Koletha Kakuru: 'Nilijisaidia haja kubwa kupitia njia ya haja ndogo"

Waswahili walisema hujafa hujaumbika. Usemi huo wa busara ya Kiswahili ulidhihirika mnamo mwaka 2019 kwenye Maisha ya Koletha, ambaye alikuwa na umri wa miaka 20 tu, yalibadilika kabisa baada ya kujifungua mtoto wake wa kwanza. Kwa bahati mbaya, wiki moja tu baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, alianza kushuhudia mabadiliko yasiyo ya kawaida katika mwili wake – alianza kujisaidia haja kubwa kupitia njia ya haja ndogo, hali iliyomshtua sana.
Fuatilia Makala hii kwa kina iliyoandaliwa na Hilder Ngatunga wa BBC Media Action.
"Nilishtuka sana. Hata ndugu zangu walishangaa, hawakuwa wamewahi kuona tatizo kama hili," anasema Koletha kwa huzuni.
Kabla hata ya kupata jibu la matatizo hayo kiafya, alikumbana na tuhuma na maswali kutoka kwa mama yake ambaye alidhani huenda tatizo hilo limesababishwa na kufanya mapenzi akiwa bado mdogo au kufanya kazi ngumu akiwa na umri mdogo. Kauli hizo zilimvunja moyo zaidi na kuongeza msongo wa mawazo.
Wakati hali hiyo ikiendelea kuzidi kuwa mbaya, alijikuta akitengwa na familia na jamii. "Awali walikula pamoja nami, lakini baadaye wakaanza kuniepuka. Wifi yangu alikuwa anafunga mlango wa chumba chake ili nisiingie na kuacha harufu. Hata wageni wakija, alihakikisha sipo karibu nao," anasimulia kwa uchungu Koletha.
Kutengwa na kuchekwa kulimvunja moyo na kumnyima hali ya kujiamini. Wapo waliomshutumu kuwa anafanya makusudi, bila kuelewa kuwa alikuwa hana uwezo hata wa kujizuia. Katika harakati za kutafuta tiba, kaka yake alimshauri kwenda kwa mganga wa kienyeji akiamini labda amerogwa. Lakini alipofika kwa mganga huyo, hakumkuta, na ndipo alipofanya uamuzi wa kwenda hospitali.
Taarifa za matumaini kwa Koletha

Baada ya miezi kadhaa ya mateso, mama mlezi aliyekuwa akiishi naye Dar es Salaam alimueleza kuwa tatizo lake linaweza kutibiwa hospitalini. Hatimaye Koletha alikwenda hospitali na baada ya uchunguzi, alipewa rufaa ya kwenda Mwanza na baadaye hospitali ya CCBRT jijini Dar es Salaam, ambako alianza matibabu.
"Nilipofika hospitalini nilijiona mwenye thamani tena, hasa baada ya kuwaona wasichana na wanawake wengine waliokuwa na tatizo kama langu. Nilijua kuwa mimi si wa kwanza wala wa mwisho," anasema Koletha kwa matumaini.
Tangu aanze matibabu, hali yake imeimarika sana na sasa anaweza kuchangamana na wengine kama awali. Ingawa bado hajawasiliana tena na baadhi ya ndugu waliomtenga, anatamani kuwaambia kuwa tatizo lake lilikuwa la kawaida na linatibika.
"Nataka kuwa balozi wa kutoa elimu kuhusu Fistula. Jamii isiwatenge wanawake wanaopitia hali hii, bali iwaunge mkono katika safari ya kupona," anasisitiza.
Kupitia kituo cha Mabinti Center kilichopo CCBRT, Koletha amepata mafunzo ya ushonaji ili kumwezesha kujitegemea baada ya matibabu hatua inayolenga kurejesha furaha yake binafsi na wanawake waliowahi kupitia tatizo la Fistula.

Chanzo cha picha, BBC Media Action
Watalaam wanasema nini juu ya fistula?

Chanzo cha picha, BBC Media Action
Fistula ni jeraha au shimo linalojitokeza kati ya kibofu cha mkojo na njia ya uzazi, mara nyingi kutokana na matatizo wakati wa kujifungua. Daktari Timothy Mushi kutoka CCBRT anasema kuwa matibabu ya Fistula hufanyika kwa njia ya upasuaji, na hutegemea aina ya fistula na ukubwa wa tatizo.
Kundi lililo kwenye hatari kubwa ni wasichana walio chini ya miaka 20 ambao nyonga zao huwa hazijakomaa vya kutosha kustahimili uchungu na mikikimikiki ya kujifungua. Hata hivyo, tatizo hili linaweza kuzuilika kwa kuwaelimisha wasichana kuepuka ujauzito wakiwa na umri mdogo, na kwa jamii kuhamasika kuhusu umuhimu wa kuhudhuria kliniki na kujifungulia hospitalini.Hata hivyo kampeni zaidi inahitaji ili wanawake wengi na jamii waweze kuwa na ueledi ili kutowatenga wenye matatizo haya kama ilivyotokea kwa Koletha.
































