Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amwita Putin ‘muuaji’ baada ya Trump kumtaja kuwa ‘rafiki’ yake
Rais wa Ukraine, amemtaja Rais wa Urusi Vladimir Putin, kuwa ni "muuaji", akijibu matamshi ya Donald Trump aliyemtaja kiongozi huyo wa Urusi kuwa "rafiki" yake.
Muhtasari
- Shambulizi dhidi ya daraja la Crimea lilikuwa jibu la haki - Zelensky
- Wadukuzi walenga hifadhidata ya FBI katika shambulio la kimtandao
- Zohram Mamdani: Kijana wa Ghana aliyeuawa Marekani alistahili maisha bora zaidi.
- Meli ya kubeba mafuta yashambuliwa karibu na Oman
- Saudi Arabia yazuia shambulio la Wahouthi mjini Riyadh
- Gharama za Manchester United kuajiri na kufukuza makocha zakaribia pauni milioni 100
- Iran imesema imedungua droni ya Marekani aina ya MQ-9
- Trump asema bei ya mafuta itashuka hivi karibuni
- Trump apiga marufuku ujenzi wa vituo vya AI nje ya Marekani
- Rais wa Ukraine amtaja Rais wa Urusi kuwa 'muuaji'
Moja kwa moja
Na Beldeen Waliaula
Shambulizi dhidi ya daraja la Crimea lilikuwa jibu la haki - Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametetea mashambulizi ya Kyiv dhidi ya daraja muhimu linaloiunganisha Urusi na eneo la Crimea linalokaliwa na Urusi.
Zelensky ametaja shambulizo hilo kuwa "jibu la haki" kufuatia mashambulizi 109 tofauti ya Urusi dhidi ya madaraja nchini Ukraine.
Akizungumza na BBC mjini Kyiv, Zelensky amesema mashambulizi makali ya Urusi dhidi ya Ukraine yaliyofuata mashambulizi dhidi ya Daraja la Crimea ni "ishara tu kwamba Vladimir Putin hataki kusitisha vita. Anataka kupata sababu ya kuendelea kupigana".
Zelesnky amepinga madai ya Rais wa Urusi kwamba daraja hilo, linaloiunganisha Urusi na rasi ya Crimea ambayo awali ilikuwa sehemu ya Ukraine, ilikuwa ikitumiwa kwa shughuli za kiraia pekee.
Rais huyo wa Ukraine alielekeza kwenye picha zinazosambaa mtandaoni zinazoonyesha vifaru na vifaa vingine vya kijeshi vya Urusi vikitumia daraja hilo kusafirisha vifaa na kurahisisha shughuli za kijeshi kuelekea Crimea inayokaliwa na Urusi.
"Kama Putin angekuwa anatumia intaneti, angeweza kuona hilo," alisema.
Zelensky aliongeza kuwa Urusi imekuwa ikifanya mashambulizi dhidi ya madaraja nchini Ukraine kwa kutumia makombora na droni.
Soma pia:
Wadukuzi walenga hifadhidata ya FBI katika shambulio la kimtandao
Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) linafanya uchunguzi kuhusu uwezekano wa kudukuliwa kwa hifadhidata yake ya taarifa za uhalifu.
Hifadhidata hiyo inayojulikana kama National Crime Information Center (NCIC), hutumiwa na vyombo vya usalama vya serikali ya shirikisho na serikali za mitaa kubadilishana taarifa kuhusu hati za kukamatwa kwa washukiwa pamoja na ukaguzi wa historia za watu.
BBC imewasiliana na FBI kutaka maoni yake kuhusu tukio hilo.
Tukio hilo linajiri baada ya hitilafu kadhaa za mifumo ya teknolojia kuathiri sekta za benki, udhibiti wa safari za ndege na sekta nyingine nchini Marekani wiki iliyopita.
Maafisa wamesema hitilafu hizo hazikusababishwa na mashambulizi ya kimtandao, lakini zimeibua maswali kutoka kwa wabunge kuhusu usalama na uimara wa mifumo hiyo.
Mkurugenzi wa masuala ya usalama wa kimtandao katika Ikulu ya White House, Sean Cairncross, alifutwa kazi wiki hii, huku Rais wa Marekani Donald Trump akisema hakuwa na uwezo wa kutosha kutekeleza majukumu yake.
Hii si mara ya kwanza kwa wadukuzi kulenga FBI, shirika la Marekani linalohusika na upelelezi na usalama wa ndani ya nchi.
Mwezi Septemba, FBI ilisema ilikuwa inachunguza uwezekano wa kudukuliwa kwa mifumo yake na kundi la wahalifu wa kimtandao linalojulikana kama ShinyHunters.
