Jiji hatari la chini ya ardhi ambamo mamia ya watu wanaishi

Chanzo cha picha, CHURCHILL ROUND
"Nitaondoka. Nitatafuta kona moja ndanindani kabisa na nitapotelea huko."
Rick haongei tu kwa kujifurahisha. Anamaanisha.
Akiwa amekaa kwenye godoro, akionyesha pango lenye giza ambalo tochi haimruhusu kufahamu kuna nini na kwamba, ikiwa kila kitu kitaenda kama alivyopanga, itaishia kumfuta kabisa kwenye ramani ya dunia.
"Sipatani na watu," anakiri. "Nataka waniache peke yangu."

Chanzo cha picha, CHURCHILL ROUND
Hii ni Las Vegas. Lakini sio Las Vegas "ya kupendeza" inayojitangaza kwa mabango maarufu yakiwemo ya kamari. Hii ni Las Vegas ya chini kwa chini, na ili kukutana na mamia ya wakazi wake unapaswa kushuka ardhini au kushuka kuzimu.
Rick na mipango yake
Akiwa na umri wa miaka 72, Rick ni mmoja wa wakazi wa zamani zaidi wa chini ya ardhi wa kile kinachoitwa "mji mkuu wa pili wa dunia." Anasema kwamba ameishi hapa, kuingia na kutoka kwa miaka 35.
Ili kumfikia mtu huyu mwenye mvi, na masharubu mengi na mwenye sauti ya utulivu na ya kina, lazima ushuke kwenye mfereji ulio mbele ya kasino ya Rio, utakwepa mawe na takataka zilizokusanywa na mafuriko na uingie kwenye moja ya vichuguu vinavyoanzia hapo.
Hizi ni sehemu ya mfumo wa kudhibiti mafuriko wa jiji hili la Marekani. Mvua kubwa zaidi hutokea hasa katikati ya Julai na Septemba, wakati hatari sana wa kuishi kwenye vichuguu vya chini ya ardhi.
"Hata wakati mvua hainyeshi, si mahali pa kuchezea," inaonya Mamlaka ya Kanda ya Udhibiti wa Mafuriko ya Kaunti ya Clark kwenye tovuti yake, chombo kinachosimamia kudumisha na kupanua kila mara miundombinu inayoundwa na mifereji na matanki.

Chanzo cha picha, CHURCHILL ROUND
"Maji yanaweza kupitia mtandao huu wakati wowote. Na kusonga kwa maili 30 kwa saa, yakifika ujazo wa inchi sita tu yanaweza kukusomba."
Ipo mifano mingi ya matukio ya namna hii.
Katika zaidi ya miongo mitatu katika mfumo wa maji taka, Rick amewahi kukumbwa na matukio kama hayo moja kwa moja.
"Niliona maji yakifika karibu na dari," anaiambia BBC Mundo akiegemea ukuta ambao ulionekana kuwa wa kijivu sasa, macho yake yakiwa yamezoea mwanga hafifu wa tochi.

