Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu: Tulifikaje hapa?
Hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, itatolewa Ijumaa tarehe 6 Novemba, 2026. Kesi hiyo inafuatiliwa kwa karibu ndani na nje ya nchi kutokana na uzito wa mashtaka yanayomkabili na athari zake katika mazingira ya kisiasa ya Tanzania.
Ufuatao ni msururu wa matukio muhimu kuelekea kukamatwa kwa Tundu Lissu na kufikishwa Mahakamani kwa shitaka la uhaini na namna kesi hiyo ilivyofika hatua ya kusubiri hukumu.
Januari 2025: Lissu achukua uongozi wa CHADEMA
Mnamo Januari 2025, Tundu Lissu alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA.
Kuchaguliwa kwake kulikuja wakati ambapo chama hicho kilikuwa kikijipanga kuelekea uchaguzi mkuu na kusisitiza ajenda ya mageuzi ya mfumo wa uchaguzi.
Wafuasi wake waliona ujio wake kama mwanzo wa kampeni kali zaidi ya kudai mabadiliko ya kisiasa nchini
Januari - Machi 2025: CHADEMA yazindua kampeni ya "No Reforms, No Election"
Chini ya uongozi wa Lissu, CHADEMA ilianzisha kampeni ya kitaifa iliyopewa jina la"No Reforms, No Election" (Hakuna Mageuzi, Hakuna Uchaguzi).
Chama hicho kilidai kuwa mfumo wa uchaguzi uliokuwepo haukuwa huru wala wa haki na kushinikiza mabadiliko ya sheria, tume ya uchaguzi na mifumo mingine ya usimamizi wa uchaguzi kabla ya kura kupigwa.
Kampeni hiyo ilifanyika kupitia mikutano ya hadhara, semina na mikutano ya ndani ya chama nchini kote.
Kampeni ya "No Reforms, No Election"
Kadiri kampeni ya "No Reforms, No Election"" ilivyoendelea, tofauti za kimtazamo zilijitokeza ndani ya CHADEMA kuhusu ushiriki wa chama katika uchaguzi bila mageuzi. Wakati baadhi ya wanachama waliunga mkono msimamo wa chama, wengine walihofia kuwa kususia uchaguzi kungekipunguzia chama ushawishi wa kisiasa.
Wito wa mazungumzo ulitolewa na baadhi ya wadau, lakini mjadala uliendelea huku ukiongeza mvutano wa kisiasa kuelekea kukamatwa kwa Tundu Lissu tarehe 9 Aprili 2025
3 Aprili 2025: Hotuba iliyozua kesi
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, alitoa kauli katika mkutano wa CHADEMA jijini Dar es Salaam ambazo baadaye zilitafsiriwa na upande wa mashtaka kuwa zilikuwa na lengo la kuhamasisha kuzuiwa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Kauli hizo ndizo msingi wa shtaka la uhaini.
Lissu amesisitiza kuwa kauli zake zilihusu mapambano ya kisiasa ya kudai mageuzi na si wito wa kuipindua serikali.
Aprili 9, 2025: Lissu akamatwa Mbinga
Polisi walimkamata Lissu mjini Mbinga mkoani Ruvuma baada ya kuhutubia mkutano wa kisiasa wa CHADEMA uliokuwa sehemu ya kampeni ya mageuzi ya uchaguzi.
Aprili 10, 2025: Afikishwa Mahakamani na kushtakiwa kwa uhaini
Tundu Lissu alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa shitaka la uhaini pamoja na mashtaka mengine ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni. Uhaini ni kosa lisilo na dhamana nchini Tanzania.
Aprili - Mei 2025: Malalamiko kuhusu mwenendo wa kesi
Kuna mjadala kuhusu upatikanaji wa mahakama kwa umma, hatua za usalama na namna kesi inavyoendeshwa. Mashirika mbalimbali ya haki za binadamu yanaeleza wasiwasi wake kuhusu mazingira ya kesi hiyo.
Msimamo wa Serikali
Serikali ya Samia Suluhu Hassan imeendelea kusisitiza kuwa vyombo vya dola vinafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kwamba serikali inaheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria. Serikali imekanusha tuhuma za kulenga wapinzani kisiasa.
2025-2026: Kesi yaingia Mahakama Kuu
Baada ya hatua za awali katika Mahakama ya Kisutu, kesi iliendelea katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Mabishano yaliibuka kuhusu ushahidi, mashahidi waliolindwa na taratibu mbalimbali za kisheria, huku baadhi ya hoja zikifikishwa hadi Mahakama ya Rufaa.
21 Agosti 2026 Mahakama: Lissu ana kesi ya kujibu
Jopo la majaji watatu katika Mahakama Kuu liliamua kuwa upande wa mashtaka umewasilisha ushahidi wa kutosha kuhitaji kujitetea.
Mahakama iilifafanua kwamba uamuzi huo haukumaanishi amepatikana na hatia.
Septemba 2026: Utetezi wakamilika
Lissu alimaliza kuwasilisha utetezi wake na kudai kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kosa la uhaini. Nao waendesha mashtaka wanasisitiza kuwa ushahidi wao umethibitisha shtaka hilo pasipo shaka ya msingi.
Novemba 6, 2026 - Hukumu kusubiriwa
Mahakama Kuu ya Tanzania inatarajiwa kutoa hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu tarehe 6 Novemba 2026, baada ya kusikiliza ushahidi na hoja za mwisho kutoka kwa upande wa mashtaka na utetezi.
Hukumu hiyo itahitimisha mchakato wa kisheria uliodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja tangu kukamatwa kwa kiongozi huyo wa upinzani mwezi Aprili 2025. Kutokana na uzito wa shitaka linalomkabili na nafasi yake katika siasa za Tanzania, uamuzi wa mahakama unafuatiliwa kwa karibu na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Kesi hiyo imekuwa mojawapo ya mashauri yaliyoibua mjadala mkubwa kuhusu siasa, demokrasia na utawala wa sheria nchini Tanzania, huku pande zote zikisubiri uamuzi wa mwisho wa mahakama kuhusu tuhuma zinazomkabili Lissu.
Kwa nini kesi hii ni muhimu?
Ke si hii inamhusu kiongozi mkuu wa upinzani nchini Tanzania.
Shitaka la uhaini ni miongoni mwa makosa mazito zaidi kisheria na linaweza kuadhibiwa kwa hukumu ya kifo.
Pia imeibua mjadala mkubwa kuhusu uhuru wa kisiasa, haki za kiraia na mageuzi ya uchaguzi nchini Tanzania.
Kesi hiyo imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu na serikali, upinzani na wadau wengine wanahisi matokeo yake yanaweza kuwa na athari katika mustakabali wa demokrasia nchini.