Kundi hilo lilidai kuiba taarifa nyeti za wafanyakazi wote wa shirika hilo, ambao wanakadiriwa kuwa takriban 38,000.
Katika tukio jingine tofauti, shirika la habari la NBC limeripoti kuhusu uwezekano wa shambulizi la kimtandao dhidi ya Wizara ya Kilimo ya Marekani (USDA).
Zohram Mamdani: Kijana wa Ghana aliyeuawa Marekani alistahili maisha bora zaidi.
Kijana mwenye umri wa miaka 15 kutoka Ghana aliyeuawa nchini Marekani mwezi uliopita amekumbukwa kama mwanafunzi mwenye bidii aliyekuwa na ndoto ya kuwa daktari.
Hayo yamesemwa wakati wa mazishi yake siku ya Ijumaa, yaliyohudhuriwa na baba yake, Meya wa Jiji la New York Zohram Mamdani na viongozi wa kutetea haki za kiraia, ambao walitoa hotuba za kumuenzi.
Javits Frimpong alipigwa risasi na kuuawa alipokuwa akitembea kuelekea shuleni katika eneo la Bronx,New York. Kifo chake kimezua hasira nchini Ghana na Marekani, na kuibua tena mjadala kuhusu ukatili wa kutumia silaha nchini Marekani.
"Javits alistahili maisha bora zaidi, na kila mmoja wenu pia anastahili," alisema Meya wa New York, Zohran Mamdani.
"Ingawa alikuwa mkazi wa New York kwa muda mfupi tu, jiji hili litajivunia daima kumtambua Javits kama mmoja wetu."Frimpong alihamia Marekani takriban mwaka mmoja kabla ya kupigwa risasi.
"Baba yake, Thomas Frimpong, alisema: "Nilifanya kazi kwa bidii ili kukuleta kutoka Ghana hadi Marekani kwa sababu nilitaka upate fursa, maisha bora ya baadaye na nafasi ya kutimiza ndoto zako zote."
Mama yake alipewa visa ya dharura kutoka Ghana ili aweze kuhudhuria mazishi ya mwanawe siku ya Ijumaa, kufuatia juhudi za Mamdani kumshawishi Rais Donald Trump mapema mwezi huu.
Mapema mwezi huu, mama huyo aliiambia BBC kuwa alitaka "haki kwa mwanangu" — kauli ambayo pia ilijitokeza katika hafla ya mazishi.Maafisa wamesema wanachunguza sababu kadhaa zinazoweza kuwa zilichangia mauaji hayo. Familia ya Frimpong imesema alikuwa akidhulumiwa na wanafunzi wenzake shuleni, madai ambayo polisi wamesema wanayachunguza.
Frimpong alifuatiliwa na kushambuliwa kwa risasi tarehe 29 Oktoba. Alipelekwa katika hospitali ya eneo hilo ambako alitangazwa kuwa amefariki.
Polisi wamesema vijana watatu walihusika katika shambulio hilo. Kijana mmoja mwenye umri wa miaka 17 amekamatwa na kufunguliwa mashtaka ya mauaji, na atafikishwa katika mahakama ya watu wazima. Polisi bado wanawatafuta vijana wengine wawili.
Serikali ya Ghana imelaani mauaji hayo na kusema itafuatilia kwa karibu kesi hiyo ili kuhakikisha haki inatendeka.
Serikali hiyo imezitaka mamlaka za Marekani kufanya uchunguzi wa kina na kusema iko tayari kutoa msaada wa kisheria na kibalozi ili kuhakikisha waliohusika wanachukuliwa hatua za kisheria.
Meli ya kubeba mafuta yashambuliwa karibu na Oman
Meli ya kubeba mafuta iliyokuwa ikisafiri kutoka katika Mlango Bahari wa Hormuz imeshambulia katika sehemu yake ya nyuma na kifaa kisichojulikana, takriban maili 11 za baharini kaskazini mwa eneo la Khasab nchini Oman, Shirika la Uendeshaji Biashara za Baharini la Uingereza (UKMTO) limesema.
Hakuna majeruhi walioripotiwa, huku athari za tukio hilo kwa mazingira zikiwa bado hazijafahamika.
Khasab iko katika Rasi ya Musandam nchini Oman, kwenye lango la kuingia katika Mlango Bahari wa Hormuz.
Njia hiyo muhimu ya kimkakati ilikuwa ikipitisha karibu asilimia tano ya mafuta ghafi yanayotumika duniani kabla ya kuanza kwa mzozo wa kijeshi kati ya Marekani, Israel na Iran.
