Ukraine na Urusi: Vita ilivyoiweka njia panda Uturuki , mwanachama wa NATO na rafiki wa Putin

Chanzo cha picha, Getty Images
Saa chache baada ya Urusi kuivamia Ukraine, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilisema kitendo hicho "hakikubaliki" na "ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa."
Akizungumza na rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amelaani uvamizi wa Urusi akisema ni kama "pigo kubwa kwa amani na utulivu wa kikanda."
Msimamo wa Uturuki uliwashangaza baadhi, kwa kuwa (pande hizo) Ankara na Moscow zimekuwa washirika muhimu wa kimkakati katika eneo la Caucasus Kusini kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.
Serikali zote mbili zimekuwa zikisaidiana kwa kudumisha sera ya kupambana na Marekani na ya kupambana na Ulaya, ikiunga mkono utawala ama serikali kama ya Nicolás Maduro nchini Venezuela, na kuimarisha uhusiano wa kibiashara.
Leo, Urusi ni moja ya washirika kuu wa biashara wa Uturuki, muuzaji wake mkuu wa gesi ya asili, na watalii wengi kutoka Urusi hufuruika katika maeneo ya mapumziko ya bahari ya Kituruki kwenye pwani za Aegean na Mediterranean.
Mengi zaidi
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
- SILAHA:Mzozo wa Ukraine:Makombora ya stinger na silaha nyingine kali zinazotumiwa Ukraine
Urafiki wa wazi kati ya Putin na Erdogan umekuwa na mambo mengi ya kupanda na kushuka. Umeshinda maono yao katika vita huko Azerbaijan, Libya na Syria, ambapo Uturuki iliitungua ndege ya Urusi.
Urafiki wao pia umepita hata mauaji ya balozi wa Urusi mjini Ankara.
Urafiki wa mashaka
Ter Minassian Taline, mwanahistoria kutoka Taasisi ya Taifa ya Lugha za Mashariki na Ustaarabu (INALCO) huko Paris, anaelezea kama urafiki wao ni wa kweli ama wa "dhati".
"Kuna utata mkubwa katika uhusiano kati ya Urusi na Uturuki. Putin na Erdogan wanaelewana vizuri sana na kuelewa matatizo ya kila mmoja. Wao ni marafiki, lakini wakati huo huo maadui," mtaalamu katika masomo ya Soviet na Mashariki ya Kati aliiambia BBC Mundo.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Kwa kweli ni urafiki wa mashaka ambapo kila mtu anaangalia maslahi yao," anaendelea.
Minassian Taline anaelezea kuwa msimamo wa Uturuki katika mgogoro wa Urusi na Ukrainian ni mgumu haueleweki kwa sababu Ankara pia inaendelea kushikilia uhusiano wa kina na Kiev, hasa katika eneo la kijeshi.
Hivi karibuni uhusiano huu umeiruhusu Ukraine kuilinda miji yake kutokana na mashambulizi ya mabomu ya Urusi kutokana na ndege kadhaa zisizo na rubani za Uturuki walizozipata Ukraine.
Katika wiki za hivi karibuni, video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha ndege zisizo na rubani za Bayraktar TB2 zikisambaratisha vifaru vya Urusi, magari yake ya kivita na mifumo ya ulinzi wa makombora.
Uturuki ilianza kuuza silaha hizi kwa Ukraine mwaka 2019, na Kiev ilikuwa tayari imezitumia kupambana na waasi wanaounga mkono Urusi katika mkoa wa mashariki wa Dombas.
Ndege hizo zisizo na rubani zinatengenezwa na kampuni ya ulinzi ya Baykar, inayomilikiwa na familia ya mkwe wa Erdogan.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Putin labda anakasirishwa kuona kwamba Waukraine wanatumia ndege zisizo na rubani za kijeshi zinazozalishwa na Uturuki," anasema Ter Minassian Taline.
Jukumu la Upatanishi
Kiev pia imekuwa ikiunga mkono sera ya kigeni ya Uturuki mara kwa mara.
Ingawa haikutuma silaha, Ukraine iliziunga mkono Azerbaijan na Uturuki wakati wa vita vya Nagorno-Karabakh mnamo 2020.
Lakini katika mgogoro wa sasa, Uturuki imeamua kuchukua jukumu la upatanishi, kwa mujibu wa Dimitar Bechev, mtaalam wa Urusi na Ulaya Mashariki katika Chuo Kikuu cha oxford huko britain.
"Erdogan anataka kuwezesha mazungumzo kati ya Zelensky na Kremlin (Putin). Alikuwa anapendekeza hilo hata kabla ya kuanza kwa vita, wakati alipotembelea Kiev mwezi Februari," anasema katika mahojiano na BBC Mundo.
"Haijulikani kama Ankara inaweza kufanikiwa katika jukumu hili," anaongeza.
Nafasi ya "faida"
Licha ya hayo, jukumu la upatanishi la Uturuki limeendelea.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, serikali ya Uturuki ilisema Kiev na Moscow zimepiga hatua katika mazungumzo ya kumaliza vita na kwamba pande hizo mbili zilikuwa karibu na makubaliano.
Cavusoglu alisisitiza kuwa Uturuki ilikuwa inawasiliana na timu za mazungumzo za nchi zote mbili, lakini alikataa kutoa maelezo ya mazungumzo hayo kwa sababu, alisema, "tuna jukumu la uaminifu la mpatanishi na mwezeshaji."
Erdogan amesema mara kadhaa kwamba Uturuki haitauweka kando uhusiano wake na Urusi au Ukraine na kusisitiza ina nafasi nzuri ambao, Ankara ina uwezo wa kuzungumza na pande zote mbili.
Uturuki haijaiwekea vikwazo Urusi au kufunga anga yake kwa ndege za Urusi kama nchi nyingine za NATO zilivyofanya.
Njia panda na Utata unaojirudia
Mtaalamu wa Inalco, Ter Minassian Taline anaamini ni muhimu kuonyesha "utata" ambao Uturuki imeonyesha katika mgogoro wa sasa na inaamini kuwa inafaa.
Serikali ya Erdogan haikushirki kupiga kura ya kuunga mkono ama kutounga mkono kusimamishwa kwa kiti cha Urusi katika Baraza la Ulaya, lakini wakati huo huo, iliunga mkono azimio katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kulaani "uchokozi wa Urusi dhidi ya Ukraine."

Chanzo cha picha, Getty Images
Zaidi ya nusu karne iliyopita, baada ya kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, viongozi wa Uturuki waliamua kujiunga na nchi za Magharibi kwa sababu walikuwa na hofu ya Urusi ya Stalin na walitaka "kuwa upande sahihi wa historia."
Ndiyo sababu Rais wa zamani Mustafa İsmet İnönü alihimiza kuingia kwa Uturuki katika taasisi za kama vile NATO.
Leo, Recep Tayyip Erdogan anaonekana kukabiliwa na hali hiyo ya kuwa njia panda. Na, kwa wengi, "utata" wake unaonyesha kwamba amechagua upande wa Magharibi tena, huku akiepuka kusumbua Kremlin.
































