza mali hii kwa kaunti kwa karibu $20m na ​​hatimaye kujenga tena utajiri wa kizazi ambao waliminywa kwa karibu karne moja," alisema. Aliendelea katika taarifa yake ya Jumanne.

    m

    "Hivi ndivyo malipo yanavyoonekana na ni mfumo ambao nna matumaini serikali itafuata kwa maeneo yote nchini."

    Malipo ni marejesho ya utumwa - msamaha na ulipaji kwa raia weusi ambao mababu zao walilazimishwa kuingia katika biashara ya utumwa.

    Lakini ikiwa serikali inapaswa kufanya malipo, na jinsi ya kulipwa kuna utata wa kisiasa.

    Willa na Charles Bruce walinunua mashamba hayo mawili kwa dola 1,225 mnamo mwaka 1912, walimwambia mwandishi wa habari wakati huo:

    "Popote tulipojaribu kununua ardhi kwa ajili ya mapumziko ya ufukwe, tumekataliwa, lakini nina miliki ardhi hii na ninaenda kukaa nayo."

    Lakini idara ya polisi ya eneo hilo iliweka alama zinazozuia maegesho hadi dakika 10, na mmiliki mwingine wa eneo hilo hakuweka alama zozote, na kuwalazimisha watu kutembea nusu maili kufika majini. Hata walikabiliwa na vitisho kutoka kwa kundi la kigaidi la kibaguzi la Ku Klux Klan.

    Soma:

    • George Floyd: Maandamano makubwa ya kupinga ubaguzi yafanyika Marekani
    • Watatu wauawa kisa cha ubaguzi wa rangi Marekani
  11. Mimi ni mrefu kuliko yule Mghana -mtu mrefu wa Ethiopia

    th

    Makala yetu ya hivi majuzi kuhusu Mghana ambaye alidhaniwa na wengine kuwa mtu mrefu kuliko wote, imemfanya Muethiopia mmoja kujitokeza kwenye mitandao ya kijamii kusema kuwa yeye ndiye mtu mrefu zaidi.

    Negewo Jima aliweka picha yake sambamba na ile ya Sulemana Abdul Samed kwenye mtandao wa Facebook akisema “usiwahi kukata tamaa”.

    "Mlete ikiwa unataka - mtu huyu hatakuwa mrefu kuniliko," alisema katika chapisho la awali.

    "Kutokana na kile ninachokiona kwenye picha, naweza kusema yeye sio mrefu kuniliko," Bw Negewo baadaye aliambia BBC.

    Akiwa na urefu wa 7 ft 4.6in (225cm) Bw Negewo anasemekana kuwa mtu mrefu zaidi wa Ethiopia.

    Licha ya baadhi ya watu hapo awali kusema kwamba Mghana mwenye umri wa miaka 29 alikuwa na futi 9 na 6 mwandishi wa BBC alimpima na kumpata kuwa 7ft 4in - ambayo kwa hakika inaonenya ni mfupi kuliko Muethiopia huyo.

    Hapo awali Waethiopia wengine walisema walikuwa warefu kuliko Bw Negewo, lakini baadaye iligundulika kuwa hii haikuwa kweli.

    Soma pia

    • Je,huyu ndiye mtu mrefu zaidi duniani?
    • Julius Charles: 'Kuna wanaozimia wakiniona na wengine hukimbia'
  12. Cristiano Ronaldo:Nimeimaliza kazi yangu Ulaya

    th

    Cristiano Ronaldo anasema kazi yake barani Ulaya imekamilika, lakini alikuwa na "nafasi nyingi" kutoka kwa vilabu vingine kabla ya kujiunga na Al Nassr ya Saudi Arabia.

    Alijiunga na Al Nassr kama mchezaji huru siku ya Ijumaa baada ya kuondoka Manchester United kufuatia mahojiano yenye utata ambapo aliikosoa klabu hiyo.

    Nahodha huyo wa Ureno, 37, alisema alikuwa na ofa kutoka kwa vilabu vya Brazil, Australia, Marekani na Ureno.

    "Nilitoa ahadi yangu kwa klabu hii," alisema wakati wa uzinduzi wake Jumanne.

    "Nilishinda kila kitu, nilichezea vilabu muhimu zaidi barani Ulaya na sasa ni changamoto mpya barani Asia."

    Ronaldo anaripotiwa kupokea mshahara mkubwa zaidi katika historia ya soka wa zaidi ya £177m kwa mwaka katika mkataba unaoendelea hadi 2025.

    "Kama hakuna anayejua, naweza kusema sasa nilikuwa na fursa nyingi Ulaya, vilabu vingi nchini Brazil, Australia, Marekani, hata Ureno, vilabu vingi vilijaribu kunisajili," Ronaldo aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano wake wa kwanza na wanahabari.

    Unaweza pia kusoma;

    • Cristiano Ronaldo asema anahisi 'kusalitiwa' na Manchester United
    • Je, Manchester United ilifanya makosa kumsajili tena Ronaldo?
  13. Rais Samia abadilisha viongozi wakuu serikalini,mwakilishi wa kudumu UN atenguliwa

    m

    Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya wateule wake akiwemo kiongozi mkuu wa idara ya usalama wa taifa Diwani Athuman ambaye amebadilishiwa majukumu yake na kuwa katibu mkuu wa Ikulu huku nafasi yake ikichukuliwa na Said Hussein Nassoro. Awali, Nassoro alikuwa naibu mkurugenzi mkuu na mkurugenzi wa shughuli za ndani wa idara hiyo.

    Diwani Athuman ambaye ni Kamishana wa Jeshi la Polisi, amehudumu katika nafasi hiyo kwa takribani siku 1,210, tangu alipoteuliwa na Rais wa wakati huo, Hayati John Magufuli Septemba 12 mwaka 2019.

    Kabla ya Athumani kushika wadhifa huo wa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa alihudumu kama mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

    Hata hivyo ,Rais Samia amefanya mabadiliko mengine kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga ambaye ameteuliwa kwenda New York nchini Marekani kuwa Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa (UN).

    Balozi Kattanga ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa katibu mkuu kiongozi Machi 31, 2021, alichukua nafasi ya Dk Bashiru Ali ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Kuteuliwa.

    Kattanga aliteuliwa kushika wadhifa huo kutoka kuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan na sasa anakwenda kuchukua nafasi ya Profesa Kennedy Gaston.

    Akitoa sababu za kumrejesha nchini Profesa Kennedy, Rais Samia amesema katika mkutano wa Bunge wa Novemba mwaka jana kulikuwa na mjadala mzito wa matumizi ya fedha na madaraka katika ofisi mbalimbali za kibalozi na ulimwenguni na Serikali inazifanyia kazi dosari hizo.

    Unaweza kusoma zaidi:

    • Rais wa Tanzania amaliza marufuku ya miaka 6 kwa mikutano ya vyama vya siasa
    • Kufunguliwa kwa mikutano ya hadhara ya siasa Tanzania: 'Tumepokea kwa tahadhari' - Wapinzani
  14. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja leo tarehe 4 Januari 2023