Usafirishaji wa bidhaa kupitia njia hiyo umekumbwa na misukisuko tangu Iran ilipochukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran Februari 28.
Soma pia:
Saudi Arabia yazuia shambulio la Wahouthi mjini Riyadh
Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umesema umedungua makombora matatu ya masafa marefu yaliyorushwa na waasi wa Houthi nchini Yemen, wakilenga mji mkuu wa Riyadh.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, muungano huo umesema mifumo ya ulinzi wa anga ya Saudi Arabia ilifanikiwa kuyatambua, kuyazuia na kuyadungua makombora yote matatu, na kufanikiwa kuzuia jaribio la kushambulia mji mkuu huo.
Kwa upande mwingine, waasi wahouthi nao walidai katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X kuwa walikuwa wamelenga maeneo mbalimbali nchini Saudi Arabia, yakiwemo makazi ya mji mkuu wa Riyadh.
Hapo jana, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ulifanya mashambulizi katika bandari ya Hodeidah na maeneo mengine katika pwani ya Yemen inayopakana na Bahari Nyekundu. Muungano huo ulielezea mashambulizi hayo kuwa "operesheni maalumu".
Waasi wa Houthi walitishia kulipiza kisasi kutokana na mashambulizi hayo.
Mapigano katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen yameongezeka tena katika wiki za hivi karibuni, huku mashambulizi ya wahouthi dhidi ya Saudi Arabia yakiongezeka.
Soma pia:
Gharama za Manchester United kuajiri na kufukuza makocha zakaribia pauni milioni 100
Manchester United imekopa pauni milioni 10 siku tatu baada ya kumtangaza Mauricio Pochettino kuwa kocha wake mkuu mpya.
Katika taarifa ya kina iliyowasilishwa kwa soko la hisa ikiambatana na matokeo ya kifedha ya robo ya kwanza ya mwaka, klabu hiyo ilisema italazimika kulipa fidia ya pauni milioni 7.5 kwa Shirikisho la Soka la Marekani ili kumpata kocha huyo kutoka Argentina.
Manchester United ilitangaza tarehe 13 Novemba kuwa Pochettino amekubali mkataba wa miaka miwili na nusu. Siku tatu baada ya klabu hiyo kukopa pauni milioni 10.
Mkopo huo ni miongoni mwa mikopo mitatu iliyothibitishwa baada ya tarehe 30 Septemba, na imepandisha jumla ya deni la klabu hiyo kufikia pauni milioni 240.
Malipo ya kumwachia Pochettino kutoka kwenye mkataba wake na Marekani yamepandisha jumla ya fedha zilizotumika kuajiri na kuwafuta kazi makocha tangu Sir Alex Ferguson alipostaafu mwaka 2013 hadi pauni milioni 95.
Hata hivyo, kiasi hicho kinatarajiwa kuzidi pauni milioni 100 baada ya kujumlisha gharama za kuajiri benchi la ufundi la Pochettino na kumfuta kazi Michael Carrick.
Carrick alitimuliwa wiki iliyopita wakati Manchester United ilikuwa katika nafasi za kushushwa daraja, huku ikikabiliwa na mwanzo mbaya zaidi wa msimu ndani ya miaka 40.
Pochettino ni kocha wa tisa wa kudumu kuteuliwa na Manchester United tangu Ferguson astaafu, akiwemo Ralf Rangnick aliyeteuliwa Novemba 2021.
Manchester United imekuwa ikibadilisha makocha katikati ya misimu katika misimu yake mitatu iliyopita.
Soma pia:
Iran imesema imedungua droni ya Marekani aina ya MQ-9
Jeshi la Iran (IRGC), limedai kuwa mfumo wake wa ulinzi wa anga umedungua droni ya Marekani aina ya MQ-9 iliyokuwa ikiruka juu ya Mlango Bahari wa Hormuz.
Kulingana na idara ya mahusiano ya umma ya jeshi hilo, mfumo wa ulinzi wa anga uliitambua droni hiyo, ukaifuatilia na kisha kuilenga.
Katika taarifa yake, jeshi hilo lilisema kuwa hiyo ni droni ya 58 ya Marekani aina ya MQ-9 ambayo wameilenga.
Hata hivyo, maafisa wa Marekani bado hawajatoa tamko lolote kuhusu madai hayo, huku kukiwa hakuna uthibitisho huru kwamba droni hiyo imedunguliwa.
Soma pia:
Trump asema bei ya mafuta itashuka hivi karibuni
Rais wa Marekani Donald Trump amesema bei ya mafuta ilikuwa nafuu kabla ya kuanza kwa operesheni ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iran, na kutabiri kuwa bei za mafuta zitashuka kwa kiasi kikubwa hivi karibuni.
