Rais wa Ufaransa alaani shambulio la Nice

Iliyochapishwa

Rais wa Ufaransa ameongeza hali ya hatari kwa miezi 3 kufuatia vifo vya watu 80 baada ya kutokea shambulio katika mji wa Nice.

Francois Hollande ameliita shambulio hilo kuwa ni la kigaidi.

Tukio hilo limetokea baada ya dereva wa lori kuendesha kwa kasi gari hilo kwenye umati wa watu waliokuwa wakiangalia maonyesha ya fataki katika sherehe za siku ya Uhuru.

Mwendesha mashtaka wa Nice Jean-Michel Pretre amesema polisi wamempiga risasi na kumuua dereva wa gari hilo ambalo limegunduliwa kubeba bunduki na maguruneti.

Maafisa wa kupambana na ugaidi wanachunguza tukio hilo.

Rais Hollande amesema jitihada za kutafuta usaidizi wa maelfu ya wanajeshi kuwasaidia polisi zitaendelea.

Katika hatua nyingine, vyombo vya habari Ufaransa vinasema makaratasi ya utambulisho ya Mfaransa mwenye asili ya Tunisia yamepatikana kwenye gari hilo.

Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo.

Tayari tukio hilo limeshutumiwa vikali kimataifa, Rais wa baraza la Ulaya Donald Tusk, amesema ni la kusikitisha kwamba watu waliokuwa wanasherehekea uhuru na usawa wameshambulia.

Huko Nice kwenyewe, tamasha lililoandaliwa Ijumaa na muimbaji maarufu Rihanna na kundi la musiki wa Jazz lililotarajiwa kuanza Kesho jumamosi limefutiliwa mbali.