Chanzo cha picha, CHURCHILL ROUND
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Pia anakumbuka nyakati ambazo alijaribu kumsaidia mtu mmoja kuokoa maisha...ingawa hakumbuki tarehe. Lakini kumbukumbu yake inamrejeshwa kwa kukio la kusombwa kwa mwanamke alipokuwa anajaribu kuvuka mkondo wa mfereji bila mafanikio.
"Tulimpigia kelele. Alikuwa amebeba mtoto mgongoni, na hakufanikiwa. Wote wawili walikufa. Ni jambo ambalo sitasahau," anasema kwa huzuni.
Anathibitisha kwamba kwa muda sasa hajashuhudia mafuriko ya kutisha, zaidi anaorodhesha masuala mengine ambayo yanamtia wasiwasi zaidi: panya "wa ukubwa unaotisha mtu yeyote", polisi na idadi inayoongezeka ya watu.
Anasema ameishia kuishi hapa kutokana na maisha yake ya zamani akiwa kama mwanajeshi. Yamekuwa kikwazo chake kikubwa katika miongo hii kupata maisha ya maana.
"Nilikuwa Vietnam, nilitumia miaka mitatu kuishi kwa shida au kuzimu na hiyo iliniletea matatizo ya kiakili," anaeleza. Aliishia kuondolewa kwenye kikosi cha Wanamaji kwa utovu wa nidhamu baada ya kufyatua risasi bila kupewa ruksa.
Baadaye, katika maisha yake ya kiraia, alifanya kila kitu: "Nilijaribu shughuli za uchunguzi, ujenzi, nilifungua kasino, niliendesha teksi.. . Kulikuwa na wakati ambapo ningeweza kufanya kazi, lakini maisha yaliniletea shida na kuishia kuacha".
Leo anaishi kwa dola 23 za Marekani ambazo hupokea tarehe 3 ya kila mwezi na kwa takrima ama vipesa vya hapa na pale, huku aishi kuzoea ukweli kwamba watu wengi zaidi wanakimbilia kwenye handaki lake.
"Sababu iliyonifanya kukaa katika eneo hili kwa miaka mingi ni kwa sababu nilijua watu. Lakini sasa kuna wapya na sijihusishi nao kabisa… sitangamani na mtu yeyote… nimekuwa mtu mpweke."
"Ndio, wewe ni mpweke!" sauti inaita kutoka gizani, ikitushtua.
Tunamulika tochi. Kuna mwanaume aliyekonda sana amelala kwenye kipande cha mbao yapata mita nne kutoka tulipo.
"Ni Glenn. Tumefahamiana kwa takriban miaka 15," Rick anatuambia. Ni pamoja naye kwamba ana nia ya kuingia ndani ya kina cha handaki (jiji). "Twende tukapotelee huko" .
Jay au utambulisho uliopotea
Tunamuaga Rick, tukampita mwenziwe (Glenn), ambaye sasa anaonekana amelala, na kuendelea kuzama ndani zaidi kwenye handaki.
Tunavuka sehemu zilizojaa maji, ingawa mvua haijanyesha kwa wiki kadhaa, tunakwepa uchafu na kuona tandabui zinazoning'inia kwenye dari ya saruji. Kwa bahati nzuri, hakuna dalili ya panya wa ukubwa wa paka ambao Rick alitufahamisha.

Chanzo cha picha, RONDA CHURCHILL
Tunatembea kwa kasi kwa dakika nyingine 10 hadi tufike kwenye kona moja ya ukuta, ambayo tunakutana kumening'inizwa soksi, kitambaa, na mfuko wa plastiki.
"Ninakuja. Ninafunga viatu vyangu ili vionekane," inasema sauti ya taratibu kutoka ndani ya mkondo mwingine wa pango.
Ni Jay na anaonekana kufurahishwa na ugeni huo, yuko tayari kupigwa picha. “Hata nimejipodoa,” anatania.
Ana "takriban umri wa miaka 47" na aliwasili Las Vegas miaka 14 iliyopita kwa basi kutoka New Hampshire, jimbo la mbali kaskazini-mashariki mwa Marekani.
"Nani angefikiria kwamba mara moja hapa wangeiba pasipoti yangu, kadi yangu ya Hifadhi ya Jamii, kila kitu, na kwamba ningebaki na dola $ 27 mfukoni mwangu?"
Anasema kuwa haijalishi amejitahidi vipi kwa miaka mingi, hajaweza kupata kitambulisho chake na ndio maana amekuwa akiishi katika mfumo huo wa mifereji ya maji wa Sin City kwa miaka tisa iliyopita.
Hilo ndilo toleo la muhtasari wa hadithi inayojirudia-rudia na yenye mkanganyiko. Jay ni muongeaji na ni vigumu kuendelea kuwa naye sawa na kuangalia mbali jicho lake moja bovu la kushoto ambalo lilitoka kwa kupigwa risasi ya kichwa.
Robert na "mawazo ya kikabila"
Kulingana na takwimu za serikali ya jiji, zaidi ya wakaazi 6,500 wa Las Vegas hawana makazi ya kudumu.
Na mashirika yanayofanya kazi na watu wasio na makazi yanakadiria kuwa hadi watu 1,500 wanaishi kwenye vichuguu, mifereji na mapango.
"Lengo la jiji sio kuwakamata watu wasio na makazi. Lengo la jiji ni kufanya kazi na watu wasio na makazi kuwasaidia kuwa na afya njema, kuwa na makazi na waweze kuajiriwa," alisisitiza msemaji wa serikali ya manispaa ya Las Vegas.
Jiji la Las Vegas ni mojawapo tu ya mamlaka kadhaa zinazounda eneo la jiji ambalo hutoa huduma kwa watu wasio na makazi.

Chanzo cha picha, RONDA CHURCHILL
Robert Banghart, ambaye leo ni mkurugenzi wa mawasiliano wa Shine A Light, alipitia kile anachopendelea kuiita "ukanda wa kukata tamaa" na pia aliishi chini ya ardhi.
"Niliamua kuingia kwenye mifereji ya maji kwa sababu mtu ambaye alikuwa akilala huko alinialika. Nimekuwa nikiishi mitaani kwa miaka mingi, ambapo kila kitu ni hakieleweki: … Kwa hiyo nilipoenda kule chini nilihisi kitu sawa na kile ninachohisi sasa ninaporudi nyumbani , "anaiambia BBC Mundo huku tukirudi kwenye mlango wa handaki la Rio.
"Mbali na hilo hakuna mtu anayekuona au kukusumbua," Robert anaendelea, akirudia yale ambayo tayari tumesikia kutoka kwa Rick na Jay wakisema.
Hakika wao hawalindwi wala hawafukuzwi au kukamatwa. Idara ya Polisi ya Jiji la Las Vegas (LVMPD) iliithibitishia BBC kwamba wanafanya kazi na mashirika yanayofanya kazi na watu wasio na makazi na kwamba haya ndiyo yenye jukumu la kuwaonya wakazi wanaoishi kwenye mapango na mifreji kuhusu hatari ya kuishi humo na kuwapa rasilimali za kufanya mabadiliko ya makazi yao.
Ilichukua miaka Robert kuchukua hatua hiyo na kubadilika.
Beverly na jamii yake
Tunaliona likitenda kazi tunapokuwa nje katika ulimwengu wa nje na kukutana na Beverly kwenye mlango wa mtaro unaopakana.

Chanzo cha picha, RONDA CHURCHILL
Mrembo na mwembamba, mwenye ngozi iliyoathirika na hali ya hewa na hana baadhi ya meno, ametoka tu kuweka kitu ambacho hatuwezi kuona kwenye sufuria akipika na kuning'iniza nguo chache.
Anatuambia kwamba anatoka jimbo la Mississippi, lakini siku moja alikutana na mvulana ambaye alimwambia "twende tusafiri." Bila kujua, waliishia Las Vegas. Ana umri wa miaka 44 na amekuwa katika handaki hili kwa miaka sita.
- Darling, na wewe, unatoka lini? Robert anauliza.
- Sijui. Si rahisi. Naweza kukuambia tu kwamba leo sitoki.
— Kumbuka kwamba tunaweza kukusaidia. Ikiwa umeweza kufika hapa, unaweza kufanya hivyo popote.

Chanzo cha picha, RONDA CHURCHILL
Kabla hatujaondoka, Beverly anatuambia kwamba anahisi kuwa sehemu ya jumuiya ya hapo.
"Handaki la kwanza zuri sana," anasema, akionyesha baadhi ya majirani ambao hukasirika na kututazama kwa nje kutoka umbali wa mita chache.
"Pango" la Steve
Hiki ndicho kisa cha handaki linalojulikana kama Ali Baba's, lililoko katika eneo la viwanda magharibi mwa Ukanda huo. Ingawa anayetoka kwenye pango hili ni Steve.