"Mtashuhudia bei za chini sana hivi karibuni," alisema Trump katika mkutano na waandishi wa habari hapo jana.
Rais huyo wa Marekani aliongeza kuwa bei ya mafuta kuanzia sasa itategemea jinsi Marekani itakavyotatua mizozo yake na Iran.
Trump alisisitiza kuwa Iran inataka kufikia makubaliano na Marekani, lakini haiko tayari kukubali masharti ya Marekani.
"Tunataka kufikia makubaliano ya kweli, si makubaliano ya uongo," alisema.
Soma pia:
Trump apiga marufuku ujenzi wa vituo vya AI nje ya Marekani
Rais wa Marekani Donald Trump, amesema atapiga marufuku kampuni za Marekani kujenga vituo vya kuhifadhi na kuchakata data za akili unde (AI) nje ya nchi hiyo.
Trump amesema kmapuni zitakazokiuka sera hiyo zitatozwa kodi kubwa.
"Tutahakikisha shughuli zote hizo zinafanyika ndani ya nchi hii," alisema Trump, bila kutoa maelezo ya kina kuhusu sera hiyo inayopendekezwa.
Vituo vya kuhifadhi na kuchakata data au data centres vilikuwa miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa sana katika uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani mapema mwezi Novemba, huku wagombea wengi wa chama cha Democratic wakiahidi kuweka masharti makali zaidi kuhusu ujenzi wake.
Kampuni kubwa za teknolojia, zikiwemo Meta na Google, tayari zimesaini mikataba ya kujenga vituo hivyo katika nchi za nje. Hata hivyo, bado haijabainika jinsi sheria hiyo itakavyotekelezwa iwapo itapitishwa.
"Tutazizuia kampuni zetu kujenga vituo vya data nje ya nchi yetu, kwa sababu China itavichukua vyote, na hatutaruhusu hilo kutokea," Trump aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano mfupi baada ya kurejea kutoka ziara yake barani Asia.
Hata hivyo, bado haijafahamika iwapo wazo hilo litabadilika na kuwa sera rasmi.
Soma pia:
Zelensky amwita Putin kuwa ‘muuaji’ baada ya Trump kumtaja kuwa ‘rafiki’
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amemtaja Rais wa Urusi Vladimir Putin, kuwa ni "muuaji", akijibu matamshi ya Rais wa Marekani Donald Trump aliyemtaja kiongozi huyo wa Urusi kuwa "rafiki" yake alipokuwa China wiki hii.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha CNN, Zelensky alisema kuwa "kwetu sisi,Putin ni adui kwetu sisi, yeye ni muuaji".
Pembeni mwa mkutano wa kihistoria wa pande tatu kati ya Trump, kiongozi wa China Xi Jinping na Putin siku ya Alhamisi, Trump alimtaja Putin kuwa "rafiki" yake na kusema viongozi hao wawili wamekuwa na "uhusiano mzuri kwa miaka mingi".
Zelensky alielezea mashambulizi ya hivi karibuni ya Urusi dhidi ya Ukraine kuwa makubwa zaidi kuwahi kutokea mwaka huu. Alisema mashambulizi hayo yalisababisha vifo na majeruhi miongoni mwa raia, baada ya Urusi kurusha makombora 110, yakiwemo 27 ya masafa mafupi ya balistiki, pamoja na zaidi ya droni 400.
Saa chache baada ya mashambulizi hayo nchini Ukraine, Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House kwamba Putin "angependa kumaliza vita".
"Wote wawili Zelensky na Putin wanataka vita vikome, na ni jambo zuri sana kwamba nina uhusiano nao," alisema Trump siku ya Ijumaa.
Takriban watu tisa waliuawa katika mashambulizi ya Urusi yaliyolenga madaraja mjini Kyiv na vituo vya reli siku ya Ijumaa, siku chache baada ya Ukraine kuharibu vibaya Daraja la Crimea.
Hata hivyo, Zelensky alisema licha ya msimamo wa Trump, yeye anamwona Putin kuwa "muuaji".
"Nadhani watu wengi duniani wanamwona kuwa muuaji kwa sababu anaua watu kila siku na kila usiku," alisema.
Mabadilishano hayo ya matamshi makali yalijiri wakati Poland, nchi jirani ya Ukraine, ilipotangaza kuwa kombora la Urusi aina ya cruise lilikuwa miongoni mwa vitu vitatu vilivyoingia katika anga yake katika eneo la kusini-mashariki mwa nchi hiyo mapema siku ya Ijumaa.
Soma pia:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja